Habari za Punde

Vijana Watakiwa Mabega yao Kutowabeba Viongozi Wanaovuruga Shughuli za Serekali.x

Na Mwantanga Ame
WANACHAMA wa Umoja Vijana wa CCM, wametakiwa mabega yao kutowabeba viongozi wanaovuruga shughuli za serikali, na badala yake wawaumbue kwa kutowapa kura ndani ya chaguzi za Chama zinazoendelea kwa vile tayari wameanza kutembeza fedha ili kupanga safu yao.

Hayo yalisemwa jana na Mjumbe wa Kamati ya Siasa Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja, Mama Asha Suleiman Iddi, katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Vijana Tanzania Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja, ikiwa ni sehemu ya uchaguzi Mkuu wa ngazi hizo unaoendelea kufanyika nchini kote Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi.

Mama Asha, alisema UVCCM, ni moja ya Jumuiya muhimu ndani ya Chama na haitakuwa busara kwa wanachama wake kuona wanakubali kutumiwa kuwapitisha viongozi ambao tayari wameonesha dalili za kuvuruga utekelezaji wa shughuli za serikali.

Alisema katika siku za karibuni baadhi ya viongozi wameonekana kwenda kinyume na matakwa ya sera na mipango ya serikali, jambo ambalo linaonesha kuwa hawako tayari kuisaidia serikali yao ili iweze kufikia malengo iliyojipangia .

Alifahamisha kutokana na mazingira ya kutambulika kwa viongozi hao tayari kuna taarifa za kuanza kupanga safu ndani ya chaguzi hizo ikiwa ni hatua ya kuwawezesha watu wanaotaka kuendelea kushika madaraka ndani ya chama hicho.

Alisema ili kuiondoa hali hiyo ni vyema kwa wanachama wa umoja huo, kuanza kuwaona kwa kuwanyima nafasi watazoomba kwani baadhi yao hivi sasa wameanza kutembeza fedha ili waweze kuchaguliwa kuingia katika uongozi.

Alisema ni lazima wachukue tahadhari hiyo kwa vile Uchaguzi Mkuu ujao bado ni Mgumu kwa Chama cha Mapinduzi, na ni lazima wanachama wa CCM kuona wanaowachagua ni viongozi wazuri ambao watakiwezesha kusonga mbele.

Alisema baadhi ya viongozi hao baada ya kuanza kujiona kuwa katika mazingira magumu kuweza kushinda katika chaguzi hizo wameamua kutumia nafasi walizonazo kuwapangia safu kwa kuweka wagombea wataoweza kutekeleza matakwa yao ya kuichafua serikali.

“CCM haitaki kupangiwa safu, CCM inahitaji wenye uchungu wa Chama na ni lazima muwaze namna ya kupata vingozi safi sio kukubali vipandikizi achaneni naoi wakija na pesa kuleni kisha wekeni viongozi safi” Alisema  Mama Asha.

Alisema hatari ya kuwaacha watu hao kufanya wapendavyo kinaweza kukisababishia chama hicho kuwa katika mazingira magumu kutekeleza majukumu yake hasa katika kuzilinda sera za Chama hicho na kuweza kupata nafasi ya kufanya mambo yao.

Alisema vipandikizi hivyo tayari Uongozi wa Chama cha CCM, imeanza kuwabaini kuwapo kwao katika Mkoa wa Kusini, Kaskazini, na Mjini Unguja, ikiwa ni hatua ikiwa ni maandalizi ya viongozi hao kutaka watu hao wapiti kwa njia yoyote ile ili waliowaweka kuweza kuwatumia kwa matakwa yao.

Alisema maamuzi ya serikali ya Zanzibar kuingia katika mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa dhamira yake ni kuona Wazanzibari wanapata maendeleo zaidi, na amani ya nchi inakuwa, na haitakuwa busara kuona wanawarejesha madarakani waaanaotaka kuichafua amani ya nchi.

Hata hivyo, Mama  Asha aliwataka wanachama hao kuona wanajitolea kuzifanya kazi za chama kwa kujitolea badala ya kuweka mbele maslahi ya kuhongwa.

Aidha, Mama Asha aliwataka vijana hao kuepuka vitendo vya vurugu juu ya hoja zinazojitokeza katika mambo ya Muungano, na badala yake waendelee na msimamo wa Chama cha Mapinduzi na kutekeleza Miongozo yake.

Hoja za baadhi ya viongozi kudai hawajazaliwa na nafasi za uongozi ndani ya Chama hicho zioneshe wazi kuwa watu hao wana lao na ni vyema wakaona umuhimu wa kuwaondoa kabla ya uchaguzi mkuu kufika.

“Mtu anasema hataki Muungano, hataki sensa hataki dawa ya mbu, hataki chanjo tuwaangalie hawa kwani ndo wale wale wasiopenda Wazanzibari waendelee Chagueni mtu mwenye sura moja hatutaki vichwa viwili kuleni pesa zeo kura kapigieni viongozi bora hakuna ataewajua” Alisema Mama Asha.

Akiendelea alisema ni vyema kwa wanachama hao kuona wanakaa mbali na viongozi anaoonyesha wako kwa ajili ya CCM na sio vigeu geu.

Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja Khamis Ali, akitoa maelezo yake aliwataka vijana kuona wanachagua viongozi ambao wataweza kukitetea Chama hicho katika uchaguzi Mkuu ujao.

“Sisitizo langu chagueni watu wazuri kufuata muendelezo wa kazi chama kusonga mbele tumeanza kuchagua ngazi ya chini tayari tumeshaapata viongozi wazuri sasa tunahitajiwazuri zaidi” Alisema Mwenyekiti huyo.

Alisema waanalazimika kufanya maandalizi hayo kwavile Chama cha Mapinduzi ndani ya mkoa huo kinajiandaa kuona Jimbo la Nungwi linarudi katika mikono ya CCM na nguvu ya vijana ni moja ya nguzo muhimu ya kuweza kufanikisha hilo.

 Nae Katibu wa Jumuiya hiyo Wilaya ya Kaskazini ‘B’, Salum  Suleiman Tate, amewataka wanachama hao kushirikiana na uongozi mpya utaokuja, kwa kutambua umoja huo ni tanuri kuu la kuweza kupatikana kwa viongozi bora.

Alisema jambo la msingi ambalo wanachama hao wanapaswa kulizingatia ni kuwa kitu kimoja na kuacha malalamiko yatayoweza kuwagawa kutokana na baadhi ya watu wameamua kutumia dini vibaya kwa kuingiza mambo ambayo yanaenda kinyume na matakwa ya dini.

Alisema ni lazima wanachama wa CCM kuanza kuyaona hayio hivi sasa kwani Tanzania imekuwa na taratibu mbali mbali za kushughulikia mambo ya dini kwa kuweka mabaraza maalum kufanya kazi hiyo kwa vile serikali tayari haina dini ila watu wake ndio wenyedini.

Aidha, Katibu huyo aliwataka wanachama hao kuona wanaendelea kushiriki katika sensa pamoja na mchakato wa kupatikana kwa Katiba mpya kwa vile bado Chama cha CCM kinahitaji kuendelea kuongoza serikali kikiwa na katiba bora itayowawezesha Waatanzania kuishi kwa amani na utulivu..

Nae Mjumbe wa  Kamanda wa Umoja huo Khamis Ali Salum, akitoa Shukrani zake, alisema vija wa CCM Mkoa huo watahakikish wanaisaidia Serikali kuona amanai ya Mkoa huo inaendelea kudumu kwa kuziya kutokea kwa vitendo vyenye kuashiria kuvurugika kwa amani.

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.