Salim Said Salim
SASA ni mwaka mmoja toka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilipoeleza kuwa ilikuwa katika hatua za mwisho za kutayarisha vitambulisho maalum kwa wazee, watu wenye ulemavu na wanafunzi.
Kwa mujibu wa hiyo taarifa ya serikali ilitolewa wakati ule lengo kuu la kuwepo kwa vitambulisho hivyo ni kuwawezesha watu waliomo katika makundi haya matatu ambayo yanakabiliwa na hali ngumu ya maisha, kuweza kupata usafiri kwa bei nafuu na kuwaondolea usumbufu.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa, kuanzia watu hawa watatumia vitambulisho hivi kupatiwa usafiri wa mabasi mijini na vijijini na ule wa baharini katika visiwa vya Unguja na Pemba kwa kulipa nusu ya nauli inayotumika wakati huo.
Hatua hii ilipokewa kwa furaha kubwa, hasa na watu waliomo katika makundi haya matatu. Wengi waliuona uamuzi huu wa serikali ulionesha namna ambavyo Serikali ya umoja wa kitaifa ya Zanzibar inavyowajali na kuwaonea imani wazee, wanafunzi na watu wenye ulemavu.
Uamuzi huu wa serikali ambao umekuwa ukitumika kwa muda mrefu katika nchi nyingi za nje ulitarajiwa kusaidia kupunguza matatizo ya usafiri yanayowakabili watu waliomo katika makundi haya matatu, hasa wale ambao ni maskini ambao hata chakula kinawapiga chenga.
Ukweli ni kwamba, hakuna mtu anayejali utu anayeweza kufanya ubishi kwamba watu waliomo katika makundi haya wanapata usumbufu mkubwa wa usafiri, mawasiliano na maeneo mengine mengi.
Badhi ya wakati watu hawa sio tu hawasaidiwi na madereva na makondakta, bali pia hudhalilishwa huku abiria wakiangalia kama vile kilichofanyika ni sahihi.
Sote tunashuhudia karibu kila siku namna wanafunzi, wengine wadogo sana ambao wanatokana na familia za kimasikini wanavyoteseka kupata usafiri.
Baya zaidi utaona wanasukumwa na makondakta wanapoingia kwenye magari wakati wa kwenda na kurudi shule.
Lakini kilichoonekana baada ya kutolewa kwa tamko la Serikali hakuna lililosikika kwa mwaka mzima sasa. Mwenendo huu wa kutoa ahadi na utekelezaji wake usionekane mekuwa kama ni utamaduni unaokubalka hivi sasa.
Watu wa Zanzibar katika miaka ya hivi karibuni wamekuwa wakipewa ahadi zinazowapa matumaini ya kuisha maisha bora siku za usoni ambazo hawazioni kutekelezwa.
Vile vile wananchi hutajiwa miradi mbali mbali kama ya ujenzi wa mji wa kibiashara wa Star City katika eneo la Fumba, nje ya mji wa Zanzibar wakati wa utawala wa Rais mstaafu, Komandoo Salmin Amour, ambayo hatimaye huwa ndoto ya mchana.
Hali kama sio nzuri hata kidogo na inawakatisha tanaa wananchi na hata kupoteza imani kwa serikali yao. Ni vizuri kwa serikali kuhakikisha inatekeleza ahadi zake na kama zinatokea sababu zinazosababisha kukwamisha utekelezaji wa hiyo mirada au ahadi zilizotolewa wananchi waambiwe, badala ya kukaa kimya.
Kwa hili suala la vitambulisho kwa wazee, watu wenye ulemavu na wanafunzi inafaa kwa serikali kwani kutayarisha sheria juu ya vitambulisho hivyo na kuweka kanuni juu ya matumizi ya vitambulisho hivyo.
Kwanza kabisa panatakiwa pawepo tafsiri isiyokuwa na utata inayoeleza sifa za mtu kuitwa mzee. Sheria pia ieleze wazi wazi nani ni mwanafunzi na pawepo maelezo yakinifu yanayofafanua nani anahesabika kuwa ni mtu mwenye ulemavu.
Baada ya hapo panahitajika sheria kuweka wazi kuwa kutotambua vitambulisho hivyo ni kosa la jinai na ielezwe adhabu anayestahili kupata anayeivunja sheria hii. Sio sahihi kutarajia maelekezo na maagizo ya serikali kwa kutoa tangazo kufuatwa na kuheshimiwa, hasa na wale waliozowea kuwadhalilisha wazee, watu wenye ulemavu na wanafunzi.
Tumesema tunajaribu kutandika utawala wa haki na sheria nchini na ili tuelekeee huko basi tutegemee sheria kufanya kazi na sio maombi, maelekezo au maagizo ya Rais, mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya auviongozi wa dini.
Huu wakati tulionao sio tena zama za utawala kutoa amri, miongozo, maagizo au maelekezo. Hizi ni zama za utawala wa haki na sheria na ni kwa kuwepo kwa sheria tu ndio kutaweza kuvifanya hivyo vitambulisho kuwa na maana na kufanya kazi iliokusudiwa bila ya matatizo au pingamizi yoyote ile.
Miongoni mwa mambo yanayofaa kuzingatiwa kwa haraka ni kwa sheria za utoaji leseni za usafiri wa dalala na boti kufanyiwa marekebisho kwa kuwekwa kipengele kinachoeleza wazi kuwa moja ya masharti ya kupatiwa hizo leseni za biashara ni kuvitambua na kuviheshimu hivi vitambulisho maalum kwa wazee, wanafunzi na watu wenye ulemavu.
Vile vile wale wote wataoonyesha dharau kwa vitambulisho hivi, pamoja na kuchukuliwa hatua za kisheria, wanyang’anywe leseni zao za biashara.
Serikali ya Zanzibar imeonyesha nia ya kuheshimu wazee na kuwaonea imani watu wenye ulemavu na wanafunzi, ijapokuwa kauli yake bado haijaonekana kutekelezwa.
Suala hili linapaswa kuungwa mono na wananchi na kila mtu kuelewa kuwa aliyekuwa kijana hii leo ipo siku atakuwa mzee na kuhitaji msaada kama wanaohitaji wazee wa hii leo.
Vile vile sote sisi tunapaswa kujuwa kwamba ni watu wenye ulemavu watarajiwa. Tunayajuwa ya jana na leo, lakini hatutambui kinachotungojea kesho au wiki ijayo.
Tushirikiane kuwasaidia wazee wetu, ndugu zetu wenye ulemavu na vijana wetu wanaohangaika usiku na mchana kujitafutia elimu ili wajikomboe kimaisha na hatimaye kusaidia kulijenga taifa hili.
Chanzo : Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment