Habari za Punde

Zanzibar itarajie kupata Watalii wengi kutoka China

Na Maelezo Zanzibar    07/09/2012
 
Naibu Waziri Mkuu wa China Hui Liangyu amesema kuwa Zanzibar itarajie kupata watalii wengi kutoka China kutokana na Visiwa vyake kuwa na Mandhari nzuri kwa Watalii.
 
Naibu Waziri Mkuu huyo ameyasema hayo leo kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume wakati alipokuwa akiagana na mwenyeji wake Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd.
 
Amesema kuwa Zanzibar ina rasilimali nyingi na zakuvutia hivyo yeye mwenyewe binafsi amefurahishwa nazo kwa hivyo atafanya kila linalowezekana kuona kuwa watalii zaidi kutoka China wanakuja kuitembelea Zanzibar.
 
Hui Liangyu amesifu Ukarimu alioupata wakati wote alipokuwepo Zanzibar na kuipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuimarisha ushirikiano kati ya China na Zanzibar
 
Naye Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd ameiomba Serikali ya China kuzidisha ushirikiano na kuzidi kuitangaza Zanzibar nchini China ili Watalii wengi wapate kuitembelea Zanzibar.
 
Amesema kuwa Ushirikiano uliopo hivi sasa kati ya nchi hizo mbili utazidi kuimarika na kuiomba China kutoisahau Zanzibar katika kutoa misaada yake mbalimbali ili Zanzibar iweze kuimarika katika masuala ya uchumi na maendeleo.
 
Mapema Naibu Waziri Mkuu huyo wa China Hui Liangyu alitembelea Kanisa la Angilicana lililopo Mkunazini ambapo aliangalia historia ya Kanisa hilo na baadaye kuelekea Beit el Ajaib na hatimaye Jumba la Wananchi Forodhani ambapo mote alielezewa historia ya mambo mbali mbali yaliyokuwemo katika majengo hayo pamoja na kupewa CD na Vitabu vinavyoonesha historia ya Majengo hayo.
 
Naibu Waziri Mkuu huyo ameondoka Zanzibar kuelekea Dar es Salaam asubuhi na kuagwa na Mwenyeji wake Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd,Mawaziri,Naibu Balozi wa China Zanzibar Mama Chen,Makatibu Wakuu na Manaibu wao, pamoja na Maofisa mbalimbali wa Ubalozi huo na Wataalamu mbalimbali wa China waliopo Zanzibar
 
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR
07/09/2012

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.