Na Husna Mohammed
WIZARA ya Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar, imekabidhi vifaa vya alama za mistari zenye kuitambulisha bidhaa zinazozalishwa Zanzibar kitaifa na kimataifa.
Hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo yalifanyika jana ofisi za Wizara ya Viwanda na Masoko, ziliopo Forodhani mjini hapa, ambapo kwa upande wa Serikali iliwakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Raphael Julian, na Sekta binafsi ambayo ni Jumuiya ya Wafanyabiashara, Wenyeviwanda na Wakulima (ZNCCIA) iliwakilishwa na Makamu wa Rais wa Jumuiya hiyo, Ali Talib Mzee.
Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na samani za ofisi, kompyuta mbili, mashine za kupriti, projekta, mashine na vifaa vyengine vya utambuzi wa alama hizo ambavyo vyote vinagharimu shilingi milioni 22.
Mara baada ya makabidhiano hayo, Katibu Mkuu Raphael, alisema alama hizo za utambulisho wa bidhaa zitawagusa wazalishaji wadogowadogo hadi wafanyabiashara wakubwa.
Alisema kwa muda mrefu sasa Zanzibar, imekosa alama ya utambulisho wa bidhaa jambo ambalo linawakosesha soko la uhakika la kimataifa.
Aliitaja nambari ya utambulisho wa bidhaa zinazozalishwa Zanzibar kuwa ni 620, hivyo aliwataka wazalishaji, wafanyabiashara na hata watumiaji kuangalia kwa makini utambulisho huo kwa bidhaa za ndani wanazonunua.
"Wafanyabiashara wote ambao wanatumia utambulisho wa nje ya Tanzania kama Kenya,Afrika Kusini, UAE, Ufaransa na nchi nyengine kuacha kutumia alama za nchi hizo na kuanza kutumia alama zitakazotolewa na taasisi ya kusimamia alama hizo Tanzania," alisema.
Aidha alisema kufanya kazi kwa vifaa hivyo kutaweza kuzitambua alama za bidhaa zinazozalishwa nchini kwa upeo mkubwa ikiwa ni pamoja na kuzikamata bidhaa zitakazotengenezwa kwa kughushi na kampuni nyengine.
Sambamba na hilo Katibu Mkuu huyo alisema Wizara itaandaa mafunzo kwa ajili ya kuhamasisha matumizi ya huduma hizo za alama za mistari.
Nae Makamu wa Rais wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, Wenyeviwanda na Wakulima, Ali Talib Mzee, alisema kuwepo kwa mpango huo ni suala la msingi na aliahidi kufanya uadilifu katika kufanikisha majukumu hayo.
"Sisi kama wasimamiaji wa suala hili nitahakikisha tunalifanya kwa uadilifu mkubwa kwa lengo la kuzifanya kazi zetu kutambulika kama tulivyotaka," alisema.
Kutokana na hilo alitaka kuwepo kwa mashirikiano makubwa kati ya wizara husika, wafanyabiashara na wadau wengine wa uzalishaji.
NBC Yakutana na Wateja Wake Wakubwa wa Jijini Arusha, Yajadili Fursa,
Ufanisi wa Huduma Zake Kwa wateja.
-
Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imekutana na wateja wake wakubwa kutoka
kampuni, wateja binafsi na taasisi mbali mbali (Corporates) wa jijini
Arusha ili k...
9 minutes ago
No comments:
Post a Comment