Habari za Punde

Bandari ya Mkoani yafanyiwa matengenezo

Na Nafisa Madai       WMM
Msaidizi Mkurugenzi mkuu wa shirika la bandari Pemba Hamad Salim Hamad amesema hivi sasa shirika la bandari Pemba limeweza kupiga hatua baada ya kufanyiwa matengenezo ya gati ya Mkoani ambapo awali ilikuwa ikituama maji.
Amesema hayo alipokua akimpa maelezo kuhusu bandari hiyo  Waziri wa Miundombinu na Mawasilano Mhe Rashid Seif Suleiman alipofanya ziara bandarini hapo na kufanya mazungumzo na wafanyakazi.
Mkurugenzi huyo amesema tatizo la kutuama maji bandarini limedumu kwa muda mrefu lakini kwa sasa tatizo hilo limepatiwa ufumbuzi yakini na limeweza kutoweka kabisa.

Akimuelezea matatizo yaliyopo kwa sasa mkurugenzi huyo amesema shirika lake kupitia bandari ya Mkoani imekabiliwa na tatizo kreni ambapo alisema iliyopo haiwezi kukidhi haja ya matumizi yalipo na mara nyengine hushindwa kufanya kazi kabisa.
Aidha alisema kreni hiyo imechakaa kutokana na kuwa na umri usiopungua miaka 28 ambapo alisema tokea kuletwa hapo mwaka 1984 inafanya kazi hadi leo.
Sambamba na hayo mkurugenzi huyo amesema shirika lake lina mpango wa kununua kreni mpya ambayo  itamudu shughuli za bandarini hapo na isiyopungua tani 25.
Kwa upande wake Waziri wa miundombinu na mawasiliano Rashid Seif Suleiman amesema imefika wakati kwa shirika hilo kubadilika kiutendaji ili waweze kwenda sambamba na ushindani kwa kibiashara.
Aidha alisema wizara ya miundombinu ni wizara ambayo inafanya kazi ya kuhudumia jamii moja kwa moja hivyo hakuna budi kuwajengea mazingira mazuri wateja wao
Hata hivyo alishauri shirika hilo kufanya mazungumzo na wafadhili ili waweze kuwajengea turubali katika njia inayopita abiria wakati wa kwenda kupanda meli kwani masafa ni marefu sana.
waziri huyo amesema kuanzia sasa shirika hilo kushirikiana na ZMA kuandaa utaratibu maalumu wa kupima uzito wa gari zinazoingia gatini ilikuepusha kuharibu miundombinu iliyopo.
Hata hivyo alisema gari ambayo itabaanika kuvunja miundombinu ya gati hiyo itachukuliwa hatua za kisheria kwa vile watakua wamekiuka utaratibu uliopo.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wa shirika hilo Salim Said  amesema ni vyema serikali ikishirikiana na wizara ya miundombinu kutafuta chombo cha uokozi kwani amesema bandari zote tatu hazina kifaa hicho
Aidha amesema watendaji wa shirika hilo kwa upande wa Pemba wanahitaji kuboreshwa kwa kupatiwa vitendea kazi pamoja na kuboreshwa kwa bandari yenyewe.
Kabla ya kufanya Ziara Bandarini hapo Mhe Rashid alitembelea maendeleo ya barabara ya kipitacho  yenye urefu  wa kilomita 1.6 bonde la mpunga wilaya ya Mkoani mkoa wa kusini Pemba.
Mhe Rashid alipatiwa maelezo kuhusu maendeleo ya barabara na mhandisi mkaazi Khamis Masoud ambapo alisema hatua ya ujenzi umefuatiwa agizo la mhe Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein na utekelezaji wake umefanikiwa asilimia mia moja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.