Habari za Punde

Masiku kumi bora yamewadia- tufaidike nayo


Leo Jumatano, kwa mujibu wa mwezi mwandamo ni tarehe 1 Dhulhajj (Mfunguo tatu) 1433 kwa mujibu wa sehemu alipoichagua Allaah Subhaanahu Wata’ala kuwa ndio Qiblah chetu (Saudia).

Hivyo tumeingia katika masiku kumi bora kabisa katika tarekhe ya kiislamu. Amesema Mtume Swalla Allaahu ‘Alayhi Wasallam katika Hadithi “Hakuna siku bora ambazo Allaah Subhaanahu Wata’ala huzikubali amali za waja kama siku kumi za mwanzo za Dhul Hajj” (Bukhaari)

Tukijaaliwa siku ya ‘Arafah itakuwa ni Alkhamis 9 Dhulhajj (mfunguo tatu) 1433 sawa na 25/10/2012

Sikukuu ya kuchinja (Iydul Adh –haa) tukijaaliwa itakuwa siku ya Ijumaa tarehe 10 Dhulhajj (mfunguo tatu) 1433 sawa na tarehe 26/10/2012.

Niwakumbushe Waislamu na waumini wenzangu pamoja na kuikumbusha nafsi kufanya ibada kwa wingi katika masiku haya, kuhakikisha tunafunga siku ya ‘Arafah (kwa wasiokuwa Mahujjaaj).


Ninakumbushia tu, tulioagizwa kufunga na Al Habib Mustafa Swalla Allaahu ‘Alayhi Wasallam katika Hadithi ni Siku ya ‘Arafah kwa hivyo tuhakikishe tunapofunga tunafunga siku ambayo Mahujjaaj waliopo Makkah husimama kwenye Mlima ‘Arafah  ili tuweze kupata fadhila za funga hii muhimu katika dini yetu.
Anasema Mtume Swalla Allaahu ‘Alayhi Wasallam “ Funga ya ‘Arafah hufuta madhambi ya mwaka uliopita na mwaka unaofuatia” Muslim.

Pia kuihuisha Sunna ya kuchinja siku Iydul Adh-haa kwani Sunna hii imekuwa mbali sana na Waislamu na wengi wetu tayari tuna uwezo wa kuitekeleza Sunna hii adhimu tokea enzi za kipenzi cha Allaah (Khaliilu Llaah) Ibraahim ‘Alayhis Salaam.

Ndugu yangu katika imani, hakikisha unazitumia vizuri siku hizi, badilisha mwenendo wa maisha yako, kithirisha kufanya ibada, rudi kwa Mola wako na wakumbushe Waislamu wengine ukumbusho huu baada ya kujikumbusha nafsi yako.

Tuwaombee dua Mahujjaaj wote ambao ni wageni wa Arrahmaan, Hija zao zitakabaliwe na kukubaliwa na Allaah Subhaanahu, madhambi yao wasamehewe na Sa’ay (mwendo wao kati ya Mlima Safa na Marwa)  yao iwe ni yenye kushukuriwa.

1 comment:

  1. Katika misha yangu naamini kwamba waandishi wa khabari wote ni waongo sawa na wana siasa, lakini kwa hapa Sheikh wangu MPARA umesema kweli na inshaAllah Allah atakulipa kwa hili ulilolifanya la kukumbusha.

    Lakini mbali na ushahidi huu ulioutoa wa kwamba waislamu tunatakiwa kuungana katika ibada hii ya hijja na asiyekua na uwezo anatakiwa afunge kwa kuwaunga mkono walioko huko kwenye nyumba tukufu, basi utakuja kuwaona wale wanaoitwa mshekhe tena wamekabidhiwa nyadhifa muhimu za kuwasimamia waislamu nchini wakisema kwamba hawataki kufuata saudia tena hii ni kwa kiburi chao tu walichonacho,lakini hapo hapo wanakubali kufuata kalenda waliopanga makafiri huko roma kwa kuizingatia siku ya x-mas kwa kufunga maofisi na shughuli zote za serikali ilhali wao haiwahusu......Al-junuunu funuunu.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.