Habari za Punde

Meli ya Azam Sea Link 1 yawasili. Kuanza safari karibuni, boti nyengine iko njiani 
MELI kubwa ya abiria kutoka kampuni ya Azam Marine imewasili visiwani Zanzibar  jana tayari kwa kuanza safari zake kati ya Unguja, Pemba na Dar es Salaam.

Meli hiyo iliyowasili bandari ya Malindi saa 8 mchana ikitokea nchini Ugiriki, ambapo ilitumia muda wa siku 14 hadi kuwasili kwake inatarajiwa kuanza kazi siku za hivi karibuni.

Akizungumza na waandishi wa habari bandarini hapo, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo, Hussein Mohammed Said alisema kuwasili salama kwa meli hiyo ni moja ya hatua muhimu ambayo kampuni yake ilikuwa ikitarajia katika azma yake ya  kuwaondolea adha ya usafiri wananchi wa Zanzibar.

Alisema meli hiyo inayojulikana kwa jina la Azam Sea Link 1 ni  meli kubwa ya kisasa katika ukanda wa Afirka Mashariki, ambayo itakuwa na uwezo wa kuchukua abiria 1500,mizigo, gari 240 yakiwemo malori 40 kwa wakati mmoja bila ya usumbufu wa aina yoyote.


Aliongeza kuwa kutokana na meli kuwa na viwango vinavyokidhi kimataifa ana imani kubwa kuwa hivi sasa wananchi wanaofanya safari kati ya visiwa hivyo, wataweza kuondokana na adha ya usafiri ambayo kwa muda mrefu umekuwa ukiwakabili.

“Lengo la kampuni ni kuhakikisha wananchi wa Zanzibar wanaondokana na adha ya usafiri, hivyo tumaini langu kubwa ni kuwa kilio cha wananchi kitaweza angalau kuondoka baada ya kuwasili kwa meli hii,” alisema.

Akizungumzia kuhusu nauli  kwa abiria watakaosafiri na meli hiyo, Hussein alisema kampuni hiyo mara nyingi imekuwa ikiangalia hali za wananchi wake hivyo, atahakikisha inaweka nauli ambayo kila mwananchi ataweza kumudu, kwa vile hali ya wananchi wengi ni maskini.

Hivyo amewataka wananchi kuwa tayari kwa ajili ya kuitumia meli hiyo mara tu itakapoanza kufanya kazi katika kipindi kifupi kijacho, kwa kutoa ushirikiano kwa kampuni yake ambayo imedhamiria kuwekeza zaidi katika usafiri wa bahari.

Aidha aligusia ujio wa boti mpya ya Kilimanjaro 4 ambayo alisema tayari mipango imefanyika ya kuhakikisha kuwa boti hiyo inafika Zanzibar nchini si muda mrefu ujao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.