Habari za Punde

Uhusiano wa Cuba, Zanzibar kuimarishwa



 Na Othman Khamis, OMPR
ZANZIBAR itaendelea kuwa mshirika mkubwa wa Jamuhuri ya Watu wa Cuba kutokana na historia ya muda mrefu kati ya mataifa hayo mawili rafiki tokea Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi  alitoa kauli hiyo wakati alipokuwa akizungumza na Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa Cuba nchini Tanzania, Ernesto Gomez Diaz aliyefika nyumbani kwake Mazizini nje kidogo ya mji wa Zanzibar kumuaga  baada ya kumalizika muda wake wa utumishi Tanzania.
Balozi Seif alisema wananchi wa Zanzibar kwa muda mrefu wameshuhudia juhudi kubwa za Cuba katika kuunga mkono maendeleo na ustawi wa jamii wa wananchi wa Zanzibar .
Aliitaja sekta ya afya kuwa ni miongoni mwa maeneo yaliyopata fursa ya kuimarika kitaalamu na utendaji kufuatia mpango wa wataalamu wa mabingwa wa afya wa Cuba kuwafundisha madaktari wazalendo  nchini.

Balozi Seif alimueleza Balozi wa Cuba kwamba  mpango huo unaonyesha  ishara njema ya kupata wataalamu wazalendo wanaotarajiwa kutoa huduma za afya mara wamalizapo mafunzo yao.
“Kwa muda mrefu tulikuwa tukishuhudia vijana wetu wengi wanaopata fursa za masomo ya juu nje ya nchi hutoweka mara wamalizapo masomo yao bila ya kujali kuwa wanaitia hasara nchi yao  kwa tamaa ya maisha mazuri zaidi,”alisema.
Alimpongeza Balozi Diaz kwa juhudi zake za kuendelea kuunganisha nguvu ya uhusiano uliopo kati ya Zanzibar na Cuba.
Mapema Balozi huyo Cuba alielezea matumaini yake kwamba mpango wa kufundisha madaktari wazalendo chini ya usimamizi wa madaktari mabingwa wa Cuba utasaidia kupunguza uhaba wa madaktari Zanzibar.
BaloziErnesto alisema katika kuimarisha uhusiano wa pande hizo mbili Cuba inakusudia kuongeza fursa za masomo kwa vijana wa Kitanzania hatua ambayo hata Zanzibar itafaidika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.