Habari za Punde

Watanzania 2,700 kuhiji mwaka huu

Na Othman Khamis, OMPR
 
VIONGOZI wa Taasisi zinazoandaa safari za hijja hapa Nchini wamenasihiwa kuunganisha baadhi ya Jumuia zao zinazofanana ili kuwa na Taasisi chache zenye nguvu na uwezo mkubwa wa kutekeleza kazi hiyo kwa umakini na ufanisi zaidi.
 
Nasaha hizo zimetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi wakati akiwaaga Mahujaji watarajiwa wa Zanzibar wanaojiandaa kuelekea Maka Nchini Saudi Arabia kwenda kutekeleza ibada ya Hijja Mwaka huu, hafla iliyofanyika katika Msikiti Mkuu wa Ijumaa wa Muembe Shauri Mjini Zanzibar.
 
Balozi Seif alisema hatua hii itasaidia kuwapunguzia gharama nyingi na kupelekea kupatikana kwa lengo kuu la Hijja ambalo ni kujenga Umoja na Mshikamano miongoni mwa Waumini wa Dini ya Kiislamu.

  Alieleza kuwa Jamii inaendelea kushuhudia idadi kubwa ya Mahujaji kutoka Mataifa ya Bara la Asia na nyengine za Kiafrika wanavyojipanga mapema kupitia jumuia zao chache lakini madhubuti na kuwezeshana kutimiza Ibada hiyo.
 
“ Kwa wenzetu hili halikuja kwa sadfa, bahati au kujitokezea tu. Juhudi kubwa ilipita ya uelimishaji na uhamasishaji hadi watu wakafahamu, wakahamasika na kuanza kujipanga mapema na kuwawezesha kutimiza ibada hii”. Alifafanua Balozi Seif.
 
Aliuomba Umoja wa Taasisi za Hijja Zanzibar { UTAHIZA } ni vyema ukaangalia uwezekano wa kuziunganisha baadhi ya Jumuiya zilizodhaifu kiutendaji na hatimaye kupata nguvu za pamoja na kuimarisha Jumuiya hizo kwa pamoja.
 
Balozi Seif aliwaeleza Mahujaji watarajiwa kwamba fursa hiyo waliyoipata ni neema kuwa ambayo inahitaji shukrani na wanapaswa kumshukuru Mwenyezi Muungu kwa kuwawezesha kuwemo katika Mahujaji wa mwaka huu.
 
  Aliwataka Mahujaji hao watarajiwa watakapojaaliwa kurudi salama wazingatie kuzilinda Hijja zao kwa kumudu katika twaa ya Allah. “Allah {SW} awajaalie muende salama na mrudi salama na mrudi na hidaya ya uongofu pamoja na hidaya { zawadi }, kwani wengi huenda wakarudi na hidaya {zawadi} bila ya hidaya ya uongufu”.
 
Alisisitiza Balozi Seif. Mapema Mwenyekiti waTaifa wa Umoja wa Taasisi za Hijja Zanzibar {UTAHIZA } Sheikh Sultan Khamis Mbarouk ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa uamuzi wake wa kutaka kununua Meli kubwa kwa ajili ya usafirishaji wa Wananchi kati ya Visiwa vya Unguja na Pemba.
 
Sheikh Sultan alisema ni vyema Meli itakayonunuliwa iwe na uwezo pia wa kuandaliwa mazingira ya kuwasafirisha Mahujaji wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla kwa gaharama nafuu utaratibu ambao hufanywa na baadhi ya Mataifa Duniani kusafirisha Mahujaji wao.
 
“ Kuna malalamiko kutoka kwa Waislamu kuhusu kupanda kwa gharama za nauli ya Hijja kila mwaka na kutupiwa lawama Taasisi za Hijja”. Alisema Sheikh Sultan na kufafanua kwamba hilo si sahihi kwa ongezeko hilo husababishwa na kupanda kwa bei ya gharama za usafiri wa ndege, Nyumba pamoja na Mahema huko Saudi Arabia.
 
  Mwenyekiti huyo wa Umoja wa Taasisi za Hijja Zanzibar ameishauri Serikali kuimarisha na kuipa uwezo zaidi Taasisi inayounganisha shughuli za Hijja kati ya Wizara ya Hijja ya Saudia na Tanzania {BIITHA} ili itekeleze kwa upeo zaidi kazi zake.
 
Alisema Zanzibar hivi sasa ndio yenye mamlaka ya kuiongoza Taasisi hiyo ya Biitha kwa mujibu wa Sheria na taratibu za Saudia Arabia za kutaka Chombo kinachosimamia masuala ya Hijja kiongozwe na Mtu asiyepunguwa wadhifa bwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Serikali.
 
Vile vile Sheikh Sultan aliishauri Serikali kwa vile bado waumini wengi hasa vijana hawajatekeleza Ibada ya Hijani vyema ikafikiria kuanzisha mfuko wa hiari wa Hijja kwa wafanyakazi wake mara tuu baada ya kuwaajiri ili kuwajengea uwezo mapema wa kujiandaa na ibada hiyo hapo baadaye.
 
Kwa upande wake Kiongozi wa Taasisi inayounganisha shughuli za Hijja Kati ya Tanzania na Wizara ya Hijja ya Saudi Arabia { BIITHA } Sheikh Khalid Mohd Mrisho alisema kwamba Tanzania hivi sasa ina Taasisi karibu 25 ambapo Zanzibar pekee ina Taasisi 7 zinazoshughulikia safari za Hijja.
 
Sheikh Khalid alifahamisha kwamba Timu ya Uongozi wa Taasisi hiyo inatarajiwa kuondoka Nchini Wiki ijayo kwa ajili ya kujiandaa kuwapokea Mahujaji watarajiwa wa Tanzania watakaowasili Saudia kwa ajili ya Ibada hiyo. Jumla ya Mahujjaji wa Tanzania wapatao 2,700 kati ya hao 1000 kutoka Zanzibar wanatarajiwa kuondoka Nchini katika makundi tofauti yatakayoanzia Tarehe 8 na 16 Oktoba mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.