Habari za Punde

Dk.Shein: Viongozi wajibikeni mkuze uchumi

Na Hafsa Golo
 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk. Ali Mohamed Shein amewataka viongozi na watendaji wakuu wa serikali kutekeleza majukumu yao ipasavyo ili nchi iweze kukua kiuchumi.
 
Dk.Shein alitoa kauli hiyo alipokua akifungua semina ya viongozi na watendaji wakuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika hoteli ya Zanzibar Beach Resorti bweni jana.
 
Alisema viongozi watakapofanya kazi kwa bidii na kufuata taratibu ipasavyo wataweza kuifanya nchi kuwa katika hali nzuri ya maendeleo.

Dk.Shein aliwataka viongozi hao kufanya tathmini ya utendaji wao wa kazi na kubainisha matatizo yanayozikabili taasisi zao ili waweze kuelewa hatua mbali mbali za kiutendaji walizofikia.
 
Aidha alisema viongozi na watendaji wote waliokwenda kujifunza na kupata uzoefu katika nchi mbali mbali ikiwemo China ni vyema wakawajibika ipasavyo kwa kutumia mafunzo hayo kwa vitendo ili taifa liweze kukua kimaendeleo.
 
Alisema iwapo watendaji hao wataiga mbinu za ukuaji wa uchumi wa nchi walizozitembelea maendeleo ya haraka yataweza kupatikana katika mpango wa miaka mitano ijayo.
 
Aidha aliwahimiza watendaji hao kufanya kazi kwa ushirikiano na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali ili (CAG) kuhakikisha fedha wanazotumia zinafuata sheria za matumizi.
 
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee alisema sababu kubwa zilizoifanya serikali kuichagua China kupewa mafunzo ni kwa sababu nchi hiyo imepiga hatua katika maendeleo.
 
Alisema pamoja na maendeleo makubwa ambayo China imeyapata ikiwe ukuaji wa uchumi, afya na elimu , vifo vya mama na wajawazito vimepunguwa kutoka 1500 kwa kila watu 100,000 hadi kufikia 30 kwa kila watu 100,000.
 
Semina hiyo ya siku tatu yenye kauli mbiu ‘Viongozi lazima tubadilike’ inakusudia kutafuta njia ya kuiwezesha Zanzibar kupata mafanikio katika mipango yake ya maendeleo.
 
Mada mbali mbali za kuhamasisha maendeleo zitawasilishwa katika semina hiyo, ikiwa ni pamoja na mapitio ya Vision 2020, MKUZA II na athari za ongezeko la watu nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.