Na Mwandishi wetu Dodoma.
WAJUMBE wa Mkutano Mkuu wa nane Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamemchangua Dk.Jakaya Mrisho Kikwete kuwa Mwenyekiti wa Chama hicho na Dk. Ali Mohamed Shein kuwa Makamu Mwenyekiti Zanzibar na Phillip Mangula kuwa Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara.
Uchaguzi huo uliongozwa na Mwenyekiti Mstaafu wa CCM na Rais Mstafu wa Awamu ya tatu, Benjamin William Mkapa, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano Kizota, nje kidogo ya Mji wa Dodoma.
Akitangaza matokeo hayo msimamizi wa uchaguzi huo, Spika Anna Makinda alisema Dk. Kikwete amepata kura 2395 kati ya kura 2397 zilizopigwa na wajumbe wa mkutano huo ambapo ushindi huo ni sawa na asilimia 99.92 huku kura zilizokataa zikiwa ni mbili.
Nafasi ya Makamu Mwenyekiti Tanzania Zanzibar, Mwenykiti huyo alisema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amefanikiwa kushinda uchaguzi huo kwa kupata kura 2397 kati ya kura 2397, ambapo hakuna kura iliyoharibika wala iliyomkataa ushindi huo ni sawa na asilimia 100.
Mwenyekiti huyo pia alimtangaza Phillip Mangula, kuwa mshindi wa nafasi Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara baada ya kupata kura 2397, ambapo hakuna iliyoharibika, ikiwa ni ushindi wa asilimia 100 huku kura zilizopigwa zikiwa ni 2397 na zilizosema hapana ni sufuri.
Matokeo hayo yalisababisha ukumbi wa mkutano huo kuripuka kwa furaha kwa kuwafanya wajumbe wa mkutano huo kushangiria kwa nguvu.
Baada ya uchaguzi huo Wajumbe hao kwa mara ya kwanza leo wanatarajiwa kukaa katika kikao cha kwanza kuweza kuchagua viongozi wapya kwa kujaza nafasi ya Katibu Mkuu mpya na watendaji wengine wa ngazi mbali mbali wa Chama hicho.
No comments:
Post a Comment