Ni mapendekezo kamati kuzama Skagit
Na Mwantanga Ame
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), inajiandaa kuweka sheria itayoyalazimisha makampuni ya usafiri wa baharini, kuwa na mtaji wa shilingi bilioni 3,000,000,000, ili yaweze kufanya kazi hapa Zanzibar, baada ya serikali kukubaliana na maoni ya Tume iliyoteuliwa na Rais kuchunguza ajali ya kuzama kwa meli ya Mv.Skagit.
Pendekezo jengine ambalo serikali inajiandaa nalo ni kuweka sheria itayoweza kuyabana makampuni yanayokiuka utaratibu wa kuuza tiketi kwa kutumia vitambulisho badala yake kuruhusu uuzaji tiketi kiholela jambo ambalo linasababisha abiria kutosajiliwa katika orodha ya wasafiri.
Hatua hiyo ya serikali inakusudia kuichukua baada ya kubaini baadhi ya makampuni ya usafiri baharini yanaendela kukaidi amri ya serikali kuuza tiketi kwa njia zisizo salama baada kukiuka utaratibu wa kuuza tiketi kwa vitambulisho vya mhusika halisi.
Hali hiyo imebainika baada ya serikali kufanya uchunguzi wake na kubaini baadhi ya makampuni hayo yanashindwa kutekeleza amri hiyo na yanaendeleza uuzaji wa tiketi kiholela kwa mtu mmoja kuwa na tiketi zaidi sita zikiwa na majina tofauti jambo ambalo linaweza kusababisha kutojulikana idadi ya abiria na majina yao halisi.
Hapo awali baada ya kutokea kwa ajili ya meli ya Mv. Spice Islender na Mv.Skagit, serikali ilipiga marufuku ya uuzaji wa tiketi bila ya kutumia vitambulisho kwa kila msafiri.
Kutokana na amri hiyo ya serikali imesema mtu yoyote ataefanya vitendo hivyo atakuwa anakwenda kinyume na sheria atafikishwa katika vyombo vya sheria.
Akizunumza na Zanzibar Leo Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, alisema ni kweli kumekuwa na hali ya kujirejea ya tabia ya baadhi ya makampuni kuuza tiketi bila kuzingatia marufuku hiyo.
Alisema hivi sasa serikali inajiandaa kufanya mabadiliko ya sheria na 5 /206 inayosimamia usafiri wa baharini ambayo itabadilishwa pamoja na kanuni zake.
Alisema sheria hiyo itapokuwapo itaweza kuleta mabadiliko ya mfumo wa uuzaji wa tiketi kwani utamlazimisha mwenye kampuni kuifanya kazi hiyo kwa matakwa ya sheria.
Alisema hivi sasa inawezekana matatizo yanayojitokeza ya baadhi ya wauzaji wa tiketi kutofuata amri hiyo kutokana na kutomfunga kisheria jambo ambalo limekuwa likiwafanya kufanya wapendavyo.
Eneo jengine ambalo Katibu huyo alisema limo katika mapendekezo ya Tume iliyochunguza ajali ya kuzama meli ya Mv Skagit, ni kuweka sheria itayomlazimisha mmiliki wa kampuni inayoendesha biashara ya kusafirisha abiria baharini kuwa na mtaji wa shilingi bilioni tatu.
Katibu huyo alisema mapendekezo hayo yanadhamiria kuiwezesha kampuni ya usafirishaji wa abiria kumudu majukumu ya kifedha pale inapotokezea maafa.
Pendekezo hilo Katibu huyo alisema linakuja kutokana na biashara ya meli kukabiliwa na hatari kubwa na ni lazima kuwe na mtaji wa kampuni kwa kiwango cha chini utaoweza kuoanisha kisheria.
Mapendekezo mengine yaliyopendekezwa na Tume kufanywa katika sheria hiyo Katibu huyo alisema ni pamoja na kipengele kitachokuwa kinazilazimisha uongozi wa kampuni za usafiri baharini kuwa na wataalamu wa masuala ya usafiri wa baharini.
Katibu Mkuu huyo alisema Tume hiyo pia imetoa mapendekezo mbali mbali yanayohusu ulazima wa mabadiliko ya sheria 5/2006, kikiwemo kifungu cha 7 (8), kinachotowa mbadala kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri Baharini, kuteuwa Mrajis wa meli na Mrajis wa Mabaharia kifutwe na badala yake vibakie bila ya kuwa na mbadala kwenye kifungu cha 7 (2) na (3) ili nafasi hizo ishikwe na mtu mmoja.
Sehemu nyengine ambayo Katibu huyo alisema inakusudiwa kuwekwa katika sheria hiyo ni kuwepo kwa utaratibu maalum wa kisheria utaoongoza suala zima la uuzaji wa meli na ulipaji wa fidia utawekewa utaratibu utaoiwezesha serikali kusimamia madai ya fidia kwa niaba ya watu walioathirika na maafa.
Pia Tume hiyo Katibu huyo alisema imependekeza kuwekwa kwa utaratibu wa sheria utaoweka kiwango cha chini cha bima kwa ajili ya abiria kutokana na hivi sasa umekuwa ukitoa mwanya kwa wamiliki wa vyombo vya baharini kuweka viwango kidogo vya bima.
Akizungumzia namna ya kuimarisha usafiri baharini Katibu huyo alisema ipo haja ya kuona kunakuwa na wataalamu wa kutosha wenye ujuzi, uzoefu na sifa stahili katika fani mbali mbali ikiwemo ya ukaguzi wa meli, ubaharia, usimamizi na udhibiti wa usalama wa abiria wanaopanda vyombo vya usafiri wa baharini na kusomesha waliopo kazini ili waweze kwenda na mfumo wa teknolojia ya kisasa.
Aidha, mapendekezo mengine ambayo aliyataja ni pamoja na kuviimarisha vyombo vya uokozi vikiwemo vikosi Maalum ili waweze kuifanya kazi hiyo kitaalamu kwa kuwa na mazoezi ya pamoja kila baada ya muda.
No comments:
Post a Comment