Na Masanja Mabula, Pemba
WIZARA ya Biashara, Viwanda na
Masoko Pemba, imekusudia kutoa elimu ya biashara kwa wafanyabiashara wa Pemba
ili waweze kuimarisha biashara zao kwa mfumo wa kutumia mtandao.
Akizungumza na mwandishi wa
habari hizi huko ofisini kwake Wete, Ofisa Mdhamini Wizara hiyo Pemba, Hemed
Suleiman Abdalla, amesema kuwa mfumo huo utawarahisishia utendaji wa kazi kwa
wafanyabiashara kwani watakuwa na uwezo wa kuagizia bidhaa kutoka nje ya nchi
wakiwa kisiwani Pemba.
Alisema utaoji wa elimu hiyo
utafanywa na watendaji wa Wizara hiyo kwa kushirikiana na taasisi nyingine
ambazo zinahusiana na masuala ya fedha ikiwemo Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB),
Halmashauri, Mabaraza ya miji pamoja na jumuiya ya wafanyabiashara na wakulima
Zanzibar (ZNCIA).
Alifahamisha kuwa uamuzi wa
kuwapa elimu ya biashara wafanyabiashara wa Pemba ni kutaka kuimarisha hali zao
za biashara sambamba na kuwafanya waingie katika biashara ya kisasa jambo
ambalo linawafanya waweze kuongeza kipato na kuimarika kwa mitaji yao.
“Ni utaratibu mzuri, kwani
wafanyabiashara watakuwa na uwezo wa kuagizia bidhaa wakiwa kisiwani hapa na
hivyo kupunguza gharama za kufuatilia bidhaa ambapo hutumia fedha nyingi
kusafiri na kusafirisha mizigo yao," alifahamisha.
Katika hatua nyingine, Hemed
aliwataka wafanyabiashara kisiwani Pemba kutumia fursa hiyo kuagizishia bidhaa
kutoka nje ya nchi na kusisitiza kuwa
uingizaji wa vyakula hauna kizuwizi isipokuwa kila mmoja ana uhuru kuingiza
alimradi afuate sheria na taratibu.
Akizungumzia suala la
kuimarisha kilimo cha mikarafuu, ofisa huyo, alisema kwa sasa wana mpango wa
kupita kila wilaya na kuzungumza na wakulima ili kuwaelimisha juu ya mkataba
ulioingiwa na serikali wa kuitangaza karafauu kwenye soko la dunia.
Alisema mkataba huo
utawanufaisha wakulima na serikali kwani karafuu wa Zanzibar itakuwa na
inajulikana katika soko la dunia na hatatokea mtu kuisafirisha kwa njia ya
magendo.
Hivyo aliwaomba wakulima kuunga
mkono juhudi za serikali za kuitangaza karafuu kwenye soko la dunia ili lengo
lililokusudiwa liweze kufikiwa.
No comments:
Post a Comment