kusalimiana na Rais
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akizungumza na Balozi wa Ubelgiji Nchini Tanzania Koen Adam, alipofika Ikulu Mjini Zanzibar,kwa ajili ya
kusalimiana na Rais.[Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]
Rajab Mkasaba, Ikulu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amefanya mazungumzo na Balozi wa Belgium nchini Tanzania Mhe. Adam Koenraad na kumueleza jinsi Serikali inavyoimarisha sekta za maendeleo huku akiwataka waekezaji wa nchi hiyo kuja kuekeza Zanzibar hasa katika sekta ya utalii.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu mjini Zanzibar, Dk. Shein alimueleza Balozi Koenraad kuwa Zanzibar inawakaribisha waekezaji kutoka Belgium kuja kuekeza katika sekta mbali mbali ikiwemo sekta utalii ambayo tayari imeanza kupata mafanikio makubwa hapa nchini.
Alimueleza balozi huyo kuwa Zanzibar imepata mafanikio makubwa katika sekta ya utalii na ndio maana juhudi za makusudi zimekuwa zikichukuliwa na serikali anayoiongoza katika kuiimarisha sekta hiyo muhimu ambayo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa.
Kutokana na mafanikio hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa itakuwa ni jambo la busara na faraja kwa wawekezaji wa nchi hiyo kuja kuekeza Zanzibar hatua ambayo itazidi kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya pande mbili hizo.
Aidha, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo ambyae alikuja kujitambulisha kwa Rais kuwa mikakati maalum imewekwa katika kuhakikisha haiba ya Mji Mkongwe wa Zanzibar inadumishwa ili iendelee kuwa kivutio kikubwa cha watalii pamoja na kudhihirisha kuwa ni urithi wa kimataifa.
Pamoja na hayo, Dk. Shein aliipongeza Belgium kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza sekta zake za maendeleo.
Nae, Balozi Koenraad alimueleza Dk. Shein kuwa Belgium inathamini uhusiano na ushirikiano uliopo kati yake na Zanzibar na kusisitiza kuwa nchi yake itaendelea kuiunga mkono Zanzibar kwa kutambua juhudi inazozichukua katika kujiletea maendeleo endelevu.
Katika maelezo yake balozi huyo, alimueleza Dk. Shein kuwa atatumia nafasi yake vizuri ya ubalozi kwa kuitangaza Zanzibar nchini kwake kwa lengo la kuwavutia wafanyabiashara na waekezaji kuja kuekeza Zanzibar.
Mbali na hayo, Balozi huyo pia, aliahidi kuwa ataitangaza Zanzibar kiutalii nchini mwake.
Akieleza kuhusu yeye mwenye binafsi amevutiwa na Zanzibar kutokana na mazingira yake sanjari na vivutio kadhaa ilivyonavyo ambacho kimoja wapo katika hivyo ni utulivu mkubwa uliopo hapa nchini.
Pamoja na hayo, Balozi Koenraad alimueleza Dk. Shein kuwa sifa kubwa imekuwa ikipata Zanzibar ulimwenguni kutokana na Mji Mkokwe wake ambao ni urithi wa kimataifa wa kitaifa hivyo alisisitiza haja ya kuuendeleza na kuendelea kuutunza kwani ni rasilimali kubwa ya taifa.
Alisema kuwa Belgium itaendelea kuiunga mkono na kuisaidia Zanzibar katika kuendeleza na kuimarisha sekta za maendeleo ili iendelee kupiga hatua katika kujiteletea maendeleo endelevu.
No comments:
Post a Comment