Habari za Punde

Dk Shein akutana na uongozi wa Wizara ya Ardhi

 Watendaji wa Wizara ya Ardhi,Makaazi,Maji na Nishati katika Idara mbali mbali wakiwa katika Mkutano na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, katika utekelezaji wa Mpango wa kazi za Wizara hiyo,leo katika Ukumbi wa Mikutano Ikulu Mjini Zanzibar,(kulia) Waziri wa Wizara hiyo Ramadhan Abdalla Shaaban.
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Ardhi,Makaazi,Maji na Nishati,leo katika utekelezaji wa Mpango wa kazi za Wizara hiyo katika Ukumbi wa Mikutano Ikulu Mjini Zanzibar leo,(kushoto) Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif


Na Rajab Mkasaba, Ikulu
 
WIZARA ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati imeeleza mikakati yake katika kuhakikisha malengo iliyojiwekea yanafikiwa kikamilifu kwa mashirikiano ya pamoja ili kutoa huduma zilizo bora kwa wananchi.
Maelezo hayo yametolewa leo na uongozi wa Wizara hiyo, wakati wa mkutano kati ya uongozi huo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, katika kuangalia utekelezaji wa kazi za Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2011-2012 na 2012-2013.
Katika mkutano huo uliofanyika Ikulu mjini Zanzibar ambapo pia, Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd walihudhuria, pamoja na Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahaya Mzee, ambapo Wizara hiyo ilieleza azma iliyoweka katika kuhakikisha inafikia malengo hayo.
Uongozi huo chini ya Waziri wake Mhe. Ramadhan Abdalla Shaaban, ulieleza kuwa utahakikisha upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na kutilia mkazo suala zima la uhifadhi wa vyanzo vya maji ili kukuza maendeleo ya wananchi kiuchumi na kijamii.
Uongozi huo ulieleza kuwa juhudi za makusudi zitachukuliwa katika kuhakikisha ongezeko la usambazaji wa maji safi na salama vijijini kutoka asilimia 60 ya mwaka 2010 hadi asilimia 75 ifikapo mwaka 2015.
Pia, kuongezeka kwa usambazaji wa maji safi na salama Mjini kutoka asilimia 80 kutoka mwaka 2010 hadi 95 ifikapo mwaka 2015, hatua ambayo itasaidia kupunguza tatizo la maji nchini.
Aidha,Wizara hiyo ilieleza kuwa Mpango Mkuu wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUZA II) unakusudia kuongeza na kuhakikisha kwamba kunakuwepo makaazi bora huku ukieleza makusudio yake katika kuuhifadhi Mji Mkongwe wa Zanzibar kiutamaduni na historia kama mji wa urithi wa kitaifa.
Kwa upande wa sekta ya ardhi, kama inavyofahamika kuwa sekta hiyo ina jukumu la kuimarisha mipango bora ya matumizi bora ya ardhi katika ngazi tofauti, kufanya usajili wa ardhi pamoja na kutatua migogoro ya ardhi inayojitokeza siku hadi siku.
Katika kuhakikisha makaazi endelevu, Wizara hiyo ilieleza kuwa Dira 2020 inaeleza kwamza taasisi husika zihakikishe zinaweka utaratibu ulio wazi na imara kwenye masuala ya uhaulishaji ulindaji wa ardhi.
Wizara hiyo ilieleza kuwa lengo hili litafikiwa kwa kuanzisha mfumo mpya wa uhakiki wa matumizi ya ardhi pamoja na kuwaelemisha wananchi kupitia vyombo vya habari.
Katika maelezo yao pia, uongozi huo ulieleza hatua unazozichukua katika kuhakikisha tatizo la maji katika kijiji cha Chwaka linapatiwa ufumbuzi na kumalizika kabisa mwishoni mwa mwezi huu.
Aidha ulieleza sababu zilizopelekea kuanguka kwa jumba la Ajabu, Forodhani na kueleza hatua zinazochukuliwa hivi sasa katika kuhakikisha ujenzi wa sehemu iliyoanguka unafanyika haraka.
Nae Dk. Shein alieleza umuhimu wa mashirikiano ya pamoja katika utendaji wa kazi huku akisisitiza hatua madhubuti katika kuwapelekea wananchi huduma bora za kimaendeleo na kijamii zinazotokana na Wizara hiyo..
Dk. Shein alitoa pongezi kwa Wizara hiyo kutokana na juhudi inazozichukua katika kuimarisha sekta zake.


2 comments:

  1. Mambo ya chai hayo!
    Wakati Mh. Rais anaendelea kuwaalika watendaji mbali mbali wa SMZ ikulu kwa ajili ya 'chai' huko mawizarani mambo hayaendi kabisa!

    Ukienda leo hii Wizara ya ardhi utaskitika..utakuta majalada mamia kwa mamia yanayosubiri 'uhaulishaji' huku yakiwa yamekamilisha taratibu zote lkn. hakuna kinachofanyika.

    Ni kweli Z'bar kuna matataizo mengi ya ardhi lkn. ni kwenye mashamba na sio viwanja sasa kuendelea kushikilia mafaili ya watu mpaka watoe rushwa huo kweli ndio utawala bora?

    ReplyDelete
  2. Nadhani Dk Shein angekuwa na utaratibu mwengine pia wa kusikiliza upande wa pili yaani wananchi Je haya wanayoyasema watendaji yanatekelezwa? Hapo atapata sura na picha kamili lakini hili la kuwasikiliza viongozi tu? kila siku utapewa faili lenye kuvutia kwa kila vinjonjo

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.