Habari za Punde

Jaji Samatta awalipua Polisi

Aeleza wanavunja haki za binadamu .
Asema wana mtazamo wa chama kimoja
 
Na Mwinyi Sadallah
 
Jaji Mkuu mstaafu, Barnabas Samatta, amelishukia jeshi la Polisi na kusema linachangia kuchochea uvunjaji wa haki za binadamu nchini.
 
Amesema miongoni mwa haki zinazovunjwa na jeshi hilo ambalo kimsingi, linapaswa kuwalinda raia na mali zao, ni kuzuia uhuru wa kutoa maoni na kuandamana.
 
Jaji Samatta alisema hayo jana wakati akifungua kongamano la wasaidizi wa sheria, lililoandaliwa na Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC), ikilenga kujadili mambo mbalimbali kisiwani Pemba.

 
Kauli ya Samatta imekuja siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete, kulihusisha jeshi hilo na harakati za kisiasa za Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho yeye (Kikwete) ni Mwenyekiti wake.
 
Akifungua Mkutano Mkuu wa CCM mjini Dodoma hivi karibuni, Rais Kikwete, pamoja na mambo mengine, alikaririwa akitoa rai kwa chama hicho kujibu hoja za upinzani badala ya kuwategemea polisi.
 
Kauli ya Rais Kikwete ilitafsiriwa kwa namna tofauti, huku ikihusishwa na malalamiko ya siku nyingi ya upinzani na asasi za kiraia, kwamba CCM inasaidiwa zaidi na vyombo vya dola kubaki madarakani.
 
Ingawa Jaji Samatta hakugusia ama kulihusisha jeshi hilo dhidi ya chama cha siasa, alisema polisi ni moja ya vyombo vinavyotumika kunyima uhuru wa kutoa maoni na kuandamana kwa raia. “Polisi bado wana mitazamo ya mfumo wa chama kimoja, wanakataza maandamano hata pale ambapo ni wazi kabisa kuwa hakuna hatari, usumbufu au amani kuvurugwa,”alisema Jaji Samatta.
 
  Alisema mtazamo huo ni potofu kwa sababu unasababisha wananchi kubakia (moyoni) na mambo yanayowasumbua.
 
Kwa mujibu wa Jaji Samatta, uhuru wa mawazo ni haki ya msingi isiyotokana na fadhila ya watawala kwa raia. Alisema haki hiyo na ile ya kuandamana ni za msingi na kwamba kuwazuia kufanya hivyo ni mtazamo potofu.
 
Aliwakumbusha polisi wanaominya uhuru wa kutoa maoni na kuandamana, wakumbuke kwamba katika mfumo wa demokrasia ya kweli, si lazima wananchi waimbe wimbo mmoja. “Katika demokrasia sio lazima kila mtu aimbe wimbo huo huo...uhuru wa mawazo ni wa msingi sana… unachukuliwa kama kitu cha kawaida, kila mtu ana haki ya msingi juu ya suala lolote linalogusa watu kwa jumla,” alisema.
 
Jaji Samatta alisema maandamano sio mtazamo potofu kama inavyodhaniwa na polisi, ndio maana katika nchi za mabara ya Ulaya, Amerika na Asia, ‘upepo’ huo unaendelea kutumiwa na wananchi kudai haki zao.
 
Alisema kuzuia maadamano kunaminya fursa kwa watawala kufahamu mambo mengi kutoka kwa waliowaweka madarakani, hasa kuhusu kitu wanachokitaka na wasichotaka. “Kwa nini wananchi wasiruhusiwe kutumia maandamano, kuwajulisha watawala kuhusu mambo yanayowakera ili yapatiwe ufumbuzi,” alihoji.
 
Hata hivyo, Jaji Samatta alisema ingawa haki ya kuandamana ina mipaka yake, lakini mipaka hiyo imewekwa na sheria na wala si jeshi la polisi. Hata hivyo, Jaji Samatta, alisema ipo haja kwa wananchi kutii sheria, kwa vile hali hiyo inachochea kustawisha demokrasia na uhuru.
 
“Vyombo vya serikali vinawajibika kwa sheria, kama ilivyo kwa mwananchi,” alisema.
 
AONYA KULIPIZA VISASI
 
Jaji Samatta alisema vitendo vya kulipiza kisasi si utamaduni unaoendana na ustaarabu wa taasisi za umma hususani vyombo vilivyo chini ya serikali, badala yake kuwajibika kwa mujibu wa sheria.
 
Alisema inapotokea vyombo hivyo kuipinda au kuidharau sheria, ‘tiba’ si vurugu, bali kuziomba mahakama zitamke juu ya uhalali wa vitendo hivyo na kuchukua hatua nyingine za kisheria.
 
AHIMIZA UWAJIBIKAJI ASASI ZA KIRAIA
 
Jaji Samatta alisema asasi zisizo za serikali, zinazoshughulikia haki za binadamu zinapaswa kuwajibika zaidi, zikisaidiana na vyombo vingine ndani ya nchi.
 
Chanzo - Nipashe

2 comments:

  1. Heko jaji Samatta kwa kusema ukweli, maneno hayo hayo akiyasema UAMSHO au AMANI KARUME inakuwa nongwa je jaji samata nae ni UAMSHO. Mwenyezi Muungu kaahidi kwamba siku zote haki itakuja juu tu na hayo sasa tunayaona kutoka kwa watu kama hawa. Tuendelee kusema ukweli na kudai haki zetu hata kama watawala watachukia.

    ReplyDelete
  2. Alichokisema Jaji Samatta sio kitu kigeni wala siokitu cha kukumbushwa kwa mtu mzima yeyote mwenye akili timamu analielewa hilo,lilopo katika maisha yetu ya kila siku katika Nchi za kiafrika ambazo zinajidai zinafuata mfumo wa Vyama vingi ni waongo na wanafiki mtupu,Ukizifuatilia kwa karibu Nchi zote ambazo zinafuata mfumo wa Vyama vingi(Multiples Parties System)kinadharia utaona ni hivyo lakini kiutendaji bado wamo katika Mfumo wa Chama kimoja (Single Parties System) Lakini Sitaki niende mbali sana kimazungumzo yangu nia yangu ni kueleza uoza ambao unafanywa na Polisi wa hapo kwetu Zanzibar wanaendeshwa kwa remote ambayo imeshikwa na viongozi wa Nchi ndio maana wanasababisha matatizo yote hapo kama wao wasingefunagama na upande wowote ule hiyo Nchi ingekuwa yakupigiwa mfano kwa amani yake lakini kinyume na hayo wananchi wanaishi kwa wasiwasi na woga mtupu.Kwa ujumla ukiangalia sisi Zanzibar tulitakiwa tuwe waalimu kwa Nchi nyengine juu ya Vyama vingi kwani huko nyuma kabla ya Mapinduzi tulikuwa tunatumia mfumo wa Vyma vingi iweje le watu wasizikane,wahasimiane ,wasiulizane na wala wasisemeshane sababu eti ni siasa ya Vyma vingi,Viongozi wa Serikali mnachotakiwa acheni ubinafsi na ujinga mmmekula kiapo kwa Kushika Msahafu maneno ya Mwenyezi Mungu iweje muwatese raia zenu waliokuchagueni kwa kufurahisha wachache? mtamweleza nini Mwenyezi Mungu?mnajidai kuingia Misikitini kusali na Sigida kubwa usoni kumbe hamna chochote zaidi ya unafiki na kuchuma dhambi tu,na nyie Viongozi wa Polisi kuweni makini acheni kuonea raia je mkisha staafu mtaishi vipi na hao raia ambao kwa sasa mnawanyanyasa?nataka niwakumbushe kidogo kwa Mungu hakuna Kubwa lolote liweza kutoke juu yenu.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.