Na Salum Vuai, Maelezo
BAADA ya kuwepo taarifa za mchezaji Seif Abdallah ‘Karihe’ wa Ruvu Shooting kwamba anatarajia kujiunga na Azam FC katika usajili wa dirisha dogo, klabu ya akademi ya Oranje ya Zanzibar imeibuka na kudai kuwa mchezaji huyo ni mali yake na timu hiyo iwasiliane nayo.
Mchezaji huyo ambaye kwa sasa yuko Uganda na timu ya taifa ya Zanzibar Heroes, amesajiliwa na Ruvu Shooting inayocheza ligi kuu ya Tanzania Bara, na hadi sasa amepachika magoli saba kwenye ligi hiyo ya Vodacom.
Mmoja wa viongozi wa akademi hiyo Ali Saleh ‘Alberto’, amedai kuwa klabu yake haikushirikishwa wala kuombwa kumtoa nyota huyo, na imepeleka malalamiko yake Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa.
Ametoa tahadhari kwa klabu ya Azam au nyengine yoyote itakayotaka kumsajili mchezaji huyo kuhakikisha inafanya mazungumzo na uongozi wa Oranje, kwani ndiyo iliyomlea na yenye haki naye, na kwamba usajili wake Ruvu Shooting haukufuata taratibu.
“Nimesoma katika gazeti moja kwamba Karihe anakwenda Azam mwezi Januari, lakini ninaomba ifahamu kuwa mchezaji huyo hayuko kihalali Ruvu Shooting, bali ni mali ya akademi yetu ya Oranje. Hatua yoyote kumsajili bila kutushirikisha ni batili”, alifafanua Alberto.
Aidha, uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa, hakuna barua yoyote iliyotolewa na ZFA kwenda Ruvu Shooting wala TFF kubariki usajili wa mwanandinga huyo chipukizi na mahiri wa kuzifumania nyavu.
Mchezaji huyo ambaye yuko Uganda, amekaririwa akiisifu Azam kwamba ni timu kubwa na tayari ameamua kujiunga nayo wakati wa usajili wa dirisha dogo mwezi Januari.
No comments:
Post a Comment