Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KLABU bingwa ya soka Tanzania Bara Simba, inatarajiwa kupiga kambi nchini Oman, kwa ajili ya kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara pamoja na ligi ya mabingwa Afrika.
Habari zilizopatikana kutoka ndani ya uongozi wa Simba, zimefahamisha kuwa, Simba itakwenda nchini humo kwa mwaliko wa klabu kongwe ya huko, Fanja FC.
Ikiwa huko, Simba itacheza pia mechi za kujipima nguvu dhidi ya timu tishio katika ligi kuu ya Oman, wakiwemo wenyeji wao hao, Fanja FC.
Simba inakuwa timu ya tatu ya ligi kuu kuwa katika mpango wa ziara ya nje ya nchi, baada ya wapinzani wao katika mbio za ubingwa msimu huu, Yanga na Azam nao kutangaza ziara zao.
Wakati Azam watakwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ndani ya siku mbili hizi, Yanga watakwenda Uturuki mwishoni mwa mwezi huu.
Mbali na ligi kuu na ile ya mabingwa Afrika, mapema Januari Simba na Yanga zitacheza pia klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, michuano ambayo itafanyika mjini Kigali, Rwanda.
Yanga itashiriki michuano hiyo kama mabingwa watetezi, baada ya kutwaa kombe hilo Julai mwaka huu mjini Dar es Salaam, wakati Simba watakwenda kwa tiketi ya kuiwakilisha nchi kwenye michuano hiyo, wakiwa mabingwa wa Bara.
Kwa miaka miwili mfululizo, timu za Bara zinaonekana kurejesha utawala wake kwenye michuano hiyo, kutokana na fainali mbili mfululizo zilizopita kuzikutanisha timu za Tanzania tupu.
No comments:
Post a Comment