Habari za Punde

Speech ya Mhe Said Ali Mbarouk akizindua kikao cha makamishna wa Utalii Zanzibar

HOTUBA YA MHE. WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, UTALII NA MICHEZO KATIKA UZINDUZI WA MAKAMISHNA WA KAMISHENI YA UTALII – ZANZIBAR TAREHE 30/12/2012 – BWAWANI HOTEL #
 
MHE. NAIBU WAZIRI WIZARA YA HABARI, UTAMADUNI, UTALII NA MICHEZO - ZANZIBAR MHE.
 
KATIBU MKUU WIZARA YA HABARI, UTAMADUNI, UTALII NA MICHEZO - ZANZIBAR
 
MHE. MWENYEKITI KAMISHENI YA UTALII – ZANZIBAR
MHE. KATIBU MTENDAJI KAMISHENI YA UTALII – ZANZIBAR
WAHESHIMIWA. MAKAMISHNA KAMISHENI YA UTALII - ZANZIBAR
WAHESHIMIWA. VIONGOZI MBALI MBALI
WAHESHIMIWA.
WAALIKWA MABIBI NA MABWANA ASSALAM ALLEYKUM:
 
Mhe. Mwenyekiti, Awali ya yote, sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na mjuzi wa kila kitu, kwa kutujaaliya sote sisi uhai na uzima na kutuwezesha kukutana hapa leo hii.
 
Aidha, ninamuomba Mwenyezi Mungu atujaaliye shughuli yetu hii ya leo, iwe ya kheri, baraka, amani na mafanikio, ili tufike lengo na azma tuliyokusudia.
 
Mhe. Mwenyekiti, Nina heshima kubwa tena kuitumia nafasi hii adhimu kwangu kukupongeza wewe binafsi pamoja na Katibu Mtendaji kwa kuteuliwa kwenu na Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kushika nyadhifa mulizopewa.

 Zaidi ninawashukuru kwa kuukubali uteuzi wenu. Sambamba na hili ninatumia nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru Makamishna wote kwa kupata uteuzi wao na kuukubali.
 
Kwangu mimi binafsi, hali hii imenipa faraja na heshima kubwa kwamba uteuzi uliofanywa na Mhe. Rais pamoja na mimi Waziri wenu, haukuwa na makosa.
 
Mhe. Mwenyekiti, Kamisheni ya Utalii Zanzibar ni chombo kilichoundwa kwa mujibu wa Sheria, kwa lengo la kusimamia, kuendeleza na kuutangaza Utalii wa Zanzibar ndani na nje ya nchi yetu.
 
Chombo hiki tokea kuundwa kwake mwaka 1992, kimepitia katika vipindi mbalimbali kimuundo na kukabiliana na changamoto tofauti. Katika kuimarisha muundo wa utendaji wake kwa lengo la kuongeza ufanisi na tija kwa Taifa, Serikali ya awamu ya saba, chini ya uongozi wa Dkt. Ali Muhammed Shein, imepitisha sheria nambari 7 ya mwaka 2012, ambayo imefanya marekebisho yaliyopelekea kuundwa kwa Baraza hili la Makamishna. Nirudie tena kuwapongeza siyo tu kwa kuteuliwa kwenu, bali nyinyi kuwa Makamishna wa kwanza katika muundo huu mpya wa Kamisheni ya Utalii.
 
Mhe. Mwenyekiti, Sote sisi tunajua kwamba, Utalii kwa hapa Zanzibar ndio sekta kiongozi katika uchumi wa nchi yetu. Sekta hii inachangia wastani wa asilimia 27 ya pato la Taifa na wastani wa asilimia 80 ya fedha za kigeni zinatokana na sekta ya utalii.
 
Aidha, utalii kwa ujumla wake umesaidia na unaendelea kusaidia kutoa ajira kwa Wazanzibari wa rika na jinsia zote, ambapo kiasi cha watu 12,000 wamepata ajira ya moja kwa moja na wengine wapatao 46,000 wanategemea kipato chao kupitia sekta ya utalii, kwa ama kuuza au kutoa huduma mbali mbali. Kadhalika sekta ya utalii inasaidia uhifadhi wa mazingira ya asili na kuongeza haiba ya nchi yetu.
 
Mhe, Mwenyekiti na Makamishna, Dira ya 2020, na Mkakati wa Kukuza Uchumi, na Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA), kwa pamoja vinalenga kufikia ukuaji wa uchumi utakaowajali wananchi na zaidi wananchi masikini.
 
Utalii unalo jukumu kubwa katika ukuzaji wa uchumi wa Zanzibar na hatimaye kufikia lengo la kupunguza umasikini wa wananchi wake. Ushahidi tulionao unadhihirisha kuwa sekta hii tokea ianze kupewa kipaumbele katika miaka ya 80 baada ya mageuzi ya kiuchumi yaliyofanyika hapa Zanzibar, yaliyotokana na kuporomoka kwa zao la karafuu, imeweza kuleta mabadiliko yenye mafanikio katika uchumi wetu.
 
Takwimu za miaka 10 iliyopita zinaonyesha sekta ya utalii imepata mafanikio makubwa, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaokuja nchini, hadi kufikia watalii 175,056 kwa mwaka 2011.
 
Kadhalika ndani ya kipindi hiki uwekezaji katika mahoteli yenye hadhi ya juu imeongezeka, miundo mbinu ya barabara, bandari na uwanja wa ndege imeimarika, wigo wa masoko nao pia umekuwa.
 
Mhe. Mwenyekiti, Mbali na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta hii ya utalii, lakini bado utalii kwa ujumla wake hapa Zanzibar unakabiliwa na changamoto nyingi na kubwa. Hapa ndipo Makamishna nyinyi pamoja na Kamisheni yenu jukumu lenu la kwanza ni kubuni mbinu, mikakati na njia thabiti na endelevu za kutatua changamoto hizi zinazotukabili.
 
Kwa leo nitazitaja chache, nikiamini nyinyi ni weledi na hivyo mnazijua nyingi zaidi yangu. Mhe. Mwenyekiti, Changamoto ya kwanza inayotukabili ni utalii wenyewe. Utalii ni biashara inayobadilika kila kukicha, na kwa siku za hivi karibuni kasi ya mabadiliko imekuwa kubwa sana, ikipewa msukumo na mwendo kasi wa sayansi na teknolojia. Kwa msingi huo, ninaamini akili ya ubunifu ndio itakayotuwezesha kukabiliana na mabadiliko haya.
 
Changamoto ya pili ni kuwa utalii ni biashara yenye ushindani mkubwa sana. Kwetu sisi Zanzibar ambapo tupo katika utalii wa Visiwa tunashindana kwa karibu na wenzetu wa Seychelles, Mauritius, Maldives, Kenya ya Pwani (Mombasa) Tanzania Bara ya Pwani (Saadani, Mafia, Kilwa n.k), lakini pia tunashindana na utalii wa juu kama vile utalii wa mbuga.
 
Kukabiliana na changamoto hii hatuna budi kuja na mikakati thabiti na endelevu ya kutangaza vivutio tulivyonavyo na kubuni vivutio vipya. Ni kweli hali yetu ya fedha tulizowekeza katika matangazo na masoko siyo nzuri, lakini bado isiwe ni kikwazo.
 
Changamoto ya tatu ni ya mazoea ya kutegemea soko la nchi za ulaya kusini (Italy, England, Spain, Germany) na kwa kiasi fulani Marekani (USA). Nchi hizi kwa miaka ya karibuni hali zao za kiuchumi zimekuwa siyo nzuri. Idadi ya watalii wanaotoka katika nchi hizi imeonekana kupungua. Ili kukabiliana na hali hii, ni budi tuanze sasa kusaka masoko mapya katika nchi za Ulaya ya Mashariki, China, Mashariki ya mbali, Uarabuni, Afrika, wakati huo huo tukiyaimarisha masoko ya asili.
 
Changamoto ya nne ni juu ya suala zima la kukabiliana na wadau wa utalii wanaofanya shughuli zao bila ya kuzingatia sheria za nchi na zile za utalii. Mathalani tunao tatizo la watu wanaoitwa “Mapapasi” au watembezaji watalii wasio na vibali. Kadhalika zipo hotel zinazofanya shughuli za “Tour Operator”. Pia wapo watu ambao siyo Wazanzibari na wala siyo Watanzania wanaofanya kazi ambazo kwa mujibu wa sheria zinatakiwa zifanywe na Wazanzibari wenyewe au Watanzania.
 
Msingi wangu hapa ni kwa Makamishna pamoja na Kamisheni ya Utalii kuweka mkazo mkubwa na kuondokana na muhali katika kusimamia sheria ili zitekelezwe ipasavyo kwa kila mmoja wetu.
 
Changamoto ya tano, ni umuhimu wa kuwa na program za mafunzo kuhusiana na sekta hii ya utalii kwa watendaji wetu, na zaidi kwa vijana wetu wa Zanzibar, ili waweze kuingia katika soko la utalii lenye ushindani. Itakuwa aibu kwa Taifa letu, kuwa na kundi kubwa la vijana ambao wamebaki kuwa watizamaji katika maendeleo ya sekta hii ya utalii, na wakati huo huo wakiendelea kuilaumu Serikali yao kwa kukosa ajira.
 
Ninawaombeni katika kutekeleza majukumu yenu ya Ukamishna changamoto hii nayo muipe kipaumbele katika kupanga mikakati ya kukabiliana nayo.
 
Changamoto ya sita na ya mwisho kwa leo, ni utalii wa ndani na utekelezaji wa Dhana ya Utalii kwa Wote, yenye lengo la kumshirikisha na kumnufaisha mwananchi. Imebainika bado, utalii wetu haujafikia kiwango cha kuridhisha katika kumshirikisha kila mwananchi, ili awe sehemu ya utalii wa nchi yake na hatimaye kwa njia moja ama nyengine apate tija na faida zinazotokana na shughuli za utalii, bila ya kuathiri utamaduni na silka ya Mzanzibari.
 
Kufikia lengo hili, Baraza hili la Makamishna na Kamisheni ya Utalii kwa ujumla, hamna budi kuwa karibu sana na bila ya kujenga dhana yoyote, kushirikiana na Kamati za Utalii za Wilaya ambazo zimeundwa kwa mujibu wa Sheria. Aidha, sheria pia imeweka jukwaa la wadau wa utalii (Tourism stake holder forum) na kuzitambua jumuiya za kijamii (community based association) zenye mnasaba na harakati za utalii, nazo zitumieni ipasavyo ili kuufikia utalii kwa wote.
 
Mhe. Mwenyekiti na Makamishna. Kwa minajili ya uzinduzi wa Baraza lenu hili, nimeona ni vyema niyaeleze haya, lakini bado nina imani ya kwamba kwa uwezo na ujuzi mulionao mutaibua mambo mengi zaidi na kuweka mikakati mingi na mizuri zaidi, kwa lengo la kuleta ufanisi na tija katika sekta yetu hii ya utalii.
 
Mhe. Mwenyekiti, Mwisho, lakini siyo kwa umuhimu ninapenda kuwanasihi kufanya kazi kwa mashirikiano na maelewano, kwani vitu viwili hivi ndio siri kubwa ya mafanikio popote pale ulimwenguni.
 
Tumewapeni jukumu la kuiendeleza sekta ya Utalii, na sisi Serikalini tunasubiri ushauri wenu, ili kwa pamoja tuwe na utalii endelevu na wenye tija.
 
Mhe. Mwenyekiti, Mwisho kabisa kwa heshima ninatumia wasaa huu kutamka rasmi kuwa ninazindua kikao cha Makamishna wa Kamisheni ya Utalii – Zanzibar.
 
Na nina washukuru sana kwa kunisikiliza. AHSANTENI SANA

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.