na Hassan Ali
CHAMA cha Walimu Zanzibar (Zatu), kimesema walimu wengi hawajalipwa posho zao za likizo tangu walipochukua likizo mwaka jana.
Katibu Mkuu wa Zatu, Mussa Omar Tafurwa, alibainisha hayo mwishoni mwa wiki alipozungumza na waandishi wa habari na kuongeza kuwa walimu wamekuwa wakipewa likizo bila ya malipo kinyume na sheria ya utumishi wa umma ya Zanzibar.
Alisema kwa mujibu wa taratibu na sheria, kila mwalimu anatakiwa kulipwa posho ya likizo ya sh 100,000 badala ya 30,000 baada ya serikali ya Umoja wa Kitaifa kufanya marekebisho ya kiwango hicho mwaka jana.
Alisema Zatu imepokea malalamiko mengi kutoka kwa baadhi ya wanachama wake kutolipwa posho hiyo na kusababisha wengi kukwama kusafiri nje ya vituo vyao vya kazi.
“Kuna walimu Zanzibar wamepewa likizo mwaka 2011, mpaka kufika sasa Desemba mwaka huu hawajalipwa posho za likizo kinyume na sheria za utumishi,” alisema Tafurwa.
Alisema tatizo hilo limekuwepo muda mrefu, lakini viongozi wa Wizara ya Elimu na mafunzo ya Amali Zanzibar (Wema) wamekuwa wakikwepa kukutana na viongozi wa Zatu kuzungumzia matatizo ya walimu visiwani Zanzibar.
Tafurwa alisema Zatu imeamua kufanya mkutano wa waandishi wa habari, ili serikali iweze kufahamu akiwemo Rais wa Zanzibar baada ya viongiozi wa Zatu kushindwa kupata ushirikiano kutoka kwa viongozi wenye dhamana wa wizara hiyo.
Tafurwa alisema kwa mujibu wa sheria, kila mwalimu hutakiwa kupewa kila mwaka likizo ya siku 28, lakini wizara hiyo imekuwa ikiwapa siku 12 kinyume cha sheria.
Chanzo - Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment