Na Madina Issa
KATIKA kuukaribisha mwaka mpya wa 2013, uongozi wa hoteli ya kitalii ya Blue Oyster iliyoko Jambiani Wilaya ya Kusini Unguja, juzi uliendesha shindano la resi za ngarawa lililoshirikisha wananchi wa kijiji hicho.
Jumla ya ngarawa 20 zilishiriki katika mfukuzano huo, ambapo ngarawa iliyopewa jina la Safari njema inayomilikiwa na Salum Makame, iliibuka ya kwanza.
Nafasi ya pili ilikwenda kwa nahodha Juma Abdi, aliyetweka akiwa ndani ya ngarawa iitwayo ‘Joy of Missing’, huku ngarawa ‘Sihaba’ iliyoendeshwa na nahodha Joji ikifuata katika nafasi ya tatu.
Mkuu wa Wilaya ya Kusini Haji Makungu Mgongo, alizindua resi hizo, na baadae kukabidhi zawadi, ambapo mshindi wa kwanza alipata shilingi laki moja, wa pili elfu 80, na aliyeibuka wa tatu akakunja bahasha ya shilingi elfu 50.
Aidha, washiriki wengine walifutwa jasho kwa tunza ya shilingi elfu 20 kila mmoja.
Akizungumza baada ya mashindano hayo, mmiliki wa hoteli ya Blue Oyster Cluus Beiser, alisema lengo la kuandaa mchuano huo, ni kuwaweka pamoja watu wa Jambiani na wawekezaji, na kuunganisha nguvu katika kuupeleka mbele utalii na kuviendeleza vijiji vyao.
Aliwashauri wamiliki wa hoteli mbalimbali, kuwa karibu na wanakijiji ili kuwasaidia na kuwaelimisha juu umuhimu wa kutunza mazingira
No comments:
Post a Comment