Habari za Punde

Dk. Shein :Bado kilomita 83 tu barabara za lami

Aahidi kuendelea kuimarisha elimu
Na Mwantanga Ame, Bakar Mussa,Pemba
WAKATI wananchi wa Zanzibar wakiadhimisha miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar Januari 12, serikali imesema imefanikiwa kutandaza mtandao wa barabara safi za lami kilomita 560 na kubakiwa na kilomita 83 katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, aliyasema hayo wakati akifungua rasmi barabara ya Misufini hadi Bumbwini.
Dk. Shein, alisema wananchi wa Zanzibar wana kila sababu ya kufurahia uhuru huo, kwani serikali yao imefanikiwa kuwatandazia mtandao mkubwa wa barabara nchini kote kwa kilomita 560 jambo ambalo ni tofauti na nchi nyengine.
Hatua hiyo serikali Dk. Shein alisema imesaidia kwa kiasi kikubwa kuinua maisha ya wananchi wa katika shughuli zao za maendeleo ya kila siku.
Alisema hivi sasa serikali inajiandaa kukamilisha kazi ya ujenzi wa barabara za Unguja na Pemba ambazo ni kilomita 83 ambazo zitajengwa kwa kiwango cha lami.
Alisema kuwepo kwa mtandao mkubwa wa barabara umeiwezesha serikali kupiga hatua ya kuweka mazingira bora ya mabadiliko ya uchumi katika sekta za utalii, uvuvi, afya na biashara.
Alisema jambo la msingi kwa wananchi baada ya kupata barabara ni kuzitumia vizuri kwa kuzingatia faida za kiuchumi na usalama wa maisha ya watu wote.
Dk.Shein, alizitaka mamlaka husika kutimiza wajibu wao kwa kuhakikisha wanasimamia vyema sheria za ujenzi kwa kutoruhusu ujenzi wa nyumba za makaazi na maduka maduka kwenye hifadhi ya barabara.
Alisema inasikitisha kuona baadhi ya watu kuamua kujenga karibu ya barabara jambo ambalo ni hatari.
Aliwapongeza wananchi wa Jimbo la Bumbwini kwa jitihada zao walizozionesha kwa kuwa wastahamilivu katika kipindi chote walichokuwa hawana barabara ya lami.
Aidha aliipongeza Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa jitihada inazozichukua kusaidia maendeleo ya Zanzibar kwani imefanya kuwepo mabadiliko makubwa katika sekta muhimu za utoaji huduma za kijamii.
Mwakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Tonia Kandiero, akitoa maelezo yake aliipongeza serikali ya Zanzibar kwa jitihada ilizozifanya kuinua sekta ya huduma za kijamii.
Alisema hivi sasa Benki hiyo inajiandaa kuyaangalia maeneo mapya ya kiuchumi ambayo wataweza kuisaidia Zanzibar likiwemo suala la kuimarisha miundombinu ya huduma ya maji safi na salama.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano, Dk. Juma Maliki Akili alisema barabara ya Mfenesini hadi Bumbwini ina kilomita 13.2 na kuchelewa kwake kukamilika kulitokana na serikali kuchelewa kulipa fidia za nyumba, kuondosha mabomba ya maji, nguzo za umeme, waya za redio, mvua kubwa na kuharibika kwa vifaa vya ujenzi.
Alisema mradi huo, unaojumuisha madaraja na ulipaji wa fidia, serikali, imetumia jumla ya shilingi bilioni 10.6 ambapo barabara hiyo ilitumia shilingi bilioni 8.2 na shilingi bilioni 2.07 kwa madaraja ya Mwanakombo, Mto Kipange, Mto wa Maji na kalvati ya Mkokotoni na shilingi milioni 87.7 zililipwa fidia.
Mwakilishi wa kampuni ya MECCO alisema licha ya kukamilisha mradi huo lakini bado amekuwa akikabiliwa na changamoto kubwa ya deni ambalo kampuni hiyo inaidai serikali linalofikia shilingi bilioni 5.
Waziri wa Wizara hiyo Rashid Seif, akitoa maelezo yake aliishukuru Benki ya AfDB, kwa michango yake inayoendelea kuipatia serikali ya Zanzibar na wananachi wake.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Pembe Juma Khamis, aliwapongeza wananchi wa vijiji iliyopita barabara hiyo kwa kuwa wastahamilivu katika kipindi chote walichokuwa hawana barabara.
Barabara ya Mfenesini hadi Bumbwini, kwa mara ya mwisho ilijengwa mwaka 1927.
Wakati huo huo Dk.Shein, amesema serikali ya itaendelea kuwajengea mazingira mazuri ya kielimu wananchi wake.
Akizungumza na wananchi katika skuli ya sekondari Madungu baada ya kufungua skuli hiyo, alisema Zanzibar imekuwa ikiwajengea mazingira bora ya kielimu wananchi wake kwa kuwajengea skuli za kisasa zenye huduma mbali mbali kama vile maabara,vitabu vya masomo ya sayansi ili Zanzibar iweze kuwa na wataalamu wa fani mbali mbali.
Alifahamisha kuwa malengo ya millenia ni kuwa kila mtoto alie na uwezo wa kwenda skuli ifikapo mwaka 2015, aweze kupata nafasi ya masomo, ambapo kwa Zanzibar tayari imeshatekeleza malengo hayo hata kabla ya kufika mwaka huo.
Dk. Shein, alieleza kuwa hivi sasa Zanzibar inajivunia kwa kuwa na vyuo vyake vikuu vitatu vinavyotoa masomo ya fani mbali mbali , hivyo ni wajibu wa wazazi kuwa na mashirikiano na walimu kwa kuwahimiza watoto kusoma kwa bidii.
“Hayo ndio malengo ya Mapinduzi ya mwaka 1964, lengo lake ni kuwapatia elimu bila ya malipo watoto wote wa nchi hii, kwani kabla ya Mapinduzi haikuwa rahisi watoto wa wanyonge kupata elimu na wala hakukuwa na skuli kama hizi,” alisema.
Aliwataka wazazi kuendelea kuchangia elimu kwani gharama za masomo zimekuwa kubwa, hivyo sio vibaya kuisaidia serikali.
Aidha aliipongeza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kufanikisha mradi mkubwa kama huo wenye kutumia fedha nyingi za wahisani.
Alisema kisiwa cha Pemba kitakua na skuli 12 za kidato cha sita na serikali itajenga tawi la chuo kikuu cha taifa (SUZA) katika kijiji cha Mchangamdogo Mkoa wa Kaskazini Pemba muda mfupi ujao.
Nae Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Abdalla Mzee Mpangile, alisema kumalizika kwa ujenzi wa skuli hiyo kunaifanya wilaya ya Chake Chake kuwa na skuli nne zenye kusomesha wanafunzi wa kidato cha sita.
Alisema ujenzi huo ni miongoni mwa mradi wa ujenzi wa skuli 16 za Zanzibar, kwa mkopo wa Benki ya Dunia uliogharimu dola miioni 42.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.