Na Mwandishi wetu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya
Mrisho Kikwete amekemea tabia ya baadhi ya viongozi wa kisiasa kutumia suala la
raslimali za taifa, ikiwamo gesi asilia kujifatufia umaarufu wa kisiasa na
kuwapotosha wananchi.
Aidha, Rais Kikwete alisema ni jambo la hatari na
lisilo na tija kwa wanasiasa kujaribu kuigawa nchi vipande vipande kwa sababu
ya kujitafutia umaarufu kwa kutumia raslimali za taifa.
Rais Kikwete aliyasema hayo jana wakati
alipokutana na Balozi wa Uingereza nchini ambaye anamaliza muda wake, Dianne
Corner ambaye alifika Ikulu, Dar Es
Salaam kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi katika Tanzania.
Rais Kikwete na Balozi Corner wamezungumzia
masuala mbali yanayohusu uhusiano kati ya Tanzania na Uingereza, masuala ya
ukanda wa Afrika Mashariki na masuala ya kimataifa.
Kuhusu ugunduzi wa gesi asilia uliofanywa na kampuni
BG ya Uingereza katika eneo la Msimbati kwenye bahari ya Hindi, walikubaliana
kuwa hilo ni jambo jema na lenye kuleta matumaini kwa Tanzania hasa wakati
itakapoanza kuvunwa katika miaka michache ijayo.
Kuhusu siasa zilizoanza kujitokeza kufuatia
ugunduzi huo mkubwa wa gesi asilia, Rais Kikwete alisema ni tabia ya hatari kwa
wanasiasa kutumia gesi asilia ama raslimali nyingine kujijengea umaarufu wao
ambao umeporomoka.
“Unawezaje kuwa na nchi moja na taifa moja wakati
kila mmoja anadai raslimali kutoka kwenye eneo moja ibakie na kunufaisha watu
wa eneo hilo tu. Huwezi kuwa na nchi moja na yenye umoja wakati kuna nchi ya
gesi asilia kule Mtwara, kuna nchi ya kahawa kule Kilimanjaro, kuna nchi ya
chai na ndizi kule Bukoba,” alisema.
“Kwa sababu kama gesi asilia inatakiwa kubakia na
kunufaisha watu wa Mtwara tu, basi wenye haki zaidi ya kudai jambo hili siyo
watu wa Mtwara bali ni watu wa Msimbati ambako ndiko ilipogunduliwa gesi ambako
ni maili 60 kutoka Mtwara, kilomita 200 kutoka Newala,” alisema.
"Unajua nchi yetu inao baadhi ya wanasiasa
wenye uchu wa umaarufu na ambao wanatumia jambo hili jema kwa manufaa yao
binafsi bila kujali umoja na jadi ya taifa letu la raslimali zetu kutumika
kuiendeleza nchi nzima,” aliongeza.
Kuhusu uhusiano kati ya Tanzania na Uingereza,
Rais Kikwete alimshukuru Balozi Corner kwa kazi nzuri ya kuimarisha uhusiano
huo.
“Umeufikisha uhusiano wetu kwenye hatua ya juu
kabisa na tunakushukuru kwa jambo hili,” alisema.
Corner ambaye amekuwa Balozi wa Uingereza nchini
Tanzania kwa miaka minne amehamishiwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
No comments:
Post a Comment