Na Mwantanga Ame
IDADI ya Watanzania imefika watu milioni 44,929,002 ambapo Tanzania Bara kuna watu milioni 43,625,434 na Zanzibar kuna watu 1,303,568.
Akitangaza matokeo ya sensa ya watu na makaazi kitaifa katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete alisema, ongezeko hilo ni mzigo mkubwa kwa taifa, jamii na kwa uchumi wa kuwahudumia.
Alisema idadi hiyo ni ongezeko la wastani wa asilimia 2.9 ya idadi ya watu katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Alisema takwimu hizo zinadhihirishwa kwamba ifikapo mwaka 2016 idadi ya Watanzania itakuwa milioni 51.5.
Hivyo alisema lazima serikali iandae mikakati madhubuti na mikakati hiyo ionekane katika mipango ya maendeleo ya taifa ya kila siku.
Alisema kwa upande wa serikali, itazitumia takwimu hizo hizo kupanga mikakati endelevu pamoja na kuimarisha huduma muhimu za kijamii utaosaidia kupatikana kwa mahitaji ya kijamii kwa uwiano unaoridhisha.
Kwa upande wa familia alisema, inapaswa kuona umuhimu wa kupanga uzazi vyenginevyo hali ya maisha itashuka sana.
“Ushindani wa huduma utakuwa mkubwa, hivyo suala la kupanga uzazi ni muhimu sana. Lazima ujipangie kuwa na familia ambayo utaweza kuihudumia,” alisema Rais Kikwete.
Alisema hiyo ni sensa ya tano kufanyika baada ya Muungano ambapo sensa ya kwanza ilifanyika mwaka 1967, sensa ya pili mwaka 1978, sensa ya tatu mwaka 1988 na sensa ya nne ilifanyika mwaka 2002.
Alisema katika sensa ya kwanza Watanzania walikuwa ni milioni 12,312,954 ambapo Tanzania Bara ilikuwa na watu milioni 11,958,554 huku Zanzibar ni watu 354,400.
Alisema kuongezeka kwa idadi itawalazimu wananchi na watendaji serikalini kufanya kazi kwa bidii zaidi ili kukuza uchumi utakaoweza kwenda sambamba na mahitaji ya watu.
Dk. Kikwete alisema, matokeo ya sensa hiyo yataweza kusaidia kila taasisi kuweza kuzitumia na kupanga mipango yao ya maendeleo.
Aliwashangaa baadhi ya viongozi kutumia muda wa sensa kushawishi watu kufanya vurugu huku wakisahau kuwa matokeo ya sensa hiyo ni kwa ajili ya watu wote.
Aliwapongeza Watanzania, viongozi wa dini, vyombo vya habari, wasanii, viongozi wa vyama pamoja na mashirika ya kimataifa likiwemo shirika UNFPA, JICA na wengine, kwa kufanikisha sensa hiyo na kuahidi kuendeleza kushirikiana nao.
Alisema ni vyema kwa washirika wa maendeleo kuona wanaendeleza michango yao kwa Watanzania ili kufanikisaha mipango yao ya maendeleo.
Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda, ambae ni Mwenyekiti mwenza wa sensa aliwapongeza wananchi wa Tanzania na watendaji mbali mbali wa waliofanikisha sensa.
Alisema sensa ya mwaka uliopita ilifadhiliwa na serikali kwa asilimia 90 na asilimia iliyosalia mchango wa washirika wa maendeleo tofauti na sensa ya mwaka 2002 ambapo mchango wa serikali ulikuwa asilimia 70.
Aidha alisema zoezi hilo lilikumbwa na changamoto mbali mbali na kusababisha watu wanne kupoteza maisha na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, akitoa hotuba yake alisema serikali imekamilisha kazi hiyo na ni vyema kwa watendaji wa serikali kuona wanazitumia vyema takwimu hizo.
Alisema watendaji wa serikali watalazimika kuzitumia takwimu hizo kwa kufanikisha mipango ya maendeleo ya kitaifa ukiwemo wa MKUKUTA na MKUZA II.
Balozi Seif, aliwapongeza wananchi wa Zanzibar na Tanzania Bara kwa kuhakikisha wanahesabiwa.
Waziri wa Fedha Tanzania, Dk. Wiliam Mgimwa alisema matokeo ya sensa hiyo yatachangia maendeleo ya Watanzania na kuiwezesha serikali kutunga sera na namna ya kuweza kutoa huduma kwa wananchi kwa kuangalia mahitaji yao.
Alisema wizara inakusudia kuzitawanya takwimu za sensa hiyo hadi kwa wananchi vijijini ikiwa ni sehemu ya kuisaidia jamii kuweza kujitathmini namna ya kupanga maendeleo yao.
Alisema takwimu hizo zitawawezesha Watanzania kujitathmini kimaendeleo kwa kutambua wapi Tanzania ilipo na inapohitaji kuelekea.
Alisema pia serikali inakusudia kuziweka takwimu za sensa hiyo katika mitandao ya kimataifa ikiwemo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, SADDC na Divisheni ya Takwimu kwa nchi za Afrika.
Mapema Kamishna wa Sensa na Makaazi Tanzania, Hajat Amina Mrisho Said, aliwapongeza Watanzania kwa kushiriki katika sensa jambo ambalo limeifanya serikali kuweza kukamilisha kazi hiyo kwa haraka ndani ya kipindi cha mienzi minne.
Kamishna huyo, alisema kukamilika kwa sensa hiyo ni mwanzo wa matayarisho ya sensa ya makaazi ijayo na serikali itahakikisha inatoa machapisho ya sensa hiyo kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza hadi kufikia mwezi Juni 2014.
Akitoa shukrani, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Zanzibar, Omar Yussuf Mzee, alisema Watanzania watapaswa kuiangalia kwa umuhiumu wake changamoto ya ukuaji wa idadi ya watu na namana ya kufikiria kupanga uzazi.
Alisema kupanga uzazi ni muhimu na wanaume lazima washiriki zaidi wanaume badala ya kuwawekea mkazo wanawake pekee.
Viongozi wengine waliohudhuria uzinduzi huo ni Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, Mawaziri wa serikali ya Zanzibar na Tanzania Bara, Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa yaliyopo Tanzania.
No comments:
Post a Comment