Habari za Punde

Wawili wafariki kwa kutumbukia bwawani

Na Merina Robert,Morogoro
WATU wawili wamefariki dunia baada ya kutumbukia kwenye mabwawa ya maji huku mmoja chanzo kikiwa ni ulevi wa kupindukia na mwingine inadhaniwa kuwa ni kutokana na ugonjwa wa kifafa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa polisi mkoani hapa, Faustine Shilogile alisema tukio la kwanza lilitokea Disemba 28 majira ya saa 5 asubuhi eneo la mashambani katika bwawa la Mzange Kigugu kata ya Sungaji Wilaya ya Mvomero mkoani hapa.

Kamanda Shilogile alisema katika tukio hilo mwili wa mwanamme aliyefahamika kwa jina moja la Mkagule ulikutwa ukielea kwenye bwawa la maji na baada ya uchunguzi wa awali ilibainika kuwa ni ulevi wa kupita kiasi, hata hivyo polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi.

Katika tukio jingine lililotokea Disemba 28 majira ya saa 11 jioni maeneo ya Mwandi kata ya Magubike tarafa ya Magole Wilaya ya Kilosa ambapo Shilogile alisema kuwa mwanamme aliyefahamika kwa jina la Yohna Daudi (15) alikutwa amekufa na mwili wake kuelea kwenye bwawa.

Alisema taarifa za awali zilizowafikia polisi zilidai kuwa mtu huyo alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kifafa na kwamba siku hiyo alikwenda kuoga kwenye bwawa hilo.

Wakati huo huo, mtu aliyefahamika kwa jina la Yasini Athumani (60) mkazi wa Tungi manispaa ya Morogoro amefariki dunia papo hapo baada ya kugongwa na basi dogo la abiria eneo la daraja la Shani barabara ya zamani ya Dar es Salaam.

Kamanda Shilogile alisema ajali hiyo ilitokea Disemba 29 majira ya saa 1:00 usiku wakati mtu huyo akiwa na baiskeli akitokea Bigwa kuelekea mjini.

Kamanda Shilogile alisema chanzo cha ajali ni mwendo kasi wa dereva wa basi hilo na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya mkoa kwa ajili ya uchunguzi.

Katika tukio jengine Kamanda Shilogile alisema polisi mkoani hapa inamshikilia mtu aliyefahamika kwa jina la Raymond Peter (34) mkazi wa Matambwe kwa tuhuma za kupatikana na nyama ya nyumbu wawili ambao thamni yake bado haijafahamika.

Alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa na askari wa mbuga ya Selou iliyopo Matambwe na kwamba mtuhumiwa huyo alikuwa na wenzake ambao walikimbia na polisi wanawatafuta.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.