Na Kunze Mswanyama,Dar es salaam
PAMOJA na serikali kuanzisha mfumo imara wa utoaji leseni za udereva kuanzia Oktoba 2010,hadi sasa ni madereva 616,349 tu ndio waliochukua leseni mpya huku magari zaidi ya 1,264,574 yakiwa yamesajiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hivyo kufanya jumla ya madereva zaidi ya 500,000 kuendesha vyombo vya moto bila leseni .
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa jana na Kamishna Msaidizi wa Polisi, Johansen Kahatano, leseni 135,721 ni za daraja C huku 480,628 zikiwa ni za madaraja mengine.
Takwimu hizo ni kwa nchi nzima.
Kwa takwimu hizo kuna uwezekano wa madereva wengi wanaendesha vyombo vya moto bila kuwa na leseni halali.
Wakati wa kubadilisha leseni hizo, kulikuwa na malengo kadhaa yaliyowekwa ili kuona usafiri wa barabarani Tanzania unakuwa wa kuaminika.
Lakini kubwa zaidi ilikuwa kupata takwimu za madereva wote nchini ambazo awali ilikuwa ni vigumu kupatikana kutokana na mfumo mbovu.
Kwa mujibu wa sheria ya usalama barabarani 168 iliyofanyiwa marekebisho 2002 kifungu19 na 25, kila mtu anayeendesha gari ni lazima awe na leseni inayoendana na gari analoliendesha pia ni kosa kuruhusu gari liendeshwe na asiyekuwa na leseni.
ACP Kahatano aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es salaam makao makuu ya TRA kuwa, malengo ya mpango wa utoaji leseni za mfumo wa “smart card” ulilenga kudhibiti pia upotevu wa mapato ya serikali,kuondoa leseni za kughushi na kuongeza udhibiti mienendo ya madereva nchini.
Alisema,mwisho wa kubadilisha leseni hizo za zamani bila usumbufu ili kupata ya sasa unaisha Machi 31 hivyo kuwataka madereva wote kujipatia leseni mpya haraka.
“Baada ya muda huo,ubadilishaji wa leseni yoyote hautafanyika na mfumo wa utoaji leseni utabadilika ili kubakia na uwezo wa kutoa leseni kwa madereva wanaoomba leseni kwa mara ya kwanza tu,” alisema.
“Baada ya muda huo tutaanzisha operesheni maalumu ili kubaini madereva wasio na leseni mpya,walio na zile zilizokwisha muda wake na hata wasio kabisa ana leseni ,”alisema.
Alisema katika operesheni hiyo,wataomba kila dereva kubeba leseni yake halali ili kuondoa usumbufu kwa kila mmoja huku akibainisha mambo kadhaa yatakayoangaliwa wakati wa ukaguzi kuwa ni pamoja na kama dereva anayo leseni kwa mujibu wa sheria,uhalali wa leseni,muda wa leseni na kama imetolewa na mamlaka husika.
Aliongeza kuwa, wataangalia pia kama gari limelipiwa ada ya gari ya kila mwaka,bima hai na kuhakiki utimilifu wa vyombo hivyo.
Alikemea madereva wa magari ya serikali na hasa yale ya majeshi kama Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),Polisi na Idara nyingine kuacha mtindo wa kudharau sheria za usalama barabarani kwa kuwa hakuna aliye juu ya sheria bila kuangalia anakofanyia kazi.
Aliwaonya kuwa,jeshi lake halitawaonea aibu askari yeyote atakaye kiuka sheria hizo kwa sababu yoyote ile.
No comments:
Post a Comment