ZANZIBAR NA
MUSTAKBALI WA MUUNGANO
Maoni Binafsi ya Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa
Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Katibu Mkuu wa The Civic United Front (CUF –
Chama Cha Wananchi)
UTANGULIZI
Nina
heshima kubwa ya kuwasilisha maoni yangu binafsi kwa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba kuhusiana na namna na jinsi nchi zetu mbili, Zanzibar na Tanganyika,
zinazounda Jamhuri ya Muungano zinavyopaswa kuongozwa kupitia mfumo mpya wa
kikatiba utakaopatikana baada ya kukamilika mchakato unaoendelea sasa wa kupata
Katiba Mpya.
Nafasi
iliyopo mbele yetu ni adhimu sana kwa wananchi wa Zanzibar na Tanganyika kutoa
maoni yao juu ya katiba mpya wanayoitaka ili kuamua khatima ya nchi zao,
wanataka ziwe na mahusiano ya aina gani na ziongozwe katika utaratibu upi.
Kwa
muktadha huo basi ni wazi Katiba inayokusudiwa kutoa muongozo kwa wananchi wake
inajengwa na mambo mengi ambayo kimsingi yanapaswa kujadiliwa kwa kina na
baadaye kufikia muwafaka wa kitaifa katika kupata Katiba Mpya.
Pamoja
na ukweli huo, ni ukweli pia kuwa kwetu sisi Wazanzibari ni fursa pekee ya kuangalia
upya uhusiano kati ya Zanzibar na Tanganyika, ni aina gani ya muungano
tunaoutaka na utakaoweza kukabiliana na changamoto zilizopo na kwa hivyo basi
maoni yangu yatajikita katika eneo hilo tu.
Tume
ya Mabadiliko ya Katiba imetoa mwongozo ambao unawataka watoa maoni wajikite
katika maeneo makuu tisa (9). Maeneo hayo ni kama ifuatayo:
(a)
Misingi na Maadili ya Kitaifa;
(b)
Madaraka ya Wananchi;
(c)
Muundo wa Nchi na Taifa ndani
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
(d)
Haki za Binadamu na Wajibu wa
Wananchi;
(e)
Ardhi, Maliasili na Mazingira;
(f) Mihimili
ya Nchi:-
(i)
Ardhi;
(ii)
Watu; na
(iii)
Utawala.
(g)
Mihimili ya Utawala:-
(i)
Serikali;
(ii)
Bunge; na
(iii)
Mahkama.
(h)
Serikali
za Mitaa, Muundo na Mamlaka yake;
(i)
Vyombo vya
Ulinzi na Usalama.
Yanapotazamwa kwa undani maeneo hayo itaonekana kwamba
takriban mengi si mambo ya Muungano na hivyo hayawahusu wananchi wa Zanzibar
ambao kwa mujibu wa Mkataba wa Muungano wa 1964 yanasimamiwa na Zanzibar
yenyewe ambayo ina mamlaka kamili (exclusive jurisdiction) kuhusiana na mambo
yote yasiyo mambo ya Muungano. Hata yale maeneo ambayo yanaweza kuwahusu
Wazanzibari kwa mfano misingi na maadili ya kitaifa, madaraka ya wananchi,
mihimili ya utawala (Serikali, Bunge na Mahkama) na vyombo vya ulinzi na
usalama, kuhusika kwao kutakuwa ni kwa kiasi kile yanapohusika na uendeshaji wa
Muungano. Ndiyo kusema kwamba jambo lililo katikati ya mjadala kwa Wazanzibari
katika mchakato huu ni Muungano wenyewe.
Kwa msingi huo, maoni yangu binafsi ninayoyatoa hapa yatajikita
kwenye kile ambacho Wazanzibari walio wengi wamekuwa wakikizungumzia mbele ya
Tume ya Mabadiliko ya Katiba – Muungano wa Zanzibar na Tanganyika. Sehemu kubwa
ya waraka wangu huu wa maoni ninayoyawasilisha mbele ya Tume ya Mabadiliko ya
Katiba msingi wake ni waraka wangu nilioutoa mwaka 2008. Nimeamua kuutumia
waraka huo kwa sababu kwa kiasi kikubwa bado maoni yangu na sababu zake
yanabaki kama yalivyokuwa. Kilichobadilika ni kile kinachohusu nini naamini
unapaswa kuwa ufumbuzi wa matatizo ya Muungano huu ambayo hayo ninayaeleza
mwishoni mwa waraka huu pamoja na sababu zilizopelekea mabadiliko hayo ya
fikra.
MISUKOSUKO
KATIKA MUUNGANO
Muungano wa Zanzibar na Tanganyika umepita katika masaiba
kadhaa tokea kuasisiwa kwake takriban miaka 49 iliyopita lakini mtikisiko
ulioukumba katika siku za karibuni ni mkubwa sana. Ni
mkubwa kwa sababu umegusa kiini cha Muungano huu ambapo suala linaloulizwa ni
iwapo kwa kule kukubali kushirikiana katika baadhi ya mambo, je, Zanzibar na
Tanganyika zimejifuta na hivyo kupoteza hadhi zake kama nchi? Hilo limekuwa
ndiyo suala kubwa linaloulizwa na Wazanzibari hasa baada ya Waziri Mkuu Mizengo
Pinda kutamka Bungeni kwamba Zanzibar si nchi.
Hakuna awezaye kubisha kwamba tokea kuasisiwa kwake,
Muungano huu umejengeka kutokana na misingi ya khofu, kutiliana shaka na
kutokuaminiana baina ya pande mbili zinazouunda, ambako wakati mwengine kumepelekea
hata kutishia uhai wa Muungano wenyewe.
Muungano umekuwa gumzo kuu katika takriban kila
mjadala wa katiba na siasa katika nchi yetu. Umejitokeza na kujionyesha hivyo
katika mwaka wa mwanzo wa Muungano kuhusiana na sakata la kuwa na Ubalozi wa
iliyokuwa Ujerumani Magharibi kwa upande wa Tanganyika na Ubalozi wa iliyokuwa
Ujerumani Mashariki kwa upande wa Zanzibar, kuhusiana na uwakilishi wa Zanzibar
katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na uanzishwaji wa Benki Kuu ya
Tanzania (BOT) mwaka 1964 – 1966, wakati wa kuunganisha vyama vya ASP na TANU
kuunda Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 1977, katika mjadala wa marekebisho ya
Katiba wa 1983/84 na hatimaye kujiuzulu kwa Rais wa pili wa Zanzibar Sheikh
Aboud Jumbe, wakati wa kuondolewa katika Uwaziri Kiongozi kwa mwandishi wa maoni
haya na hatimaye kufukuzwa katika CCM na wenzake 6 mwaka 1988, katika harakati
za madai ya kutaka kura ya maoni kuhusiana na Muungano huo mwaka 1989/90,
wakati wa mjadala wa kuanzishwa vyama vingi mwaka 1991, katika sakata la
Zanzibar kujiunga na Umoja wa Nchi za Kiislamu (OIC) mwaka 1993, wakati wa
mjadala wa G-55 kudai kuanzishwa kwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano
mwaka 1994, katika mjadala wa marekebisho ya 11 na 14 ya Katiba ya Muungano
mwaka 1994/95, wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 1995 na ule wa 2000 na
karibuni kabisa kuhusiana na suala la matarajio ya ugunduzi wa mafuta visiwani
Zanzibar, harakati za kuanzisha Shirikisho la Afrika Mashariki na pia baada ya
kupitishwa kwa Marekebisho ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 yaliyofanywa
mwaka 2010.
Ukiondoa kuibuka kwake katika mijadala mikubwa ya
kikatiba na kisiasa nchini, kwa upande mwengine katika uendeshaji wa shughuli
za Serikali za kila siku, “matatizo na vikwazo kadhaa ya kiutawala na
kiutendaji” vimekuwa vikiripotiwa kila mara kwamba vinakwamisha uimarishaji wa
Muungano.
Tume na Kamati kadhaa zimeundwa kuainisha matatizo ya
Muungano na kupendekeza njia za kuyatatua. Serikali ya Jamhuri ya Muungano
imeunda Tume na Kamati zifuatazo, miongoni mwa nyingi, kuhusiana na masuala
haya:
1.
Kamati ya Mtei
2.
Tume ya Jaji Francis
Nyalali (1991)
3.
Kamati ya Shellukindo
(1994)
4.
Kamati ya Shellukindo 2 ya kuandaa Muafaka juu ya Mambo
ya Muungano baina ya SMZ na SMT.
5.
Kamati ya
Jaji Mark Bomani (1995)
6.
Kamati ya
Jaji Robert Kisanga (1998)
7.
Kamati ya 'Harmonization'
8.
Kamati ya Masuala ya Simu (Kamati ya Kusila)
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) nayo kwa upande
wake iliunda Kamati zifuatazo kwa madhumuni hayo hayo:
1.
Kamati ya Baraza la Mapinduzi (Kamati ya Amina) ya 1992
2.
Kamati ya Rais ya Kupambana na Kasoro za Muungano (Kamati
ya Shamuhuna) ya 1997
3.
Kamati ya Rais Kuchambua Ripoti ya Jaji Kisanga (Kamati
ya Salim Juma Othman)
4.
Kamati ya Kuandaa Mapendekezo ya Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar juu ya Kero za Muungano (Kamati ya Ramia) ya 2000
5.
Kamati ya Baraza la Mapinduzi juu ya Sera ya Mambo ya Nje
6.
Kamati ya Rais ya Wataalamu juu ya Kero za Muungano ya
2001
7.
Kamati ya Baraza la Mapinduzi ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki
8.
Kamati ya Mafuta
9.
Kamati ya Madeni baina ya Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar na Serikali ya Muungano wa Tanzania
10.
Kamati
ya Suala la Exclusive Economic Zone (EEZ)
11.Kamati ya Masuala ya Fedha na
Benki Kuu
12.
Kamati ya Rais ya Masuala ya Simu (1996 –1999)
13.
Kamati ya
Baraza la Mapinduzi juu ya matatizo na kero za Muungano na taratibu za
kuyaondoa (2004)
Ukiacha Tume, Kamati na Ripoti hizo, kuanzia mwaka
1985 kulianzishwa utaratibu wa Kamati ya Pamoja ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano na Waziri Kiongozi wa Zanzibar pamoja na Mawaziri wa Serikali zetu
mbili ambao ulitarajiwa uwe ndiyo jukwaa la kuzungumzia matatizo kutoka kwa
washiriki wakuu wa Muungano huu na kuyapatia ufumbuzi unaofaa. Utaratibu huu
uliachwa kwa muda mrefu lakini sasa umerejeshwa upya kufuatia agizo la Rais
Jakaya Kikwete alilolitoa katika mkutano na mawaziri na watendaji wakuu wa
Serikali yake huko Ngurdoto, Arusha mwezi Februari, 2006. Mikutano hiyo sasa
imebadilishwa utaratibu wake na inaongozwa na kusimamiwa na Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano na timu za pande mbili zikiongozwa na Waziri Mkuu kwa
upande wa Serikali ya Muungano na Makamu wa Pili wa Rais kwa upande wa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mikutano, Makongamano, Semina na Warsha vimefanywa
kujadili masuala haya na kupendekeza hatua za kuchukuliwa. Wasomi na wanafunzi
wamefanya tafiti kadhaa na kujipatia shahada na stashahada hadi ngazi ya Ph.D
juu ya Muungano lakini bado matatizo yako pale pale na yanaongezeka kila
kukicha.
Yanayoonekana na kuelezwa kama matatizo, mapungufu,
dosari, kasoro na, kwa msamiati wa sasa, kero yamekuwa ndiyo yale kwa yale.
Nini basi kiini cha haya? Na vipi tutayatatua?
Mimi
nimeamua kutoa changamoto kupitia waraka huu kwa kuitazama historia ya
Muungano, jinsi ulivyoundwa, matatizo yanayoukabili, nafasi na hadhi ya
Zanzibar katika Muungano na nini khatima ya Zanzibar na mustakbali wa Muungano katika
mchakato huu tunaoendelea nao wa kupata Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano.
Nitakayoyaeleza yanaweza yakaonekana ni machungu kwa wakati huu lakini yanaweza
yakawa ndiyo ufumbuzi mujarab kwa siku zijazo.
ASILI
NA SABABU ZA MUUNGANO
Maoni yanayotolewa kuhusu asili na sababu za Muungano
yamekuwa yakitofautiana mno. Wapo wanaouleza Muungano huu kuwa ni wa pekee
katika bara la Afrika, kwani ndiyo pekee ulioweza kudumu katika kutimiza azma
na malengo ya kuleta umoja wa Afrika (Pan-Africanism),[1]
na pia wapo wanauona kuwa ni “jaribio la kusisimua la ukoloni mdogo wa nchi
moja ya Kiafrika kuiteka na kuitawala nchi nyengine ya Kiafrika.”[2]
Kutokana na maelezo na hoja nyingi na zinazokinzana
kuhusu asili na sababu za Muungano, si rahisi kusema moja kwa moja kuwa maelezo
yepi au hoja ipi ni sahihi. Utangulizi (Preamble)
wa Mkataba wa Muungano wa 1964 wenyewe unataja sababu kuu ya kuunganisha nchi
za Zanzibar na Tanganyika kuwa ni “maingiliano ya muda mrefu ya watu wa nchi
mbili hizi na mahusiano yao ya kidugu na kirafiki … na … kuendeleza umoja wa
watu wa Afrika.” Lakini miaka 49 sasa baada ya uzoefu wa Muungano huu,
Wazanzibari wanajiuliza kweli haya yalikuwa ndiyo madhumuni ya Muungano huu?
Wazo la kuungana linaweza kurudishwa nyuma tokea zama
za harakati za ukombozi wa nchi za Afrika. Waasisi na wakuu wa harakati za
kupigania Uhuru waliiona mipaka ya nchi zao iliyowekwa na wakoloni kuwa ni
‘mbinu za kibeberu’ zilizotekelezwa kwa ajili ya manufaa na maslahi yao.
Kutokana na hisia hizo, mazungumzo ya kuanzisha aina fulani ya umoja miongoni
mwa nchi huru za Afrika yalitawala duru za siasa katika miaka ya 5o na 60.
Nadharia mbili zilijichomoza. Ya kwanza, ikishadidiwa
na Kwame Nkrumah wa Ghana, ilikuwa ikitaka kuasisiwa kwa nchi moja tu ya Afrika
nzima iliyoungana ikiwa na Serikali moja kwa bara zima. Nadharia hii ilipingwa
na baadhi ya viongozi, wakiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere wa Tanganyika,
ambao walisisitiza haja ya kuanza na miungano ya maeneo (regional unions) chini
ya mfumo wa Shirikisho badala ya kuwa na mpango wa Serikali moja.[3]
Katika kulifikia lengo hilo, viongozi wa kisiasa wa
nchi tatu za Afrika Mashariki – Kenya, Uganda na Tanganyika – walikuwa
wakifanya mikutano ya mara kwa mara kipindi chote cha kati ya mwaka 1961 na
1963 kuona jinsi gani wanaweza kutimiza ndoto hiyo. Mfumo wa Muungano uliokuwa
ukiandaliwa ulikuwa ni ule wa Shirikisho. Tamko la Pamoja la viongozi hao lilisema:
“Sisi, viongozi wa wananchi na Serikali za nchi za
Afrika Mashariki … tunayakinisha nia zetu kuhusu kuwepo kwa Shirikisho la
Kisiasa la Afrika Mashariki. Mkutano wetu wa leo unasukumwa na hisia za umoja
wa Afrika (Pan-Africanism), na siyo tamaa za maslahi binafsi ya eneo hili. …
Ijapokuwa Zanzibar haikuwakilishwa katika mkutano huu,
tunapaaswa kuweka bayana kwamba nchi hiyo inakaribishwa kushiriki kikamilifu
katika mikutano yetu kwa ajili ya uundwaji wa Shirikisho .”[4]
Lakini Umoja wa Afrika (Pan-Africanism) hauonekani
kuwa ndiyo dhamira pekee au kama ndiyo dhamira halisi ya Muungano. Wengi
wanaamini, na mimi nikiwa mmoja wao, kwamba dhana hiyo ilitumiwa tu kuficha
njama za muda mrefu za Mwalimu Nyerere kutaka kuimeza na kuitawala Zanzibar.
Katika mwaka 1961, wakati Tanganyika inakaribia kupata Uhuru wake, Mwalimu Nyerere
alinukuliwa akisema:
“If I could tow
that island [Zanzibar] out in the middle of the Indian Ocean, I would do it … I
fear it will be a very big headache for Tanganyika.”[5]
Yaani, “Kama ningekuwa na uwezo wa kuvikokota visiwa
vile [Zanzibar] na kuvitupa nje kabisa, katikati ya Bahari ya Hindi, basi
ningefanya hivyo … Nakhofia vitakuja kuiumiza kichwa sana Tanganyika”.
Wakati juhudi za kuanzisha Shirikisho la Afrika
Mashariki zikiwa zinafifia, Mwalimu Nyerere aliona Zanzibar kama fursa ambayo
hakutaka kuipoteza. Katika mazungumzo ya siri kati yake na Rais Abeid Amani
Karume wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, wakakubaliana kuziunganisha nchi mbili
hizi. Hakukuwa na ushirikishwaji wa aina yoyote ule wa wananchi wa nchi hizi
mbili katika maamuzi haya makubwa. Usiri uliogubika hatua hii kubwa
unafichuliwa na si mwengine bali Mwalimu Nyerere mwenyewe pale aliposema:
“[Tanganyika] tulipeleka polisi wetu Zanzibar. Baada ya
kuyashinda matatizo kadhaa tukaungana. Sisi wenyewe kwa khiyari zetu
tulikubaliana kuungana. Karume na mimi tulikutana. Peke yetu wawili tu
tulikutana. Nilipomtajia wazo la Muungano, Karume hakufikiri hata mara mbili.
Pale pale alinitaka kuita mkutano wa waandishi wa habari kutangaza azma yetu.
Nilimshauri asubiri kidogo kwani ilikuwa bado ni mapema mno kuweza kuviarifu
vyombo vya habari.”[6]
Taarifa hizi ziliendelea kubaki kuwa siri hadi tarehe 26
Aprili, 1964 pale Redio ya Tanganyika ilipotangaza kwamba siku hiyo Marais wawili
hao watakutana katika Bunge la Tanganyika kubadilishana Hati za Muungano ambazo
zimeunganisha Zanzibar na Tanganyika kuwa Jamhuri moja. Hivyo inaonekana wazi
kwamba tokea awali Muungano huu ulikosa ridhaa ya watu. Haukuwa Muungano wa
watu, ulioundwa na watu, kwa maslahi ya watu. Bali ulikuwa na umeendelea kuwa
ni Muungano uliosimamishwa kwa ridhaa ya watawala pekee.
Jambo jengine muhimu kulitaja kuhusiana na mazingira ya
uundwaji wa Muungano ni kutokuwepo kwa usawa baina ya wakuu wa nchi mbili hizi
wakati wa kuandaliwa Mkataba wa Muungano. Inajulikana wazi kuwa Rais wa Jamhuri
ya Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere, alipata fursa ya kushauriwa na kusaidiwa
na wataalamu waliobobea wa fani ya sheria waliorithiwa kutoka Serikali ya
Kikoloni ya Kiingereza ambao ni Mwanasheria Mkuu wake, Bw. Roland Brown, na
Mwandishi Mkuu wa Sheria wa Bunge la Tanganyika (Chief Parliamentary Draftsman)
ambaye pia alikuwa Kaimu Mshauri Mkuu wa Sheria wa Serikali (Solicitor
General), Bw. P.R. Nines-Fifoot. Kwa upande mwengine, Rais wa Jamhuri ya Watu
wa Zanzibar, Mheshimiwa Abeid Amani Karume, hakupata fursa kama hiyo.
Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar wa wakati huo, Bw. Wolfgang Dourado, amenukuliwa
hadharani na hata kuandika waraka akieleza jinsi alivyofichwa habari za
maandalizi ya kuundwa Muungano. Mtu mwengine aliyekuwa karibu na Mzee Karume
alikuwa Mzee Aboud Jumbe, na yeye pia ameandika kitabu kueleza kuwa hakuwa
akijua chochote juu ya mipango ya kuunganishwa Zanzibar na Tanganyika hadi
alipoitwa kutoka safarini Pemba na kujulishwa kuwa tayari Mkataba wa Muungano
ulishatiwa saini tarehe 22 Aprili, 1964.
KIINI
CHA MATATIZO YA MUUNGANO
Kama tulivyokwisha kuona kwamba Muungano wa Tanganyika
na Zanzibar uliundwa kupitia Mkataba wa Muungano wa 1964 (Articles of Union).
Mkataba huu, kwa kutumia ushahidi wa picha, ulitiwa saini na Rais wa Jamhuri ya
Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere, na Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar,
Sheikh Abeid Amani Karume, kwa niaba ya nchi zao mbili katika Ikulu ya
Zanzibar, tarehe 22 Aprili, 1964.
Mkataba wa Muungano wa 1964 (Articles of Union between
the Republic of Tanganyika and the People’s Republic of Zanzibar) ni Mkataba
wa Kimataifa (an international treaty) na ndiyo maana kwa kuzingatia
matakwa ya sheria za kiingereza (English Common Law System) zilizokuwa
zikifuatwa na Zanzibar na Tanganyika wakati huo na hadi leo uliweka sharti
katika kifungu cha (viii) kwamba unapaswa kuthibitishwa na Bunge la Tanganyika
na Baraza la Mapinduzi la Jamhuri ya Watu wa Zanzibar likishirikiana na Baraza
lake la Mawaziri ili kuupa nguvu za kisheria ndani ya nchi mbili hizo.
Hoja ya kwanza inayojitokeza hapa na ambayo imeshindwa
kupatiwa majibu hadi leo ni kushindwa kupatikana kwa nakala halisi (original
copy) ya Mkataba huo ikiwa na saini za Rais Nyerere wa Jamhuri ya Tanganyika na
Rais Karume wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Hoja hii imeibuliwa ndani ya Bunge
la Jamhuri ya Muungano na pia katika Mahkama Kuu ya Zanzibar ambako Serikali
zote mbili, Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, zimeshindwa kutoa nakala hiyo licha ya kuahidi kufanya hivyo. Nusura
pekee iliyobaki ni kutegemea nakala halisi (iwapo ipo) inayoelezwa kwamba
ilikabidhiwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kumbukumbu za
Umoja huo kujiridhisha kwamba nchi mbili hizi zimeungana. Kuonekanwa kwa nakala
halisi ya Mkataba huo ni muhimu sana katika kujiridhisha uhalisia wa kile
kilichokubaliwa baina ya nchi zetu mbili.
Hoja ya pili ni ile inayohusu utekelezwaji wa matakwa
ya uthibitishaji (the want of ratification) wa Mkataba huo kwa upande wa
Zanzibar. Upo ushahidi wa kutosha kwamba Bunge la Tanganyika lilikutana na
kuuridhia Mkataba huo tarehe 25 Aprili, 1964. Kwa upande mwengine, hakuna
ushahidi wowote kwamba Baraza la Mapinduzi likishirikiana na Baraza la Mawaziri
la Zanzibar lilikaa kuuridhia Mkataba huo kwa kupitisha Sheria ya Kuthibitisha
(Ratification Decree) kama ilivyotakiwa na Mkataba wenyewe. Kwa hakika ushahidi
ulioibuliwa na Prof. Issa Shivji katika kitabu chake cha karibuni kabisa, Pan-Africanism or Pragmatism? Lesssons of
Tanganyika-Zanzibar Union umeweka wazi pasina chembe ya wasiwasi kwamba
Mkataba huo haujaridhiwa na upande wa Zanzibar hadi hii leo.
Ukiachilia mbali hoja hizo, na kwa msingi wa hoja
tukichukulia kwamba Mkataba huo ni halali, bado ukitazama kwa jicho la sheria, utaona
kiini cha matatizo ya Muungano kinatokana na tafsiri ya Mkataba wa Muungano
(Articles of Union) wa 1964. Suala kubwa lililoumiza na linaloendelea kuumiza
vichwa vya wengi na hivyo kuendelea kuulizwa ni mfumo gani wa Muungano
ulikusudiwa kuwekwa na Mkataba huu? Ni muungano wa moja kwa moja (unitary) au
wa shirikisho (federal)?
Mfumo uliopo sasa ambao ulianza kutekelezwa 1964 ni
ule wa serikali mbili – ile ya Jamhuri ya Muungano na ile ya Zanzibar.
Tanganyika haikuwekewa serikali yake tofauti; madaraka yake kwa yale mambo
yasiyo ya Muungano yalielezwa kwamba yatasimamiwa na kuendeshwa na Serikali
hiyo hiyo ya Jamhuri ya Muungano. Hata hivyo, uhalali wa kisheria wa muundo huu
umeendelea kuhojiwa na hata kupingwa kwamba hauwakilishi ipasavyo makusudio
yaliyomo katika Mkataba ulioanzisha Muungano wenyewe.
Mkataba wa Muungano wenyewe hauelezi bayana aina au
mfumo wa muungano inaouanzisha lakini uko wazi kuhusiana na mgawanyo wa
madaraka (distribution of power)
inaouweka na idadi ya mamlaka (number of
jurisdictions) zitakazokuwepo. Ibara ya (iii) (a) ya Mkataba huo inaanzisha
‘Baraza la Kutunga Sheria na Mamlaka ya Utendaji’ (Legislature and Executive) ndani ya na kwa ajili ya Zanzibar ikiwa
na mamlaka kamili (exclusive authority)
kuhusiana na mambo yote yasiyo mambo ya Muungano kwa Zanzibar. Kwa upande
mwengine, Ibara ya (iv) ya Mkataba huo inaanzisha ‘Bunge na Mamlaka ya Utendaji’
(Parliament and Executive) ya Jamhuri
ya Muungano ikiwa na mamlaka kamili katika eneo lote la Jamhuri ya Muungano
kuhusiana na mambo ya Muungano na, pia, ikiwa na mamlaka kamili ndani ya,
na kwa ajili ya Tanganyika kuhusiana na mambo yote yasiyo mambo ya Muungano kwa
Tanganyika. Kwa hivyo, katika sehemu ya pili, mamlaka mbili tofauti
zimechanganywa pamoja.
Mjadala mkubwa na mkali umekuja kuhusiana na tafsiri
ya Ibara hiyo ya (iv) na kule kuchanganya kwake mamlaka mbili hizo.
Haya si masuala ya kisheria tu kama ambavyo baadhi
yetu wanataka tuamini (ingawa nayo ni muhimu mno kama ilivyodhihirika hivi karibuni),
bali pia ni masuala ya kisiasa kwa vile yanahusisha uwezo wa maamuzi, madaraka
na mamlaka, na zaidi mchango wa gharama za uendeshaji na mgawanyo wa rasilimali
na mapato kati ya wahusika wakuu. Mambo haya, katika uzoefu wa nchi za wenzetu,
ndiyo yaliyopelekea kuvunjika kwa miungano yao kwani huzaa kutiliana shaka na
kutokuaminiana. Kwa vile yanachukua sura ya kisiasa (kutokana na sababu
nilizozitaja), haya hayana chama wala itikadi kama nitakavyoonyesha huko mbele.
Kama alivyowahi kusema Prof. Issa Shivji:
“Ultimately, the
question of the Union is primarily a political question and no amount of
rhetoric about blood and cultural ties will matter when it comes to
realpolitik.”[7]
Yaani, “Mwisho wa yote, suala la Muungano linabakia
kimsingi kuwa ni suala la kisiasa, na inapofikia kwenye siasa hasa, hotuba na
kauli kali za jazba kuhusiana na mahusiano ya damu na ya kidugu, zote hazitafaa
kitu.”
Kwa hakika, kinyume na inavyojaribiwa kuonyeshwa na
wengi kwamba Tanganyika imepoteza kila kitu katika muundo huu wakati Zanzibar
imekabidhi sehemu tu ya madaraka yake, muundo wa Serikali mbili umepelekea
wengi kuamini kwamba kilichofanyika ni kiini macho tu kwani ni Zanzibar
iliyokabidhi sehemu muhimu ya mamlaka yake (mahusiano ya nchi za nje, ulinzi na
usalama, uraia, kodi na ushuru, sarafu, nguvu kuu za kuendeshea uchumi na
mengineyo) kwa Tanganyika na kisha Tanganyika ikajigeuza jina na kujiita
Jamhuri ya Muungano. Na haya si maoni ya ngumbaru
(kwa lugha ya Mwalimu Julius Nyerere) bali ni maoni ya watu wazito wakiwemo
aliyekuwa Spika wa Bunge na baadaye akawa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Mheshimiwa Pius
Msekwa ambaye alisema kwa jinsi mambo yalivyofanyika, Zanzibar inaonekana kama
vile ni ‘invited guest’ (mgeni
aliyealikwa) katika Muungano.[8]
Naye msomi mashuhuri ulimwenguni, Prof. Ali Mazrui alisema baada ya Muungano
Zanzibar imepoteza kila kitu muhimu wakati Tanganyika imebadilika jina tu na
kuwa Tanzania huku ikiwa na mamlaka zaidi lakini ikibaki na Rais wake, nembo
yake ya Taifa, wimbo wake wa Taifa na hata kiti chake katika Umoja wa Mataifa.[9]
MKATABA
WA MUUNGANO HAUJAFUTA SERIKALI YA TANGANYIKA
Katika
makubaliano ya kimataifa yaliyounda Muungano, ambayo hata hivyo katika muda
wote wa uhai wa Muungano yamekuwa hayafuatwi, hakuna kifungu hata kimoja
kilichotoa au kuagiza kwamba Serikali ya Tanganyika ifutwe kwa mujibu wa
makubaliano hayo. Serikali ya Tanganyika, kama ilivyo ile ya Zanzibar,
imelindwa na kifungu cha (v) kinachosomeka kwamba: “The existing laws of Tanganyika
and of Zanzibar shall remain in force in their respective territories…”.
Kinachosemwa hapa ni kwamba “Sheria zilizopo za Tanganyika na za Zanzibar
zitaendelea kufanya kazi na kuwa na nguvu katika maeneo yao.”
Wataalamu
wa katiba na sheria wanafahamu kwamba katiba ndio sheria mama ya sheria zote za
nchi. Hivyo Katiba ya Tanganyika imelindwa na inapaswa kuwepo na Serikali yake
iwepo, pamoja na viongozi wake kuwepo na kusimamia mambo yasiyo ya Muungano.
Katiba na sheria za Tanganyika ndizo zilizotakiwa zitumike katika eneo la
Tanganyika kwa yale mambo yaliyokuwa hayamo kwenye Muungano kama ambavyo Katiba
(au kabla ya hapo Dikrii za Kikatiba – Constitutional
Decrees) na sheria za Zanzibar zinavyotumika katika eneo la Zanzibar kwa
yale mambo ambayo si ya Muungano. Hiyo ndio tafsiri ya ‘maeneo yao’.
Wazanzibari
wanafahamu kwamba Katiba na Serikali ya Tanganyika vimefutwa kwa makusudi na
Bunge la Tanganyika ili kujipa nafasi kuitumia Serikali ya Muungano, kama
kwamba ndio Serikali ya Tanganyika. Lengo ni hatimaye kuiuwa Serikali ya
Zanzibar na kufanya Tanganyika mpya ikiwa na jina jipya la Tanzania lenye
mipaka mipya, yaani kuwa nchi moja yenye Serikali
Moja.
Hiyo
ndio ghilba iliyofanywa na viongozi wa Tanganyika mara baada ya kuwekwa saini
makubaliano. Kwa kusaidia kufichuwa ukweli wa hadaa hii, ni vyema ikaangaliwa
Sheria Na. 22 ya mwaka 1964 inayoitwa “Union
of Tanganyika and Zanzibar Act, 1964.”
Sheria
hii ilipitishwa na Bunge la Tanganyika Aprili 25, 1964, siku moja kabla
Muungano kuanza kufanya kazi. Ilikusudiwa kuthibitisha kukubalika Muungano huo
wa Tanganyika na Zanzibar upande wa Tanganyika (ratification). Kifungu cha (viii) cha Makubaliano ya Muungano kinaagiza ifanyike hivyo kwa pande
zote mbili za Muungano.
Inasikitisha
kusoma katika kifungu Na. 2 cha sheria hiyo kwamba:
“existing law” means the written and unwritten law as it exists immediately before Union
Day … but does not include the Constitution of Tanganyika insofar as it
provides for the Government of the Republic of Tanganyika or any declaration or
law, or any provision thereof, which expires with effect from commencement of
the Interim Constitution”.
(“Sheria iliyopo maana yake ni sheria iliyoandikwa na
isiyoandikwa kama ilivyo kabla tu ya siku ya Muungano… lakini haijumuishi
Katiba ya Tanganyika kwa mintaraf ya kuiweka kwake Serikali ya Jamhuri ya
Tanganyika au tamko au sheria, au kifungu chochote ambacho kinafutika kwa
kuanza kufanya kazi Katiba ya Muda (ya Muungano)).”
Kwa
hivyo, wakati Bunge la Tanganyika linapitisha sheria ya kuridhia (ratify) kuwepo kwa Muungano kwa upande
wa Tanganyika, sheria hiyo ilianza kupinga vifungu vya makubaliano hayo. Mfano
mwengine ni kifungu Na. 7 cha sheria hiyo kinachosema:
“On the commencement of
the Interim Constitution of the United Republic, the Constitution of Tanganyika
shall cease to have effect for the government of Tanganyika as a separate part
of the United Republic”.
(“Itapoanza kufanya kazi Katiba ya Muda ya Jamhuri ya
Muungano, Katiba ya Tanganyika itasita kuwa na nguvu kwa ajili ya Serikali ya
Tanganyika kama sehemu mbali ya Jamhuri ya Muungano.”)
Kwa
maneno mengine, sheria ambazo zilitakiwa zitumike kwa Tanganyika kwa mambo
ambayo si ya Muungano zilipewa maana mpya kwamba eti zisijumuishe Katiba ya
Tanganyika.
Jambo
moja lililo wazi, pamoja na hatua hii ya kuifuta Katiba ya Tanganyika, ni
kwamba kule kuendelea kutambua kuwepo kwa sheria nyengine za Tanganyika bado
kunamaanisha kuwepo kwa mamlaka ya Tanganyika ambako sheria hizo kwa mambo
yote yasiyo mambo ya Muungano ziliendelea na zinaendelea kutumika hadi leo.
Zaidi,
inapaswa ifahamike kwamba kufuta Katiba ya Tanganyika kulikofanywa na vifungu
vya sheria hii hakukubadilisha makubaliano yaliyokwishatiwa saini kati ya
Serikali mbili zilizounda Muungano, yaliyosema kwamba sheria za nchi mbili hizi
zitaendelea kutumika katika maeneo yao.
Bunge la Tanganyika, na hata hili la Muungano, halikuwa na mamlaka kutafsiri
vifungu vya Mkataba wa Muungano ambao ni mkataba wa kimataifa.
Utaratibu
wa kisheria ni kwamba kama Mkataba ulitakiwa kutafsiriwa basi walioandika
rasimu ya mkataba huo ndio walipaswa kutoa tafsiri ya vifungu vyake, tafsiri
ambayo ingepaswa iwe sehemu ya Mkataba huo. Na wala makubaliano yale hayakufuta
wadhifa wa Rais wa Tanganyika. Si hivyo tu, bali pia Katiba ya Muungano ambayo ilitakiwa
iwe ya muda tu kwa mwaka mmoja (interim)
ilikuwa ni ile ya Tanganyika iliyofanyiwa marekebisho kwa ajili ya kutumika kwa
Serikali ya Muungano.
Haikuruhusiwa
kutumika kuiongoza Tanganyika kwa sababu Tanganyika ilikuwa na Katiba yake na
Rais wake. Mwalimu Nyerere alikuwa na vyeo viwili, Rais wa Jamhuri ya Muungano
kwa mujibu wa Makubaliano na Katiba ya Muungano na Rais wa Tanganyika kwa
mujibu wa Katiba ya Tanganyika, kama alivyokuwa Mzee Karume ambaye alikuwa
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa Makubaliano na Katiba ya
Muungano na akaendelea kubaki kuwa Rais wa Zanzibar kwa mujibu wa Dikirii za
Katiba ya Zanzibar (Constitutional
Decrees).
Hivyo
ndivyo makubaliano yalivyokuwa na ndivyo yalivyopaswa yawe hadi hii leo.
Waliobadilika ni watu tu. Kufanya vyenginevyo ni kinyume na makubaliano yale na
ndio sababu ya migogoro ya Muungano. Yaliyofanyika ni ujanja uliokuwa hauna nia
njema kwa Zanzibar kama alivyosema Prof. Issa Shivji, mtaalamu wa Katiba wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Hatua
zote ya kuepusha Serikali ya Tanganyika kuwepo zilifanywa kwa makusudi kabisa,
ili itumike Serikali ya Muungano kama ndio Tanganyika. Katika Sheria ile Na. 22
ya 1964, Rais wa Tanganyika amejipa madaraka ya kutunga na kutoa maagizo
yanayohusu Muungano kwa kutumia amri (Decrees)
za Sheria ya Tanganyika.
Siku
ile ile ilipopitishwa Sheria Na. 22 ya 1964 zilipitishwa pia Decrees mbili zilizotokana na vifungu
Na. 6 (3), cha 8 na cha 5 cha sheria hiyo Na. 22 ya 1964, yaani The Provisional Transitional Decree 1964,
na ile ya Interim Constitution Decree
1964 ambazo zilifanya mabadiliko makubwa ya Muungano nje ya yale
makubaliano yaliyokuwemo katika Mkataba wa Muungano. Sheria zile zote hazikuwa
halali maana ni Decrees zilizopitishwa
na Bunge la Tanganyika zilizotokana na Sheria Na. 22 ya 1964 ya Tanganyika
kabla hata ya Muungano wenyewe kuanza kufanya kazi tarehe 26 Aprili, 1964.
Miongoni
mwa mambo yaliyodhihirisha kuwa hakukuwa na nia njema katika Muungano huu tokea
awali ni pale wafanyakazi wa Serikali ya Tanganyika wote walipopandishwa vyeo kwa
pamoja na kuwa wafanyakazi wa Muungano kama kifungu cha 3 (1) cha Provisional Transitional Decree
kinavyosema:
“Every person who holds
office in the service of the Republic of Tanganyika immediately before the
Union Day, shall on Union Day be deemed to have been elected, appointed or
otherwise selected to the corresponding office in the service of the United
Republic.”
Yaani
kila mfanyakazi aliyekuwa wa Serikali ya Tanganyika mara kabla ya siku ya
Muungano kufumba na kufumbuwa anakuwa mara moja mfanyakazi wa Serikali ya
Muungano kuanzia siku ya Muungano. Huu tuuiteje kama si ujambazi wa kikatiba (constitutional banditry)?
Vivyo
hivyo, kifungu cha 6 (i) cha Decree
kinasema mara tu baada ya kuanza Muungano, Mahkama ya Tanganyika na Majaji wake
wote nao watakuwa ndio Mahkama na Majaji wa Jamhuri ya Muungano kinyume na
Makubaliano ya Muungano. Mpaka leo Katiba zote mbili hazitambuwi Mahkama
(ukiondoa Mahkama ya Rufaa) kama ni suala la Muungano. Nembo ya Tanganyika
inatumika kama nembo ya Serikali ya Muungano na Idara ya Mwanasheria Mkuu wa
Tanganyika inachukuliwa kama Idara ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Muungano.
Haya yote hayamo na ni kinyume na Makubaliano ya 1964.
Yote haya na kile kifungu cha 7 cha Sheria Na. 22 ya 1964 kinachofuta kuwepo
kwa Serikali ya Tanganyika hayakubadilisha na wala hayana mahusiano na
Makubaliano ya Muungano ya 1964. Yote haya yalifanywa na Bunge la Tanganyika
kwa maslahi ya Tanganyika nje ya Mkataba wa Muungano.
Aliyekuwa Spika wa Bunge na baadaye akawa Makamu
Mwenyekiti wa CCM, Mheshimiwa Pius Msekwa, analifahamu vyema suala hili. Katika
waraka wake alioutoa kwenye Semina kuhusu Muungano hapo Hoteli ya Mkonge, Tanga
tarehe 25—27 Februari 1994 anasema:
“The Transitional Decree, 1964
published on 01/05/64, transferred persons who were holding office in the
public service of the Republic of Tanganyika to the corresponding office in the
public service of the United Republic of Tanzania. By the same decree the High
Court of Tanganyika also became the High Court of United Republic of Tanzania
and the public seal of Tanganyika became public seal of the United Republic.”
Athari za hatua hizi kwa Zanzibar ziko wazi.
Tanganyika imejigeuza Tanzania na imechukua mamlaka ya mambo muhimu ya Zanzibar
huku ikijipa hadhi ya kuwa juu ya Serikali ya Zanzibar kinyume na Mkataba wa
Muungano.
Hii ndiyo siri ya viongozi wa Tanganyika wanaoongoza Serikali
ya Jamhuri ya Muungano kung’ang’ania mfumo wa Serikali mbili na kukataa kata
kata mabadiliko yoyote ya mfumo huo kwani Tanganyika inanufaika nao kwa kuwa
yenyewe ndiyo imekuwa ‘Muungano’. Kukubali muundo wa Serikali tatu ni kuzifanya
Tanganyika na Zanzibar ziwe na hadhi na fursa sawa katika Muungano, jambo
ambalo Tanganyika hailitaki maana kulikubali ni kukubali kupoteza fursa zote
inazozipata hivi sasa kwa kujikweza kwake na kujifanya kuwa ndiyo ‘Muungano’.
Ushahidi wa wazi wa hoja yangu hii ni kwamba mtu
anapoangalia taasisi zote za Muungano zilizoundwa chini ya Katiba au sheria za
Muungano ambazo zinazikutanisha Serikali mbili zilizopo sasa, ataona kuwa
wajumbe wanaowakilisha upande wa Serikali ya Muungano wote ni kutoka
Tanganyika. Hoja inayojitokeza ni kwamba Serikali ya Muungano ni ya shirika
ambapo Zanzibar ni sehemu ya ushirika huo, kwa nini basi wajumbe wanaowakilisha
Serikali hiyo ya Muungano watoke upande wa Tanganyika peke yake? Jawabu ni
rahisi. Serikali ya Muungano kwa hakika ni Serikali ya Tanganyika iliyojivika
joho la Muungano.
Rais Jakaya Kikwete amekaririwa hadharani akisema
matatizo ya Muungano hayatokani na muundo bali yanasababishwa na viongozi. Hoja,
maelezo na mifano niliyoitoa hapo juu inatosha kumuonyesha Rais kwamba kauli
yake si sahihi. Vyote viwili – muundo na pia kukosekana kwa nia njema upande wa
viongozi – ni sababu za kuwepo kwa matatizo yasiyokwisha ya Muungano.
UVUNJWAJI
WA MKATABA WA MUUNGANO
Mbali na suala la muundo wa Muungano, maeneo mengine
mengi yanayogusa msingi wa Mkataba wa Muungano yaliendelea kuvunjwa na
Tanganyika ikivaa joho la Serikali ya Muungano.
Kifungu cha (iv) cha Mkataba wa Muungano kiliorodhesha
mambo 11 tu ambayo ndiyo yaliyokubaliwa na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na
Jamhuri ya Tanganyika kuwa mambo ya Muungano. Hata hivyo, kipindi cha miaka 49
ya Muungano kimeshuhudia mambo hayo yakiongezwa isivyo halali kwa kutumia
chombo kisicho na mamlaka ya kufanya hivyo yaani Bunge la Muungano na sasa
kufikia 22 lakini ukiyanyumbua yanafikia 37. Mfano unakuta kifungu kimoja cha
11 kinayaweka pamoja mambo manne ambayo ni Bandari, Usafiri wa Anga, Posta na
Simu. Kwa lugha ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman,
anasema ni makontena 22 yenye mambo 37 ya Muungano. Ikumbukwe kwamba kila hatua
ya kuongeza mambo ya Muungano maana yake ni kuchukua mamlaka ya Zanzibar na
kuyahaulisha kwa Serikali ya Muungano ambayo kama tulivyokwisha onyesha kwa
hakika hasa ni Serikali ya Tanganyika iliyojivika joho la Muungano.
Mambo
hayo yaliyoongezwa juu ya Makubaliano ya Muungano ya asili, yaani, yale kumi na
moja (11) ni haya, kama yanavyoelezwa katika Nyongeza ya Kwanza ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano:-
(xii)
Mambo yote
yanayohusika na Sarafu na Fedha kwa ajili ya malipo yote halali (pamoja na
noti); mabenki; fedha za kigeni na usimamizi juu ya mambo yanayohusika na fedha
za kigeni.
(xiii)
Leseni za Viwanda na Takwimu.
(xiv)
Elimu ya Juu.
(xv)
Maliasili ya Mafuta, pamoja na mafuta yasiyochujwa ya motokaa na mafuta
aina ya petroli na aina nyinginezo za mafuta au bidhaa za mafuta, na gesi
asilia.
(xvi)
Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania na mambo yanayohusika na kazi za
Baraza hilo.
(xvii)
Usafiri na Usafirishaji wa Anga.
(xviii)
Utafiti.
(xix)
Utabiri wa Hali ya Hewa.
(xx)
Takwimu.
(xxi)
Mahkama ya Rufaa ya Jamhuri ya Muungano.
(xxii) Uandikishaji wa vyama vya siasa na mambo mengine yanayohusiana
nayo.
Ukiondoa
mambo hayo, yapo pia mambo mengine ya ziada ambayo yameingizwa katika Muungano
kwa Bunge tu kutunga sheria na kutangaza kwamba zitatumika hadi Zanzibar. Mfano
wa masuala kama hayo ni Uvuvi wa Bahari Kuu na Tume ya Utawala Bora na Haki za
Bianadamu. Yapo baadhi yake kwa mfano Usafiri wa Baharini ambapo Zanzibar
ilikataa kutekeleza sheria iliyopitishwa na Bunge (The Merchant Shipping Act) na hatimaye ikatunga sheria yake yenyewe
kuhusiana na suala hilo (The Maritime
Transport Act).
Kifungu cha (vii) cha Mkataba huo kinataka Rais wa
Jamhuri ya Muungano kwa mashauriano na makubaliano na Makamu wa Rais ambaye pia
ni Rais wa Zanzibar kuunda Tume ya Katiba kwa lengo la kutayarisha rasimu ya
Katiba ya Kudumu ya Muungano na baadaye kuifikisha rasimu hiyo mbele ya Bunge
la Katiba (Constituent Assembly) litakalokuwa na wajumbe kwa idadi watakayokubaliana
kutoka Zanzibar na Tanganyika. Hatua hii muhimu sana kikatiba ilitakiwa
itekelezwe ndani ya kipindi cha mwaka mmoja tokea tarehe ya Muungano. Hadi ilipokuja
hatua hii ya sasa ya kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba, hakuna Tume ya Katiba
iliyoundwa wala Bunge la Katiba lililoundwa na kuitishwa kwa madhumuni ya
kupitisha Katiba ya Kudumu ya Muungano. Kilichofanyika ni kuwa mwezi mmoja
kabla ya kumalizika mwaka mmoja uliotakiwa, Bunge la Muungano lilitakiwa na
Mwalimu Julius Nyerere kupitisha sheria ya kuahirisha kwa muda usiojulikana
tarehe ya kutekelezwa kwa hatua hii.
Lakini mbali na dhoruba hizo dhidi ya Mkataba wa
Muungano, rungu kubwa zaidi ambalo ndilo lililotumika kuimaliza Zanzibar
lilikuwa ni kule kuunganishwa kwa vyama vya TANU na ASP na kuzaliwa CCM huku chama
hicho kipya kikijipa madaraka juu ya vyombo vyengine vyote vya maamuzi katika
nchi ikiwemo Serikali na Bunge na Baraza la Wawakilishi. Chini ya dhana ya
Chama kushika hatamu (Party Supremacy)
iliyoasisiwa na Mwalimu Nyerere kwa lengo la kujilimbikizia madaraka yeye na
Chama alichokuwa akikiongoza kama milki yake binafsi, CCM iliweza kutoa maagizo
na maamuru mazito bila ya kujali madaraka ya Serikali ya Zanzibar yaliyotolewa
kupitia Mkataba wa Muungano na hivyo kujinyakulia uwezo wote wa kuitawala Zanzibar
ipendavyo huku viongozi wa Zanzibar wanaohoji wakituhumiwa kwamba wanapinga
nidhamu ya Chama.
MATATIZO
YATOKANAYO NA KIINI CHA TATIZO
Kiini cha tatizo la msingi la Muungano ambalo kwa
mtazamo wangu ni muundo wake unaotokana na tafsiri potofu ya Mkataba wa
Muungano (Articles of Union) ndicho
kimepelekea kujitokeza kwa matatizo mengine katika miaka 49 hii na ambayo
yanaongezeka kila uchao.
Mtu anapoangalia matatizo au hizi zinazoitwa kero
atagundua kuwa karibu yote yanatokana ama na mshirika mmoja (mara nyingi
Zanzibar) kutokuuamini au kuutilia shaka upande mwengine, au mshirika wa pili
(mara nyingi Tanganyika ikivaa joho la Muungano) kuamini kwamba ina haki ya
moja kwa moja kuamua na kutekeleza mambo fulani bila ya kulazimika kupata
ridhaa ya upande wa pili ambao inahisi kama imeubeba tu. Ukiangalia kwa undani
utagundua kuwa tatizo linarudi kwenye muundo. Zanzibar haifahamu mamlaka ya
Muungano katika Serikali ya Muungano yanaishia wapi ambapo mamlaka kwa mambo
yasiyo ya Muungano kwa ajili ya Tanganyika yanaanza. Tanganyika nayo kwa kuwemo
kwake katika Serikali ya Muungano kunaifanya ishindwe kufahamu ni vipi na wapi
Zanzibar inapata mamlaka ya kuhoji mambo ambayo yameshatamkwa kwamba ni ya
Muungano hata kama hayakuwemo katika Mkataba wa asili wa Muungano. Hali hii
inaonekana katika kila kile kinachoitwa “kero” za Muungano.
Mifano inaweza kutolewa kwa takriban mambo yote,
lakini kwa madhumuni ya waraka huu tuchukue mifano ya mambo matatu yafuatayo
yanayozusha malalamiko:
1.
Umilikaji
wa Mafuta na Gesi asilia.
2.
Uchangiaji
katika gharama za Muungano na mgawanyo wa mapato yanayotokana na Muungano.
3.
Uwakilishi
wa Zanzibar katika Bunge la Muungano.
Umilikaji
wa Mafuta na Gesi asilia
Kwanza, kuingizwa kwake katika orodha ya mambo ya
Muungano (kama ilivyo kwa mambo mengi yaliyoongezwa baadaye) hakukufuata
taratibu za Serikali ya Muungano (ambayo pia ni Serikali ya Tanganyika kwa
mambo yasiyo ya Muungano) kuishauri na kupata ridhaa ya Zanzibar. Pili,
Zanzibar inataka kujua ikiwa mafuta yanapaswa kuwa suala la Muungano na hivyo
mapato yatakayopatikana yanufaishe pande zote mbili, kwa nini madini mengine
yanayopatikana Bara kama vile dhahabu, almasi au tanzanite hayakufanywa pia kuwa
ya Muungano na hivyo kunufaisha pande mbili pia? Kwa
hivi sasa, ambapo si mambo ya Muungano, mapato yake yanaponufaisha Tanganyika
peke yake, yanaingia katika mfuko (account)
upi wa matumizi? Tatu, kwa miaka isiyopungua tisa (9) sasa, Tanganyika imekuwa
ikivuna gesi asilia huko Songosongo na Mnazi Bay na kwa miaka miwili sasa
imekuwa ikivuna gesi asilia kwa wingi katika maeneo ya bahari iliyopakana na
Mtwara lakini pamoja na kutajwa suala hilo kuwa la Muungano, Zanzibar
haijafaidika na chochote kutokana na mapato yake. Nne, ikiwa mapato
yatakayopatikana kutokana na mafuta na gesi asilia yataingia katika mfuko wa
Muungano, kuna uhakika gani wa kutumika kwa shughuli za Muungano tu wakati
hakuna mifuko tofauti ya fedha kwa shughuli za Muungano na zile za Tanganyika
zisizo za Muungano?
Uchangiaji
katika gharama za Muungano na mgawanyo wa mapato yanayotokana na Muungano
Je, mtu anaposema Zanzibar haichangii gharama za
uendeshaji wa vyombo na taasisi za Muungano kwa sababu tu Serikali ya Zanzibar
haitoi fungu la fedha na kuliingiza katika Serikali ya Muungano, Tanganyika
ambayo hata Serikali haina inachangia vipi na kiasi gani? Ikiwa mchango wake
unatolewa na Serikali ya Muungano, kwani hii siyo serikali ya shirika ambapo
Zanzibar ni mbia? Vipi basi Zanzibar itakiwe ichangie mara mbili kwa kutumia
hadhi mbili tofauti? Na ikichangia (iwapo itachangia), ina uhakika upi kwamba
itakachotoa hakitatumiwa na Serikali ya Muungano kwa shughuli za Tanganyika
zisizo za Muungano ikitumia mamlaka yake kwa madhumuni hayo? Vivyo hivyo kwa
mapato yatokanayo na vyombo na taasisi za Muungano, tunajua Zanzibar inapata
mgao wake na kiasi chake kimewekwa wazi (ingawa kwa sasa ni mapato ya TRA
yanayokusanywa Zanzibar; na pia gawio kutoka Benki Kuu (BOT) ambalo nalo
kiwango chake hakikubaliki kwa Wazanzibari). Zipo mamlaka nyengine za
Kimuungano zinazoingiza mapato na ambazo Zanzibar haipewi chochote kutoka kwake
zikiwemo TCRA, TCAA, TPC, TTCL, na TPDC kwa kutaja chache. Masuala zaidi yanakuja:
Yale mapato yanayobaki katika Serikali ya Muungano, kuna kipi cha kuonyesha
mpaka wa matumizi yake kwa Muungano na kwa shughuli za Tanganyika zisizo za
Muungano? Uadilifu na uwajibikaji wa matumizi yatokanayo na mgao huu wa mapato
utaonekana vipi?
Ukweli hasa kuhusiana na suala la uchangiaji katika
gharama za Muungano na mgawanyo wa mapato yanayotokana na Muungano ulipatikana
kufuatia kuundwa kwa Tume ya Pamoja ya Fedha (Joint Finance Commission) ambayo iliajiri wataalamu (consultants) kutoka taasisi
inayoheshimika duniani ya PriceWaterhouseCoopers kuangalia suala hilo. Ripoti
ya Wataalamu ilitolewa Agosti 2006 na kufanyiwa kazi na Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar lakini hadi leo imekaliwa na Serikali ya Muungano bila shaka baada
ya kutoa picha isiyopendeza kwa upande wa Tanganyika kuhusiana na hali halisi
ya vipi uendeshaji wa Muungano ulivyo. Wataalamu wa Kampuni
ya PriceWaterhouseCoopers walifanya
uchambuzi halisi wa mambo yepi ni ya Muungano na yepi ni ya Tanganyika na yepi
ni ya Zanzibar na gharama za uendeshaji wa kila moja. Baada ya orodha
kupatikana, watafiti wakatafuta matumizi halisi ya bajeti ya vifungu hivyo kwa
muda wa kiasi cha miaka 10 iliyopita. Watafiti hao walikwenda mbali zaidi ya
hapo na kukusanya mapato yote kwa kila kifungu cha mambo ya Muungano halisi.
Mwishowe, wakalinganisha iwapo mapato yanakidhi matumizi au yana nakisi
(upungufu)?
Kilichojitokeza
ni kwamba kwa mwaka wa fedha 2003/2004 pekee,
matumizi halisi kwa vifungu vya Muungano yalikuwa Shs. 537,258.4 bilioni
ambayo ni aslimia 20 tu ya bajeti yote ya Serikali ya Muungano kwa mwaka huo. Mapato
halisi ya vyanzo vya mapato vinavyotokana na mambo ya Muungano kwa mwaka huo
yalikuwa ni Shs. 1,030,826.1 bilioni. Tofauti ya vifungu hivyo vimetoa ziada ya
ya Shs. 493,567.7 bilioni kwa mwaka huo. Ziada hii haiingizi mapato
yanayotokana na misaada kutoka nje au mikopo. Ziada hii hutumika kwa shughuli
za Tanganyika zisizo za Muungano.
Ukweli
huu unaonyesha hata kama kungekuwa na Serikali tatu kusingekuwa na haja yoyote
kwa Serikali ya Zanzibar na ile ya Tanganyika kulipia fedha za ziada kama
wahusika watatunza na kuweka kumbukumbu sahihi za mapato na matumizi ya mambo
ya Muungano halisi badala ya yale ya Tanganyika kuchanganywa na ya
Muungano. Mambo yasiyokuwa ya Muungano
ya Tanganyika yalipotengwa nje ya yale ya Muungano, gharama za mambo ya
Muungano zimejidhihirisha wazi bila ya kujificha na kuonesha kwamba zinaweza
kulipiwa kupitia mapato ya mambo ya Muungano pekee na ziada kubaki. Lakini hili
limekuwa rahisi kwa kukubali ukweli kwamba kuna mafungu matatu ya mapato na
matumizi katika Serikali zetu mbili. Mafungu hayo ni la SMZ kwa mambo yake
yasiyo mambo ya Muungano, la Serikali ya Muungano kwa mambo ya Muungano, na la
Serikali ya Muungano inayofanya kazi za Tanganyika kwa mambo yasiyokuwa ya
Muungano.
Uwakilishi
wa Zanzibar katika Bunge la Muungano
Wananchi wengi wa Tanganyika wanahoji vipi Zanzibar iliyo
ndogo na ambayo ina watu milioni 1.3 inawakilishwa na wabunge wa kuchaguliwa 50
wakati Dar es Salaam yenye wananchi wengi zaidi ina wabunge wa kuchaguliwa 7
tu? Wabunge hawa wanashiriki mijadala yote ya Bunge
ikiwemo ya mambo yasiyo ya Muungano (ambayo kwa usahihi yatakuwa ni mamlaka ya
Tanganyika kwa mambo yasiyo ya Muungano yanayosimamiwa na Serikali ya
Muungano). Wanapata wapi uhalali wa kufanya hivyo wakati Wazanzibari
hawapangiwi shughuli hizo (kwa mfano elimu, afya, kilimo, maji, umeme, habari,
michezo, biashara, viwanda, serikali za mitaa n.k.) na Serikali ya Muungano
wala hawasimamiwi katika mambo hayo na Bunge la Muungano? Uko wapi mpaka wa
mamlaka ya Wazanzibari katika ushiriki wa Bunge hilo wakati wao wana Serikali
yao inayopanga na Baraza la Wawakilishi lao linalosimamia mambo yao kama hayo
yasiyo ya Muungano?
Mifano hii inatosha kuonyesha kwamba takriban matatizo
yote, kama si yote, yanatokana na mkanganyiko na mgongano wa maslahi kati ya
pande mbili ambao nao unasababishwa na mfumo usio wazi kuhusiana na mgawanyo wa
madaraka kati ya mamlaka tatu za Muungano zinazotambuliwa katika Mkataba wa
Muungano.
NAFASI YA ZANZIBAR KATIKA MUUNGANO
Baada ya kuangalia kiini cha
matatizo ya Muungano kinachotokana na muundo wa Muungano, sasa tuangalie nafasi
ya Zanzibar katika Muungano huu, hasa kufuatia kauli za kuidhalilisha Zanzibar
zilizotolewa na wanasiasa wa Tanganyika hivi karibuni wakiongozwa na Waziri
Mkuu Mizengo Pinda.
Kutokana na kule kule
kujaribu kujisahaulisha kuwepo kwa Mkataba wa Muungano ambao ndio sheria kuu
(grundnorm) ya Muungano na kuifanya Katiba inayoitwa ya Jamhuri ya Muungano ionekane
kuwa ndiyo Katiba mama na hivyo kuikweza kwamba eti iko juu ya Katiba ya
Zanzibar, zimetolewa kauli kwamba kufuatia hatua ya kuungana na Tanganyika, Zanzibar
imepoteza hadhi na sifa ya kuwa nchi.
Waliosema hivi wanasahau
kwamba Zanzibar ina Katiba yake ambayo ina hadhi sawa na Katiba ya Jamhuri ya
Muungano, na kwamba zote mbili zinapaswa kutafsiri kisawa sawa Makubaliano ya
Muungano.
Katiba ya Zanzibar inatamka
wazi wazi kwamba Zanzibar ni nchi. Utangulizi (Preamble) wa Katiba hiyo ambao
unaeleza dhamira ya Wazanzibari wakiwa ndiyo wenye Katiba hiyo (sponsors of the
Constitution) unabainisha wazi wazi dhamira ya Wazanzibari kulinda na kudumisha
nchi yao na yale yote yanayoitambulisha
Zanzibar kama nchi. Sehemu ya Utangulizi huo inasomeka:
"NA KWA KUWA
tunazingatia na kuthamini kazi nzuri ya Kimapinduzi iliyofanywa na Viongozi wa
Mapinduzi, wakiongozwa na Mwasisi wa Chama cha ASP na Mapinduzi ya Zanzibar ya
1964, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, ambaye fikra zake zitaendelezwa na
kudumishwa daima, kizazi baada ya kizazi katika kupambana na Ukoloni, Ubepari
Unyonge, Uonevu na Dharau, na badala yake kudumisha Uhuru na Umoja, Haki na
Usawa, Heshima na Utu;"
Huko nyuma kabla ya Marekebisho ya Kumi ya Katiba ya
Zanzibar ya 1984 yaliyopitishwa mwaka 2010, ni bahati mbaya kwamba baadhi ya
watu walikuwa wakinukuu vibaya kifungu cha (1) cha Katiba ya Zanzibar kilichokuwa
kikisomeka kwamba, “Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”
kumaanisha kwamba kwa kuwa kwake sehemu ya Jamhuri ya Muungano kunaiondolea na
kuipotezea Zanzibar hadhi yake ya kubakia kuwa nchi. Tafsiri hiyo haikuwa sahihi
kama ilivyofafanuliwa na Jaji Abdullahi D. Zuru kutoka Nigeria, ambaye alikuwa
Mwenyekiti wa Tume ya Kupitia Sheria (Law Review Commission) Zanzibar.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilimuagiza Jaji Zuru
kuipitia Katiba ya Zanzibar na kupendekeza marekebisho ikibidi. Jaji Zuru alisema
katika ripoti yake kuhusu kifungu cha (1) cha Sura ya Kwanza, Sehemu ya Kwanza
ya Katiba ya Zanzibar kuwa:
"Mtu akisoma kwa
makini Utangulizi (Preamble) na Katiba yote kwa
jumla, ataelewa kwamba Zanzibar ni dola yenye mamlaka yake kamili (sovereign
state) na kwamba wale waliotunga Katiba hii hawakuwa na nia ya
kusalimisha na kuachia mamlaka (sovereignty)
ya Zanzibar wakati wa kuundwa Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar, ambao
ulizaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hata hivyo, mtu akisoma maelezo ya
kifungu cha (1) cha Katiba anapigwa na butwaa na kushangaa kwa nini kifungu
hicho cha kwanza kwa kinyemela (surreptiously) kimesalimisha au
kimepuuza mamlaka hayo."
Jaji Zuru anaendelea kusema kuwa anaamini kwamba
waanzilishi wa hatua ya kuzileta pamoja Zanzibar na Tanganyika kuwa Jamhuri
moja, hawajakusudia kuwa hatua hiyo ipoteze (erode) uhuru wa nchi yoyote kati
ya nchi mbili kamili zilizohusika.
Kinyume na hayo, maoni yake ni kwamba nia ilikuwa
kuimarisha uhuru wa kila moja ya nchi hizo mbili sambamba na ule wa
Muungano utakaozaliwa. Mtaalamu huyo anafahamisha kwamba kisheria, "Haki
mbili zikikutana ndani ya mtu mmoja, ni sawa na kusema kwamba ziko ndani ya
watu wawili."
Labda
niinukuu kwa Kiingereza, kama alivyoandika mwenyewe, kwa kufahamika zaidi: "It
is a trite law that when two rights meet in one person, it is the same as if
that were in two persons."
Anaendelea
kusema kwamba ni imani ya Tume yake kabisa kuwa ulipoundwa Muungano, Zanzibar
ilikusudia na ilisisitiza juu ya kuendeleza mamlaka yake ndani ya utaratibu wa
Muungano. Anafafanua:
"Kutokana na haya, tunaamini kwamba
hadhi ya Zanzibar kama inavyoelezwa katika kifungu cha (1) imepotoshwa kwa
sababu (kifungu) hakielezi nia ya wenye katiba (sponsors of this constitution)
na madaraka yaliyotolewa na watu wa Zanzibar..."
Labda
turudi nyuma kidogo tufahamishe kuwa Tume ya Jaji Zuru imeeleza mwanzoni kuwa
madaraka waliyo nayo Baraza la Wawakilishi, ambalo ndilo lililotunga Katiba
hiyo mwaka 1984, yanatokana na wananchi na kwamba Baraza linayashikilia
madaraka hayo kama amana (trust) kwa niaba ya wananchi hao.
"Kwa hiyo, kushindwa kwa Serikali kusimamia misingi ya katiba ni sawa na
kwenda kinyume na amana waliyokabidhiwa na watu wa Zanzibar.”
Haya
yanaelezwa wazi katika kifungu cha 9 cha Katiba ya Zanzibar kinachosema,
"9.-(1) Zanzibar itakuwa ni nchi ya
kidemokrasia na haki za kijamii.
(2) Kwa hiyo hapa inaelezwa rasmi kwamba:-
(a) Mamlaka ya kuendesha nchi ni ya
wananchi wenyewe ambapo nguvu na uwezo wote wa Serikali kufuatana na Katiba
utatoka kwa wananchi wenyewe."
Tukiendelea
na hoja, Jaji Zuru anasema maelezo ya kifungu cha (1) cha Katiba kabla ya
kurekebishwa, ambacho ndicho kama mlango wa kuingilia kwenye Katiba yenyewe,
yanampa msomaji wa nje sura ya kwamba Zanzibar si nchi yenye mamlaka yake
wenyewe. "Kwa hiyo, tunachukulia maelezo haya kama ni kwenda kinyume na
nia ya watu wa Zanzibar ambayo iko wazi na bayana katika Utangulizi (Preamble)
na sehemu nyengine zinazohusika katika Katiba."
Kutokana
na haya Tume ya Kurekebisha Sheria ikapendekeza kifungu hiki kiandikwe upya ili
kuwakilisha nia ya watu wa Zanzibar. Jaji Zuru alipendekeza kisomeke kama
ifuatavyo:
"Zanzibar ni, na itabaki dola yenye
mamlaka, na itakuwa ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa
matakwa na masharti yaliyotajwa katika Mkataba wa Muungano baina ya Dola ya
Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika.”
Kwa
madhumuni ya uelewa zaidi tutanukuu tena kwa Kiingereza kama alivyoandika
mwenyewe Jaji Zuru:
"Zanzibar is and shall remain a
sovereign state, and shall exist as an integral part of the United Republic of
Tanzania, in accordance with the terms and conditions stipulated in the
Articles of Union between the State of Zanzibar and the Republic of
Tanganyika.”
Mapendekezo
ya Tume ya Jaji Zuru yalipelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Disemba 19,
2001, lakini kwa muda mrefu yakawa hayakufanyiwa kazi na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar mpaka pale hatimaye mwaka 2010 ilipoyafikisha mbele ya Baraza la
Wawakilishi ili kurekebisha mapungufu ya kiuandishi ya Katiba ya Zanzibar na
kutafsiri kisawasawa dhamira ya wananchi wa Zanzibar. Vifungu vilivyorekebishwa
vya 1 na 2 sasa vinasomeka kama ifuatavyo:
“1. - Zanzibar ni miongoni mwa nchi mbili
zilizounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
2. - Zanzibar ni Nchi ambayo mipaka yake ni
eneo lote la Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na visiwa vidogo
vilivyoizunguuka bahari yake ambayo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
ikiitwa Jamuhuri ya Watu wa Zanzibar.”
Tukiachana
na mapendekezo hayo, tuangalie Sura ya Kumi na Tatu ya Katiba ya Zanzibar.
Kifungu cha 132 (1) kinachosema:
"132. - (1) Hakuna sheria yoyote
itakayopitishwa na Bunge la Muungano ambayo itatumika Zanzibar mpaka sheria
hiyo iwe ni kwa ajili ya mambo ya Muungano tu na ipitishwe kulingana na maelezo
yaliyo chini ya vifungu vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
(2) Sheria kama hiyo lazima ipelekwe
mbele ya Baraza la Wawakilishi na Waziri anayehusika.
(3) Pale sheria ndogo inapoundwa kwa
mujibu wa uwezo uliowekwa chini ya vifungu vya (1) na (2) sheria hii itatumika
tu pale itapotimiza shuruti zote zilizowekwa kwa matumizi ya Sheria mama kama
ilivyoamrishwa katika kifungu hiki."
Hapa
kuna mambo mawili yanajitokeza. Kwanza kati ya mambo yote ya Muuungano, zaidi
ya yale kumi na moja ya asili, yaliyoongezwa katika orodha ya mambo ya muungano
(xii –xxiii) ni moja tu, kuhusu uandikishwaji wa vyama vya siasa, ambapo mswada
ulipelekwa Baraza la Wawakilishi, ukajadiliwa na kupitishwa. Hivi karibuni
sharti hili lilitekelezwa kuhusiana na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba (Sura ya
83).
Mambo
mengine yote sheria zake hazikuwahi kufikishwa mbele ya Baraza la Wawakilishi.
Kifungu kinachofuata yaani 133 (1) kinasema:
"133.-(1) Hakuna kodi
ya aina yoyote itakayotozwa isipokuwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na
Baraza la Wawakilishi au kwa utaratibu uliowekwa kisheria na uliotiliwa nguvu
ya kisheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi.
(2) Masharti yaliyomo
katika kijifungu hiki hayatalizuwia Bunge kutumia mamlaka ya kutoza kodi ya
aina yoyote inayohusiana na mambo ya Muungano kwa mujibu wa madaraka ya Bunge
hilo, kwa kujuwa kwamba mashauriano baina ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano yamefanywa na kukubalika sehemu zote mbili
kabla kupitishwa sheria."
Si jambo la siri kwamba kulikuwa na mvutano mkubwa kati
ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Dk. Salmin Amour na Serikali ya Jamhuri ya
Muungano kuhusiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na suala zima la
uoanishaji wa viwango vya ushuru na kodi (harmonisation
of tariffs). Hadi leo wananchi wa Zanzibar wanaiona TRA kama ndiye adui
mkubwa wa uchumi wao, iliyoua biashara visiwani na kuwatia Wazanzibari katika
ufukara usiosemeka.
Ni wazi basi kwamba uundwaji wa TRA haujatimiza masharti
ya kifungu cha 133 (2) cha Katiba ya Zanzibar kwa maana ya kuwepo na
mashauriano baina ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya
Muungano na kukubalika sehemu zote mbili kabla kupitishwa sheria.
Inawezekana kukazuka hoja kwamba pale Katiba ya
Zanzibar inapopingana na Katiba ya Muungano ni ile ya Muungano ndio yenye
nguvu. Ndiyo! Hii ni kuhusu vifungu vinavyowiana na Mkataba wa Muungano kama
yalivyokuwa yamekubaliwa na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya
Tanganyika hapo mwaka 1964. Vyengine vyote ni batili na hapo moja kwa moja
Katiba ya Zanzibar ndiyo itakayosimama.
Kwa msingi wa hoja hizi, ni ukweli usio na ubishi kwamba
Zanzibar imeendelea kubaki na hadhi yake kama nchi hata baada ya kuingia katika
Muungano na Tanganyika na ndiyo maana Katiba yake, pamoja na mapungufu madogo
madogo, bado imelinda kwa nguvu zote hadhi hiyo.
Naelewa kwamba kuna watu wanatumia uamuzi wa Mahkama ya
Rufaa ya Jamhuri ya Muungano katika kesi maarufu ya Machano Khamis Ali na wenzake 18 dhidi ya SMZ uliotamka kwamba
Zanzibar si nchi na kwamba kosa la uhaini haliwezi kutendeka Zanzibar kuwa ni
msingi wa hoja kwamba vifungu nilivyovitaja vya Katiba ya Zanzibar vinakuwa
havina maana yoyote pale vinaposititiza hadhi ya Zanzibar kama nchi.
Ni muhimu kueleweka kwamba uamuzi huu wa Mahkama ya Rufaa
umejaa utatanishi. Kwanza, ulitolewa wakati Serikali ikiwa tayari imeondosha
mashtaka dhidi ya watuhumiwa na kuwaachia huru. Kwa msingi huo, mtu anajiuliza
uamuzi huo wa Mahkama ya Rufaa wakati unatolewa ulikuwa na uhalali upi kisheria
na ulikuwa unahusu kesi ipi wakati kesi ilishaondolewa na Jamhuri mbele ya
Mahkama. Lakini pili, mtaalamu wa masuala ya katiba anayeongoza hapa Tanzania,
Prof. Issa Shivji amefanya mapitio ya uamuzi huo na kubainisha makosa mengi
sana ya kisheria yaliyomo. Kubwa katika makosa hayo ni kule Majaji wanaohusika
kudharau na kutoitumia kabisa Katiba ya Zanzibar katika kufikia uamuzi wao.
Katika hitimisho lake, Prof. Shivji anasema:
“The conclusion
from this quick examination of the Zanzibar Constitution is that Zanzibar is a
sovereign and a state, albeit its sovereignty is limited and the jurisdiction
of the Executive and the Legislature is limited to non-Union matters in
Zanzibar while its Judiciary, as epitomised by the High Court, has unlimited
jurisdiction. A Mzanzibari owes allegiance to the State of Zanzibar and
therefore an offence of treason can be committed against the state of Zanzibar.
This is irrespective of the fact that treason may be stipulated as an offence
in the union law; nevertheless it can be tried in the courts of Zanzibar.” [10]
“Hitimisho la upembuzi huu wa haraka wa Katiba ya
Zanzibar ni kwamba Zanzibar ni dola na ni nchi, ijapokuwa nguvu yake ya kidola
ina mipaka na uwezo wa Mamlaka ya Utawala na Mamlaka ya Kutunga Sheria
umewekewa mipaka kwa mambo yasiyo ya Muungano ndani ya Zanzibar wakati Mamlaka
ya Utoaji Haki, ikiwa inaongozwa na Mahkama Kuu, ina uwezo kamili usio na
mipaka. Mzanzibari ana utii kwa Dola ya Zanzibar na hivyo kosa la uhaini
linaweza kutendeka dhidi ya Dola ya Zanzibar. Hii ni bila ya kujali kwamba
uhaini unaweza kuainishwa kuwa ni kosa kupitia sheria ya Muungano; lakini bado
kosa hilo linaweza kuhukumiwa katika Mahkama za Zanzibar.”
VIPI TUTOKE HAPA TULIPO?
Inakaribia
miaka 49 sasa tangu uundwe Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Kulikuwa na wakati wa kutosha kurekebisha kasoro
zilizopo. Hilo halikuwezekana kutokana na ubabe wa Mwalimu Nyerere ambaye
aliamua kuwatia shemere Wazanzibari na kuhakikisha Muungano unakwenda kama
alivyotaka yeye hata baada ya “kuondoka madarakani”.
Si jambo la kuficha kwamba wananchi wa pande zote mbili
za Muungano wamechoshwa na unafiki uliopo na wanadai mfumo na muundo mpya wa
Muungano utakaoweka misingi mipya ya ushirikiano.
Katika mijadala mbali mbali inayoendelea katika
ukusanyaji wa maoni ya wananchi, vyama vya siasa na taasisi nyengine za kijamii
kumetolewa hoja kwamba suluhisho la matatizo niliyoyafafanua hapo juu na
mengine mengi yanayoukabili Muungano huu, kumejitokeza mapendekezo
yanayoelekeza kwamba ufumbuzi wake ni muundo wa Serikali Moja, Serikali Mbili
zilizopo sasa pamoja na marekebisho kadhaa au Serikali Tatu. Kwa upande wa
Zanzibar, wananchi walio wengi wamependekeza kuwepo kwa Muungano wa Mkataba
(Treaty based Union) kama njia bora ya kudumisha mahusiano makongwe kati ya
Zanzibar na Tanganyika.
Kwa upande wangu, siamini kama Serikali Moja, Mbili au
Tatu zitaweza kumaliza matatizo yaliyopo ya Muungano na hasa kule kutokuaminiana
kukubwa kulikojengeka kutokana na matatizo hayo kuachwa muda mrefu bila ya
kushughulikiwa au kushughulikiwa kwa njia za hotuba za kisiasa zaidi zisizofuatiwa na utekelezaji wowote.
Sababu zangu za kutoiona mifumo hiyo kama njia sahihi ya ufumbuzi wa matatizo
yanayotukabili ni hizi zifuatazo:
Serikali
Moja:
Mfumo wa Serikali moja umekuwa ukitajwa kuwa utaondoa
manung’uniko na kelele zote kuhusu matatizo ya Muungano lakini bado unaonekana
kuwa na matatizo yafuatayo:
i.
Mfumo huu
utazifuta kabisa nchi za Tanganyika na Zanzibar na kuwa na nchi moja yenye
mamlaka moja inayosimamiwa na Serikali moja.
ii.
Ingawa
mfumo huu unaweza kuungwa mkono na Watanganyika walio wengi, Wazanzibari
hawawezi kuukubali kabisa mfumo huu kwa sababu utafuta utambulisho wao na
historia yao.
iii.
Katika
mfumo huu wa kuwa na nchi moja yenye mamlaka moja, Zanzibar itachukuliwa kama
eneo jengine lolote la Tanzania na hivyo kutokuwa na uwezo wa kujiletea
maendeleo yake na badala yake itategemea maendeleo yatakayopangwa na Serikali
kuu kulingana na rasilimali zitakazotengwa kwa ajili ya eneo la Zanzibar kama
inavyopangwa kwa maeneo mengine.
Serikali
Mbili:
Mfumo wa serikali mbili uliopo hivi sasa una mkanganyiko
wa mambo kadhaa kwa mfano:
(a)
Kutokuwepo
kwa mshirika mmoja wa asili wa Muungano yaani Tanganyika. Hivyo linapotokea
tatizo la Muungano badala ya kukutana pande mbili za Muungano na kujadiliana
kwa misingi ya usawa sasa majadiliano yanakuwa baina ya Serikali ya Muungano na
Serikali ya Zanzibar. Majadiliano ya namna hii yanakosa misingi ya haki na
usawa.
(b)
Mabadiliko
ya Katiba yaliyomuondoa Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano yalikwenda kinyume kabisa na makubaliano ya awali ya Muungano.
Mabadiliko haya yanamuondoa mmoja wa washirika wakuu katika Serikali ya
Muungano. Mkataba wa Muungano, ibara ya (iii) (b) ulitamka bayana kwamba Rais
wa Zanzibar atakuwa ndiye msaidizi mkuu wa Rais wa Muungano. Jee hivi sasa nani
msaidizi mkuu? Makamu wa Rais kwa mfumo wa sasa kwa mfano anatoka Zanzibar sio
kiongozi mwenye dhamana ya kiutendaji Zanzibar na hivyo hawezi kuwakilisha
matakwa ya Zanzibar katika Muungano.
(c)
Kumekuwa
na mkanganyiko vile vile kwa mambo ya Zanzibar ambayo siyo ya Muungano lakini
mambo hayo yanashughulikiwa na Serikali ya Muungano katika ngazi zote za
kimataifa. Kwa mfumo huu, Tanganyika inatumia jina la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kujifaidisha kwa mambo yote yasiyo mambo ya Muungano katika nyanja za
kimataifa. Mifano michache ya maeneo haya ni elimu, afya, kilimo, mazingira,
michezo, utamaduni, mawasiliano, miundombinu, usafiri baharini na angani ambapo
katika jumuiya zote za kimataifa Tanganyika inashiriki ikitumia jina la
Tanzania huku Zanzibar ikiachwa bila ya faida yoyote au ikiwepo basi ni ile
inayotegemea hisani ya Tanganyika.
(d)
Mfumo
uliopo wa Serikali mbili hautoi fursa ya wazi kwa upande mmoja wa Muungano (Tanganyika)
kutetea maslahi yake ndani ya Muungano.
(e)
Wabunge wa
Zanzibar wanashiriki katika Bunge la Muungano kujadili mambo ambayo siyo ya
Muungano.
(f)
Mfumo
uliopo unaochanganya mamlaka mbili (ile ya Serikali ya Muungano kwa mambo yote
ya Muungano na ile ya Tanganyika kwa mambo yake yasiyokuwa ya Muungano) unaleta
mkanganyiko mkubwa katika suala la kujua mipaka ya gharama za uendeshaji wa
Muungano na mapato yanayotokana na taasisi za Muungano. Hali hiyo inaleta
kutoaminiana kuhusiana na jinsi ya kuchangia gharama za uendeshaji na jinsi ya
kugawana mapato baina ya nchi mbili zinazounda Muungano huo.
(g)
Ushahidi
wa wazi wa kwamba mfumo uliopo umeshindwa kufanya kazi na wala hauwezi
kurekebishika ni kwamba katika miaka 20 iliopita kumeundwa Tume na Kamati 8 kwa
upande wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Tume na Kamati 13 kwa upande wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mbali na kuwepo kwa Kamati ya Kudumu ya
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano ikiwajumuisha Waziri Mkuu wa Serikali ya
Muungano na Makamu wa Pili wa Rais (zamani Waziri Kiongozi) wa SMZ lakini zote
zimeshindwa kutatua matatizo ya Muungano na badala yake yamekuwa yakizidi kila
uchao.
Serikali
Tatu:
Baadhi ya vyama vya siasa na hata wasomi wa sheria
wamekuwa wakipendekeza mfumo wa Serikali tatu (Serikali ya Muungano, Serikali
ya Tanganyika na Serikali ya Zanzibar) kama suluhisho la matatizo ya Muungano.
Hata hivyo, mfumo huu nao kwa sasa unaonekana bado hautaondoa manung’uniko kwa
upande wa Zanzibar:
(a)
Mfumo wa
Shirikisho la Serikali Tatu utatoa mamlaka ya ndani kwa nchi mbili zinazounda
Muungano huu na kuwa na Serikali zake za kusimamia mamlaka hayo lakini bado
mamlaka ya kidola (sovereignty) yatabaki katika Serikali ya Muungano. Madai
makubwa yanayotolewa na Zanzibar hivi sasa yanahusu kurejesha ‘sovereignty’ ili
kuifanya Zanzibar, serikali yake na viongozi wake wawe na hadhi ya kutambuliwa
kitaifa na kimataifa. Hilo halitapatikana katika
mfumo wa Serikali tatu.
(b)
‘Sovereignty’ inayoshikiliwa na
Serikali ya Muungano ambayo ndiyo itakayoziwakilisha nchi mbili kimataifa bado
ina nafasi kubwa ya kuweza kutumika kumfaidisha mshirika mkubwa zaidi katika
Muungano huo (Tanganyika) kuliko kwa mshirika mdogo (Zanzibar) kwa kule tu
kujiona kwake ni mkubwa (big brother
attitude).
(c)
Upo uwezekano wa kuendelea
kuwepo kwa kutoaminiana kutokana na kila nchi kuwa na Serikali yake na hivyo
kuwa na chombo cha kupanga mambo yake, hali inayoweza kuifanya Serikali ya
Muungano ijikute haina uwezo wa kuzisimamia Serikali hizo za mamlaka ya ndani
na hivyo kupoteza uhalali wake wa kisiasa.
(d)
Iwapo mambo ya Muungano
yatabaki kama yalivyo au yatarekebishwa kwa uchache, kuwepo kwa mfumo wa
Serikali tatu hakutorudisha mamlaka ya Zanzibar kupanga na kusimamia uchumi
wake.
MFUMO MPYA WA MUUNGANO WA
MKATABA:
Kama
nilivyotangulia kueleza, tumedumu na Muungano wa Katiba kwa miaka 49 ambao
pamoja na mafanikio ya kuziweka nchi zetu mbili pamoja katika kipindi chote
hicho, bado umeshindwa kutujengea kuaminiana kwa dhati na zaidi umeshindwa
kuyatatua matatizo ya msingi yanayotokana na maumbile ya mfumo huo.
Ulimwengu
wa sasa umeshuhudia aina mpya ya mahusiano kati ya nchi huru ambao hutoa nafasi
ya mashirikiano kwa maeneo yanakayokubaliwa na nchi husika huku kila nchi
ikibaki na mamlaka yake kama nchi kamili (sovereign status). Mfumo huu kisheria
unaitwa ‘CONFEDERATION’ ambao kimsingi ni Muungano wa Mkataba (Treaty based Union).
Katika mfumo huu, yale maeneo ya ushirikiano huwekwa katika mkataba au mikataba
baina ya nchi zilizoamua kushirikiana na hutoa fursa ya kurekebishwa kila
mahitaji yanapojitokeza kwa kadiri na kwa mujibu wa makubaliano yaliyomo kwenye
mkataba au mikataba hiyo.
Umoja
wa Ulaya (European Union - EU) ni mfano mzuri wa muungano wa aina hii ambapo
nchi wanachama zinashirikiana katika maeneo mengi yaliyomo katika Mikataba
tofauti lakini kila nchi mwanachama imebaki kuwa na hadhi yake kama nchi na
kubaki na uanachama wake katika Umoja wa Mataifa (UN) na hata katika mashirika
mengine ya kimataifa. Katika Umoja wa Ulaya (EU), miongoni mwa maeneo
wanayoshirikiana ni pamoja na:
(a)
Sarafu moja;
(b)
Uhamiaji;
(c)
Uratibu wa sera za mambo ya nje
za nchi wanachama;
(d)
Ulinzi;
(e)
Soko la pamoja la bidhaa, ajira
na huduma;
(f) Uratibu
wa sera za uchumi na fedha za nchi wanachama;
(g)
Hifadhi ya mazingira;
(h)
Viwango vya usalama na afya
(health and safety standards).
Mfano
mwengine wa ushirikiano kwa nchi za Ulaya nje ya EU ni ule unaohusu kuwa na
visa ya pamoja kwa wageni wanaoingia katika nchi zilizo katika Mkataba wa
Schengen ambao hutoa visa inayoitwa ‘SCHENGEN VISA’. Baadhi ya nchi wanachama
wa EU na wasio wanachama wa EU (kwa mfano Norway) ni wanachama wa utaratibu
huu.
Kwa
upande mwengine, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ni mfano mwengine mzuri wa
ushirikiano wa aina hii. Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (East African
Community Treaty) unatambua maeneo 17 ya ushirikiano miongoni mwa nchi
wanachama. Maeneo hayo ni:
(a)
Ushirikiano katika Masuala ya
Sarafu na Fedha;
(b)
Ushirikiano katika Biashara
Huria na Maendeleo ya Biashara;
(c)
Ushirikiano katika Uwekezaji na
Maendeleo ya Viwanda;
(d)
Ushirikiano katika Uwekaji
Viwango, Kuhakikisha Ubora wa Bidhaa, Utabiri wa Hali ya Hewa na Vipimo;
(e)
Ushirikiano katika Mahusiano na
Jumuiya nyengine za Kikanda na za Kimataifa pamoja na ushirikiano na nchi
washirika wa maendeleo;
(f) Ushirikiano
katika Miundombinu na Huduma;
(g)
Ushirikiano katika Kukuza
Rasilimali Watu, Sayansi na Teknolojia;
(h)
Ushirikiano
katika Kilimo na Uhakika wa Chakula;
(i)
Ushirikiano
katika Utunzaji Mazingira na Usimamizi wa Maliasili;
(j)
Ushirikiano
katika Utalii na Usimamizi wa Wanyamapori;
(k)
Ushirikiano
katika Afya, Ustawi wa Jamii na Utamaduni;
(l)
Ushirikiano
katika Kukuza Ushiriki wa Wanawake katika Maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi;
(m)
Ushirikiano katika Masuala ya
Sheria na Mahkama;
(n)
Ushirikiano
katika Mambo ya Kisiasa;
(o)
Ushirikiano
katika Sekta Binafsi na Asasi za Kiraia;
(p)
Ushirikiano
katika Uhuru wa Watu kwenda watakapo, Huduma za Kazi, Haki ya Kuishi na Ukaazi;
na
(q)
Ushirikiano katika Maeneo
Mengine.
Lililo
dhahiri katika miungano ya mikataba ya aina zilizotajwa hapo juu ni kuwa
misuguano kwa kiasi kikubwa hupungua kwani kila nchi hubaki na mamlaka yake na
uhuru wa kujiamulia na wakati huo huo kujenga misingi mizuri ya ushirikiano na
nchi wanachama.
MUUNGANO WA MKATABA KATI YA
ZANZIBAR NA TANGANYIKA:
1.
Kutokana na hoja nilizozieleza
hapo juu, mimi ninapendekeza kuwa baada ya uzoefu wa miaka 49 wa Muungano wa
Katiba (Constitutional Union) kati ya Zanzibar na Tanganyika ambao baadhi ya
matatizo yake ya kimaumbile yameelezwa na kufafanuliwa hapo juu, sasa Zanzibar
na Tanganyika ziingie katika mfumo wa “CONFEDERATION”
kupitia Muungano wa Mkataba (Treaty based Union).
2.
Katika mfumo huo wa Muungano wa
Mkataba, kutakuwa na Serikali mbili ambapo Jamhuri ya Tanganyika itakuwa na
Serikali yake na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar itakuwa na Serikali yake, zote
mbili zikiwa na mamlaka kamili kitaifa na kimataifa, na kisha Serikali hizo
mbili zitafunga mkataba wa mashirikiano baina yao ambao unaweza ukapewa jina la
‘Tanzanian Union Treaty’. Yale maeneo yatakayokubaliwa kuwa chini ya
ushirikiano wa nchi mbili huru yatasimamiwa na Kamisheni ya Muungano (Tanzanian
Commission) kama ilivyo kwa Kamisheni ya Ulaya (European Commission) au jina
jengine lolote litakalokubaliwa na nchi mbili hizi.
3.
Kila nchi kati ya Zanzibar na
Tanganyika zitakuwa na hadhi ya nchi kamili (sovereign states) na zitakuwa na
uanachama wake katika Umoja wa Mataifa (UN) na pia katika jumuiya, mashirika na
taasisi nyengine za kimataifa lakini kwa kuzingatia msingi wa mashirikiano
zinaweza kukubaliana kuratibu sera zake za mambo ya nje kadiri zitakavyoona
inafaa.
4.
Maeneo ya kuingia katika
Mkataba au Mikataba ya Ushirikiano kati ya Zanzibar na Tanganyika yataamuliwa
na serikali mbili zitakazokuwa na mamlaka kamili kila moja katika eneo lake.
Mambo yanayoweza kufikiriwa ni pamoja na:
(i)
Ushirikiano katika Ulinzi na Usalama;
(ii)
Ushirikiano
katika Uwekaji Viwango, Kuhakikisha Ubora wa Bidhaa, Utabiri wa Hali ya Hewa na
Vipimo;
(iii)
Ushirikiano katika Mahusiano na
Jumuiya nyengine za Kikanda na za Kimataifa pamoja na ushirikiano na nchi
washirika wa maendeleo;
(iv)
Ushirkiano katika Kukuza
Rasilimali Watu, Sayansi na Teknolojia;
5.
Kwa
kufuata mfumo wa sheria za nchi za Jumuiya ya Madola (common law system)
inapendekezwa kuwa Mkataba wa Ushirikiano kati ya Zanzibar na Tanganyika utiwe
saini na Rais wa Jamhuri ya Zanzibar na Rais wa Jamhuri ya Tanganyika baada ya
mazungumzo yatakayohusisha wawakilishi watakaoteuliwa kuunda timu za mashauriano
na majadiliano za Serikali za nchi mbili hizi. Kabla ya kutiwa saini na Marais
wa nchi mbili hizi, Rasimu ya Mkataba huu baada ya kukubaliwa ifikishwe mbele
ya Bunge la Tanganyika na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kwa ajili ya
kujadiliwa na kutolewa maoni na kisha Rasimu hiyo ipelekwe kwa wananchi wa
Zanzibar na wa Tanganyika kupitia njia ya kura ya maoni kwa ajili ya
kuidhinishwa kufuatana na Sheria ya Kura ya Maoni ya kila nchi.
NI ZIPI FAIDA ZA MUUNGANO WA MKATABA:
1.
Hakuna
khofu ya nchi moja kuimeza au kuitawala nchi nyengine.
2.
Kila
nchi inabaki na uhuru na mamlaka yake
kamili kitaifa na kimataifa kuamua mambo yake.
3.
Kila
nchi mwanachama ina uhuru wa kujitoa katika jambo lolote ililoamua mwanzo
kushirikiana pale inapoona hakuna maslahi au faida kuendelea nalo.
4.
Huvutia
nchi nyingi kuingia katika Muungano wa aina hiyo kwa sababu hakuna khofu ya
kupoteza mamlaka au kupunguziwa madaraka au mambo yake kuamuliwa na nchi
nyengine.
5.
Mahusiano
huwa ni ya kirafiki na ya ujirani mwema yanayopelekea kuaminiana na kuondoa
kutiliana shaka kusikokwisha.
KAMA NI
MKATABA, KWA NINI ISIWE KUPITIA EAC TU?
Wapo baadhi ya watu wakiwemo Makamishna wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba waliohoji kwamba iwapo Zanzibar inaona hakuna haja tena ya
kuendelea na mfumo uliopo wa Muungano na badala yake inataka kuwa na
mashirikiano kupitia Muungano wa Mkataba kwa mambo yatakayokubaliwa, kwa nini
mashirikiano hayo yasiwe kwa kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambayo
pia ni aina ya Muungano wa Mkataba? Wenye hoja hiyo wanasema basi wacha
Zanzibar na Tanganyika zikutane Afrika Mashariki.
Hoja hii ni nzuri lakini haizingatii uhalisia wa
mambo. Pamoja na kuundwa upya kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kupitia
Mkataba ambao unahusisha maeneo mengi kati ya yale niliyoyataja hapa kwamba
yanaweza kufikiriwa kuwa ya ushirikiano kati ya Zanzibar na Tanganyika, ukweli
unabaki kuwa utekelezaji wake katika eneo la Afrika Mashariki umekuwa ni mdogo
mno.
Nchi tano zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki –
Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi – hazionekani kuwa zimejenga
kuaminiana kwa dhati licha ya matamshi ya hamasa za kisiasa yanayotolewa na
viongozi wake. Ndiyo maana maeneo mengi yamebaki katika makaratasi lakini
hakuna utekelezaji. Hata hatua zilizotangazwa kuwa zinapaswa kufikiwa kuelekea
Shirikisho la Afrika Mashariki hazionekani kutekelezwa kwa dhati na badala yake
kumekuwa na kutegana na hata kuogopana.
Baada ya miaka 49 ya kuwa pamoja katika Muungano
(pamoja na matatizo yake yote), Zanzibar na Tanganyika angalau zimekuwa na uzoefu
wa kufanya kazi pamoja. Kubadili aina ya mahusiano na mashirikiano yake kutoka
kwenye Muungano wa Kikatiba kwenda kwenye Muungano wa Mkataba kunaweza kuwa
jambo linalowezekana zaidi katika utekelezaji kuliko nchi hizi tano na pengine
kunaweza kutoa mfano wa vipi utekelezaji wa maeneo hayo ya mashirikiano
unavyopaswa kuendeshwa na kusimamiwa.
Isitoshe unaweza tukawa mwanachama wa EAC na bado
kukawepo ushirikiano wa Zanzibar na Tanganyika kupitia mkataba baina yao peke
yao. Duniani iko mifano ya nchi ambazo pamoja na kuwa ni wanachama wa pamoja wa
miungano au jumuiya za ushirikiano zenye kushirikisha nchi nyingi zaidi, bado
kunakuwa na nchi mbili ambazo kutokana na historia ya ushirikiano wake zinabaki
kuwa na ushirikiano wao mwengine unaozihusisha nchi hizo tu. Mfano katika suala
la ushirikiano wa ulinzi, pamoja na kwamba Marekani na Uingereza zote mbili ni
wanachama wa NATO lakini bado nchi mbili hizo zina mikataba ya peke yao
kuhusiana na ushirikiano wa ulinzi kati yao. Katika Ulaya, kuna mashirikiano
kupitia mkataba baina ya nchi tatu – Belgium, The Netherlands and Luxembourg (BENELUX) – lakini
bado zote ni wanachama wa Umoja wa Ulaya (European Union).
KIPINDI CHA MPITO:
Hali ya kubadilisha msingi wa mahusiano ya Zanzibar na
Tanganyika kutoka kwenye Muungano wa Katiba (Constitutional
Union) kwenda kwenye Mfumo wa kisasa wa Muungano wa Mkataba (Treaty based Union) bila shaka
utahusisha mabadiliko makubwa ambayo yanahitaji kipindi cha mpito (transitional period) na kuwepo kwa
utaratibu wa mpito (transitional process)
kutoka mfumo uliopo sasa kwenda kwenye mfumo mpya.
Katika kipindi hicho cha mpito, maoni ya watu wa Tanganyika kuhusu Katiba
yaliyokusanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba yanaweza kutumika kuandaa rasimu
ya Katiba ya Tanganyika na baada ya kupitisha Katiba ya Tanganyika, Serikali za
nchi mbili (Zanzibar na Tanganyika) zikae pamoja kuchagua maeneo ya
kushirikiana na kisha kuandaa Mkataba wa Mashirikiano yao.
Kutahitajika kuundwe timu ya watalaamu wa masuala ya
kisheria na kiutawala kutoka Zanzibar na Tanganyika na pia kuhusisha kuomba
wataalamu waliobobea wa fani hizo na waliosimamia vipindi vya mpito kama hivi
katika nchi nyengine kuja kusaidia kuweka utaratibu maridhawa utakaohakikisha
kuendelea kuwepo kwa mahusiano ya kidugu ya nchi hizi katika mfumo mpya.
Jumuiya za kimataifa kama Umoja wa Mataifa (UN), Jumuiya ya Madola (The
Commonwealth), Umoja wa Afrika (AU), Umoja wa Ulaya (EU) na nchi jirani na nchi
za nje zenye kufuata mfumo wa sheria za kiingereza kama Uingereza, Malaysia, Singapore,
Kenya, Uganda na Afrika Kusini zinaweza kuombwa kusaidia kutoa wataalamu
watakaokuwa kama washauri waelekezi (consultants) kwa nchi zetu wakati wa
maandalizi ya utaratibu wa mpito (transitional process) kuelekea Muungano wa
kisasa wa Mkataba wa Zanzibar na Tanganyika chini ya misingi ya uhuru, usawa,
udugu na ukweli.
MUUNGANO
WA MKATABA NI SAWA NA KUVUNJA MUUNGANO?
Wasioitakia mema Zanzibar au wang’ang’anizi wa mfumo
uliopo wa Muungano waliouzoea (pengine kwa sababu unawanufaisha wao) wanaweza
kudai kwamba hatua hizi zinazopendekezwa haziashirii nia njema ya kuendeleza na
kuimarisha Muungano. Mimi binafsi na wenzangu tunaoamini katika Muungano wa
Mkataba hatuamini hivyo. Tunaamini katika kuwa wakweli na wawazi, kwamba hivyo
ndivyo mahitaji ya wakati huu na zama hizi yanavyodai.
Ulimwengu unabadilika kwa kasi. Zama za kuendesha mambo
kwa ubabe na ukichwa ngumu zimepitwa na wakati. Tuache ile tabia ya kuyaona
mapendekezo ya kubadili mfumo wa Muungano kuwa yana nia ya kuuvunja Muungano
huo. Muungano ili udumu unahitaji ridhaa ya walioungana. Muasisi wa Muungano
huu, Mwalimu Nyerere mwenyewe, aliwahi kueleza umuhimu wa ridhaa katika masuala
haya na kuonyesha kwamba ridhaa ya mshirika mmojawapo ikiondoka, Muungano
hauwezi kusimama. Alisema mwaka 1968:
“If the mass of the
people of Zanzibar should, without external manipulation, and for some reason
of their own, decide that the Union was prejudicial to their existence, I could
not bomb them into submission … The Union would have ceased to exist when the
consent of its constituent members was withdrawn.” [11]
“Iwapo wananchi walio wengi wa Zanzibar wataamua, bila
ya msukumo wa kutoka nje, na kwa sababu zao wenyewe, kwamba Muungano unaathiri
kuendelea kuwepo kwao, siwezi kuwalazimisha kwa kuwapiga mabomu … Muungano
utasita kuendelea pale ridhaa ya washirika wake itakapoondolewa.”
Wazanzibari ni watu wenye historia ya maingiliano ya
jamii za watu mbali mbali na hivyo hawawezi kukataa umoja, alimradi tu umoja
huo uwe na maslahi na faida kwao. Mfumo uliopo sasa hauinufaishi Zanzibar na
hivyo haukubaliki kwa Wazanzibari. Koti la Muungano kama lilivyo sasa linabana
sana. Wakati umefika tushone koti jipya kwa mujibu wa mahitaji ya zama hizi.
Hakuna mabadiliko yasiyowezekana kufanyika na
kusimamiwa vyema iwapo tutatumia njia ya mazungumzo. Mazungumzo makini, ya kina
na yenye kuambatana na nia njema kwa wahusika wote ndiyo njia pekee ya
matumaini katika kuyapatia ufumbuzi matatizo yanayolikabili Taifa letu. Hakuna
mbadala wa mazungumzo. Nje ya mazungumzo ni fujo.
[1] Nnoli, O (1978) Self Reliance and Foreign Policy in Tanzania : The Dynamics of the Diplomacy of a New
State, 1961 to 1971, NOK Publishers (New York ),
Uk .
91; Othman, Haroub (1979) State
Succession with regard to International Treaties – Some Theoretical Observations
on the Practice of Anglophonic Africa, Ph.D. Thesis, University of Dar es
Salaam (Dar es Salaam), Uk. 413.
[2] Mazrui, Ali A.
(1994) ‘Imperialism after the Empire:
Lessons from Uganda and Tanzania ’ The Sunday Nation (Nairobi ),
May 22, 1994
[3] Kwa maelezo zaidi kuhusiana
na nadharia hizi, angalia kwa mfano, Nyerere, Julius K. (1965) ‘The Nature and
Requirements of African Unity’ katika jarida la African Forum, Vol. 1, No. 1
(1965), Uk .
46.
[4] Angalia ‘A Declaration of Federation by the
Governments of East Africa on June 5, 1963’ lenye Kumbukumbu Nam .
13/931/63/PDT/1/1 kama lilivyochapishwa katika Tanganyika Government (1964) Meetings and Discussions on the Proposed
East African Federation, Ministry of Information (Dar es Salaam ).
[5] William Edget
Smith (1971) We Must Run While They Walk:
A Portrait of Africa’s Julius Nyerere, Gollancz (London ),
Uk .
121.
[6] Nyerere, Julius
K. (1966) Freedom and Unity, Oxford University
Press (Dar es Salaam), Uk .
300.
[7] Shivji, Issa G.
(1994) ‘The Union: Hopes and Fears’ The Family Mirror (Dar
es Salaam ), First Issue, January 1994, uk . 5
[8]
Msekwa, Pius (1994) ‘The State of the
Union’ - Paper presented to a Seminar
on the State of the Union, Mkonge Hotel, Tanga 25 - 27 February, 1994.
[9] Mazrui, Ali A.
(1994) ‘Imperialism after the Empire:
Lessons from Uganda and Tanzania ’ The Sunday Nation (Nairobi ),
May 22, 1994
[10] Shivji, Issa G. (2005) ‘Sovereignty and Statehood in Zanzibar in
the Union: Critical Comments on S.M.Z. v.
Machano Khamis Ali & 17 Others’, kama ilivyochapishwa katika Peter,
Chris Maina and Othman, Haroub (2006) Zanzibar
and the Union Question, Zanzibar Legal Service Centre Publication Series
(Zanzibar), Uk. 186.
[11] The Observer (London ),
April 20, 1968
No comments:
Post a Comment