Habari za Punde

Watoa nyaraka feki wakidai mashamba ya serikali ni mali yao



 Masanja Mabula,Pemba
SERIKALI ya Wilaya ya Wete imevishtukia vitendo vinavyofanywa na baadhi ya wananchi walio nje ya kisiwa cha Pemba wanaoingia ndani ya wilaya hiyo na kudai kuwa mashamba ya mikarafuu yanayomilikiwa na serikali kuwa ni mali yao.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa wilaya hiyo, Omar Khamis Othman  amewaagiza Masheha wote kuyaorodhesha mashamba yote ya serikali na kuyawasilisha ofisini kwake.
Alisema katika kipindi  baada ya karafuu kupandishwa bei kumeibuka watu kutoka ndani na nje ya wilaya hiyo wanaodai kuwa mashamba yaliyogawiwa kwa wananchi mara baada ya Mapinduzi ni mali yao.

"Tumepokea taarifa kutoka kwa Masheha wakisema kumekuwepo baadhi ya wananchi  wanaodai mashamba yaliyogawiwa eka tatu tatu na serikali ni yao , hili sisi hatuwezi kulivumilia na tayari n tumewaagiza Masheha kuwa macho na watu wa aina hiyo,"alisema Mkuu huyo wa wilaya wakati akizungumza na gazeti hili.
Amezitaja Shehia ambazo vitendo hivyo vimejitokea kuwa ni shehia ya Mtambwe Kaskazini na Kusini , Pandani na  Kambini Shehia ambazo  karafuu zinaonekana kuzaliwa kwa wingi.
 Aidha alisema wananchi ambao wanatuhumiwa kuwakabidhi  watu hao mashamba, wajue kuwa wamekwenda kinyume na sheria kwani walitakiwa kuyakabidhi kwa serikali kwanza kabla ya kuchukua hatu hiyo.
Hata hivyo alifahamisha kuwa wapo baadhi ya watendaji wa Idara ya Ardhi Pemba ambao wamekuwa wakichohea hali hiyo, lakini bado serikali ya wilaya inaendelea kufanya uchunguzi na wakibainika watawatolewa taarifa kwa viongozi wao.
Naye Sheha wa Pandani, Said Hamad  alisema iwapo masheha hawatakuwa makini juu wa watu hao , basi wananchi waliopewa mashamba na serikali watakosa sehemu ya kulima kufuatia na nyaraka bandia wanazotoa watu hao.
Aliwataka Masheha kuwa makaini na kutokubali kutokea kwa vitendo hivyo katika maeneo yao, na kwamba wawe waangalifu na wepesi wa akutoa taarifa katika ofisi za wilaya ili hatua za haraka zichukuliwe.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.