Na Mwandishi wetu
WIMBI la ujambazi limeanza kuibuka
upya katika manispaa ya mji wa Zanzibar kwa kuvamiwa wafanyabiashara wa dawa
katika maeneo mbali mbali.
Katika tukio la hivi karibuni,
muuzaji wa duka la Izamir Pharmacy Limited liliopo Majestiki mjini Unguja,
alinusurika kushambuliwa na majambazi hayo wakati akiwa njiani kuelekea
nyumbani kwake.
Mfanyabiashara huyo, Nizar Machano
aliiambia gazeti hili kwamba watu wanne
ambao anaamini kuwa ni majambazi walimvamia katika eneo la Maisara majira ya
saa 3:45 usiku.
Alisema lengo la majambazi hayo ni
kumshambulia na kumpora fedha lakini hata hivyo hawakufanikiwa.
Alisema wakati akiwa Maisara
majambazi hao walimzingira kwa mbele kwa kutumia gari aina ya Scudo na baada ya yeye kusimama majambazi manne
yalishuka kwenye gari wakiwa na mapanga kwa lengo la kumshambulia.
“Kabla ya kushuka kwenye gari lao
sikufahamu kuwa walikuwa majambazi, lakini baadae niligundua kuwa hawakuwa watu
wema. Nilifanya maamuzi ya haraka ya kuliendesha gari langu kwa kasi kupitia
kwenye mvinje na nikakimbia kituo cha polisi Madema,” alisema.
Alisema baada ya kuwakimbia
majambazi hayo, alikimbilia polisi kuomba msaada wa polisi ambao walimuongoza
hadi nyumbani kwake.
Hilo si tukio la kwanza kwa
majambazi kuvamia maduka ya kuuzia dawa.
Katika tukio jengine la hivi
karibuni majambazi hayo yalivamia duka la dawa la Mwembeladu.
Katika tukio lilitokea mwezi wa Desemba mwaka 2012, majambazi yaliyokuwa na silaha yalivamia duka
la dawa liliopo karibu na hospitali kuu ya Mnazimmoja na kufanikiwa kuiba
kopyuta na mamilioni ya fedha.
Aidha katika tukio jengine
lililotokea mwaka 2012, majambazi yalivamia dula la dawa la Karibu Pharmacy na kumuua mlinzi wa duka hilo na
kupora mamilioni ya fedha.
Kamanda Polisi wa Mkoa wa Mjini
Magharibi, ACP, Azizi Juma Mohamed alikiri kupokea taarifa za mfanyabiashara
huyo kuvamiwa na majambazi.
Alisema mfanyabiashara huyo baada
ya kufanikiwa kuwakwepa wahalifu hao alikimbilia kituo cha polisi ambapo
alipatiwa ulinzi hadi nyumbani kwake.
Aliwataka wananchi na
wafanyabiashara kuwa makini na
waangalifu wanaposafirisha fedha pamoja na kuomba msaada wa kusindikizwa na
polisi wanapokuwa na kiwango kikubwa cha fedha.
Aidha aliwataka kutoa taarifa
mapema iwapo wataona vitendo wanavyovitilia mashaka.
"Huduma ya kuwapa ulinzi wafanyabiashara
inatolewa bure lakini sijui kwani wanakuwa wasiri kulitumia jeshi la polisi
kuwapa ulinzi,” alisema.
faida za muungano hizo):
ReplyDeleteWizi ulikuwepo kabla ya muungano.
ReplyDelete