WATANZANIA wanastahili sifa kwa kufanikisha
kwa kiasi kikubwa kuandaa mchakato wa maoni ya katiba mpya bila ya kuzuka
migogoro ambayo ingeliweza kuleta uvunjifu wa amani.
Spika wa Baraza la Wawakilishi,
Pandu Ameir Kificho, aliyasema hayo jana wakati akizindua kitabu cha elimu ya katiba
kwa wananchi wa Zanzibar , kilichoandaliwa na Baraza la Wawakilishi, kituo cha
huduma ya sheria Zanzibar na Ubalozi wa Norway.
Spika Kificho alisema, mchakato wa mabadiliko
ya katiba ya nchi umekuwa ukitekelezwa na nchi mbali mbali duniani lakini
humalizia kwa migogoro mikubwa ya kuhatarisha amani.
Alisema hali hiyo inawezekana imetokana
na mchakato huo kuasisiwa na wanachi wenyewe kwa kuiomba serikali yao kuandaa
katiba mpya jambo ambalo lilikubaliwa.
Alisema kwa vile Baraza la wawakilishi
ni chombo kinachosimamia wananchi kimeona haja ya kusaidia mchakato huo kwa
kuwapatia elimu ya katiba waananchi ili waweze kutoa maoni yao.
Alisema kitabu hicho ni muhimu kwani kitaweza
kuwafanya wananchi kuyaelewa maeneo muhimu ya kuyafanyia kazi ili kuifanya
Tanzania kupata katiba bora.
Aliupongeza Ubalozi wa Norway
nchini Tanzania na kituo cha huduma cha sheria kwa kufanikisha kupatikana kwa
kitabu hicho amabapo aliahidi baraza hilo kuendeleza ushirikaino na taasisi
hizo.
Nae Balozi wa Norway nchini
Tanzania , Ingunn Klepsvik, alisema suala la madailiko ya katiba nchini
Tanzania ni moja ya jambo la msingi na elimu ndio njia pekee itakayowawezesha
Watanzania kuwa na katiba bora.
Mapema Mwenyekiti wa Bodi ya
Wadhamini ya kituo cha huduma cha Sheria Zanzibar, Profesa Criss Peter Maina,
alisema kituo hicho kimeweza kupata mafanikio mbali mbali ya utoaji elimu ya
sheria katika majimbo 50 ya Unguja na Pemba.
Katibu wa Baraza la Wawakilishi,
Yahya Hamad, akitoa shukrani zake alisema kufanikiwa kwa mradi huo kwa kiasi
kikubwa utaweza kuwasaidia wajumbe wa baraza hilo pamoja na wananchi wa
Zanzibar .
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na
Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Iddi, mabalozi waliopo Zanzibar na watendaji wa serikali wakiwemo mawaziri na
watendaji wa baraza la wawakilishi.
No comments:
Post a Comment