Na
Mwantanga Ame
KAIMU Waziri wa Habari, Utamaduni,
Utalii na Michezo, Abdilah Jihadi Hassan, amesema mswada wa sheria ya
uanzishwaji shirika la utangazaji Zanzibar (ZBC), utaifanya Zanzibar kufuata
mfumo wa kimataifa katika kutoa matangazo yake.
Hayo aliyasema jana wakati
akiwasilisha mswada huo mbele ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika kikao
kinachoendelea Chukwani nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Waziri huyo ambaye pia ni Waziri wa Uvuvi, alisema
mengi ya mashirika ya kimataifa yanafanya kazi zake kwa ufanisi kwa lengo la kuyaweka katika mfumo ya kimataifa
inayotumika sasa katika baadhi ya nchi.
Alisema mswada huo utawezesha
kupunguza gharama za uendeshaji katika vyombo vya habari vya serikali na
italeta ufanisi kwa wasikilizaji wa
redio na televisheni.
Alisema mfumo wa sasa wa dunia
umekuwa ukiendesha vyombo vya habari kwa mtindo wa mashirika kama lilivyo la
BBC, Xinhua, Reuters na CNN ambayo yameonekana kujiendesha kwa faida na ufanisi
katika mfumo wa utangazaji.
Alisema kuja kwa sheria hiyo,
kutaweza kulifanya ZBC, kuwa na mfumo wa kisasa unaokubalika kimataifa.
Alisema pia mswada huo utasaidia
kuweka mazingira mazuri ya kazi kwa watumishi wa shirika hilo ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kuwa na vifaa vya kisasa
na kuimarisha uongozi wa shirika hilo.
Kamati ya Mifugo, Utalii,
Uwezeshaji na Habari ya Baraza la Wawakilishi, imesema kwamba mswada huo utalifanya shirika hilo kuwa bora zaidi
katika matangazo yake ikiwa ni pamoja na kujiendesha kibiashara na kiushindani
na utoaji huduma bora kwa kuangalia rika.
Mjumbe wa kamati hiyo, Salim Abdalla Hamad,
akisoma maelezo ya kamati, alisema kwa vile mswada huo umezingatia mambo mengi
yatakayoliwezesha shirika hilo kuwa na mabadiliko ni vyema kwa viongozi na
watendaji wakafanya kazi kwa ufanisi.
Alisema kazi kubwa ambayo itahitajika kufanywa
na shirika hilo ni kuzingatia suala la utafiti wa habari zake na uwakilishi wa
wananchi wa mjini na vijijini.
Nae Mwakilishi wa Mtambile,
Mohammed Haji Khalid, akitoa maoni yake juu ya mswada huo aliomba shirika hilo
kuwa makini katika kufanya kazi zake hasa taarifa na vipindi ili visivunje maadili
ya Mzanzibari.
Nae Mwakilishi wa Matemwe, Abdi
Mosi, alisema ni vyema wakati shirika hilo likiimarishwa suala kubwa la
kuangaliwa ni namna ya kuwa na vipindi bora vitakavyoweza kutoa elimu ya
kilimo, ustawi wa jamii na uimarishaji utamaduni.
Mwakilishi wa viti vya wanawake
ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati hiyo, Asha Bakari Makame, alisema ipo haja
kwa shirika hilo likapewa vitendea kazi zaidi kwa sababu vilivyopo sasa
haviendani na hadhi ya shirika.
No comments:
Post a Comment