Na Hassan Hamad, OMKR
JUMUIYA ya Jumaa Al-Majid Foundation ya Dubai imesema iko
tayari kushirikiana na Zanzibar katika utunzaji nyaraka na kumbukumbu ili
kuzihifadhi katika mfumo wa kisasa.
Mkuu wa taaluma na mambo ya nje wa Jumuiya hiyo, Dk.
Azzeddine Benzeghiba alieleza hayo alipokuwa na mazungumzo na Makamu wa Kwanza
wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ofisini kwake Migombani.
Dk. Azzeddine alisema nyaraka ni kitu muhimu cha kukienzi
katika kutunza historia ya nchi, hivyo taasisi hiyo itashirikiana kwa karibu na
Zanzibar katika kuhakikisha inasaidia kutunza nyaraka na historia yake.
Jumuiya hiyo pia imeonesha mwelekeo wa kushirikiana na
taasisi za elimu nchini zikiwemo skuli za sekondari, vyuo vikuu, maktaba na
taasisi binafsi za elimu.
Nae Maalim Seif Sharif Hamad alisema kuna haja kubwa ya
kuzihifadhi nyaraka katika mfumo wa kisasa ili kutunza historia ya Zanzibar.
Alisema hali ya utunzanji na uhifadhi wa nyaraka kwa sasa
sio ya kuridhisha, hivyo ipo haja ya kushirikiana na taasisi hiyo katika
kutunza nyaraka na kumbukumbu za taifa.
Kuhusu elimu, Maalim Seif alisema Zanzibar imepata
mafanikio makubwa katika miaka ya hivi karibuni kwa kufanikiwa kuwepo kwa vyuo
vikuu vitatu kikiwemo Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), pamoja na
kuwasajili watoto wote wenye sifa ya kuanza skuli.
Kwa upande mwengine Maalim Seif alisema Zanzibar
inaendelea kuwakaribisha wawekezaji kutoka maeneo mbali mbali kuja kuwekeza
hasa katika sekta ya utalii ambayo imekuwa ikiimarika kila mwaka.
Alisema miundombinu ya uwekezaji katika sekta hiyo
imeimarika baada ya kuwepo kwa usafiri wa moja kwa moja kutoka Oman hadi
Zanzibar, na kwamba serikali inaangalia uwezekano wa kuwepo usafiri zaidi wa
moja kwa moja utakaoziunganisha nchi za kigeni na Zanzibar.
Alisema tayari serikali imefanya mazungumzo na makampuni
mbali mbali ya ndege yakiwemo ya Uturuki, Emirates na Anatalia la Italia, ili
kuweza kuleta ndege zao moja kwa moja, na kwamba yameonesha mwelekeo mzuri.
No comments:
Post a Comment