Habari za Punde

JK akemea rushwa polisi



Na Mwandishi wetu, Dodoma
RAIS Jakaya Kikwete ameliagiza jeshi la polisi kupambana na utovu wa maadili ili lipunguze kunyooshewa vidole  kuhusu tuhuma za rushwa na kasi ndogo ya upelelezi wa makosa.
Rais Kikwete aliyasema hayo jana  wakati wa akifungua mkutano mkuu wa maofisa waandamizi wa jeshi la polisi katika ukumbi wa Bunge, Dodoma
 “Suala la rushwa nimekuwa nikilikemea mara kwa mara lakini lakini kutokana na umuhimu wake leo narudia tena kulisema,” alisema Rais Kikwete.
Alisema tuhuma za rushwa zinachafua sifa nzuri ya jeshi la polisi ingawa alisema sio wote  wanaojihusisha na vitendo vya kuomba na kupokea rushwa.
“Jeshi lina maofisa na askari wengi ambao ni waadilifu na wachapa kazi wenye uzalendo wa kweli kwa nchi yetu. Lakini waswahili wana msemo usemao: “nazi mbovu harubu ya nzima”.
Alisema askari wachache wasiokuwa waadilifu wanaweza kuharibu sifa ya wengi walio wazuri. 

Aidha amelitaka jeshi la polisi kuweka utaratibu mzuri wa kupokea na kushughulikia maoni na malalamiko ya wananchi na kutaka wale watakaobainika kupokea rushwa wasionewe aibu.
Aidha alisema pamoja na vitendo vya kuomba na kupokea rushwa, jeshi la polisi linalalamikiwa na wananchi kwa kuendesha upelelezi wa kesi za jinai kwa kasi ndogo hali inayosababisha kesi zilizoko mahakamani kuchukua muda mrefu kumalizika kuliko inavyostahili. 
“Mimi nilidhani tulipotenganisha shughuli za upelelezi na uendesha mashtaka ingesaidia lakini inaelekea bado.  Nawasihi maafisa, wakaguzi na askari waliopangiwa kufanya kazi za upelelezi kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi na kasi inayokubalika kisheria.  Mkifanya hivyo mtasaidia kupunguza moja ya kero kubwa na ya muda mrefu ya msongamano wa mahabusu magerezani,” alisema.
Aliwataka polisi kuendelea kuwashirikisha wananchi kwa karibu katika kupambana na uhalifu, akisema hilo ndio jawabu sahihi la uhaba wa polisi nchini.
Rais Kikwete alieleza jinsi alivyovutiwa na kauli mbiu ya mkutano huo inayosema ‘Tujenge Uwezo wa Jamii na Polisi Kukabiliana na Vurugu, kwa kuimarisha utii wa sheria bila shuruti.”

Alisema kauli mbiu hiyo imebeba ujumbe muafaka katika mazingira yaliyopo sasa nchini.

Alisema hivi sasa matukio ya vurugu yanaanza kuwa taarifa za kawaida na kuongeza kuwa kila kukicha au kila baada ya muda mfupi kuna tukio la vurugu kutokana na sababu mbalimbali. 

Alisema kauli mbiu hiyo, inakumbusha ukweli huo na umuhimu wa jamii na polisi kushirikiana katika kukabiliana na vurugu nchini. 

Aidha alisema inasisitiza nafasi ya utii wa sheria bila shuruti katika kuzuia vurugu zisitokee au pale zinapotokea ziweze kumalizwa haraka bila ya madhara makubwa kwa pande husika. 

“Mimi naamini kama shabaha za kauli mbiu hii zitatimia, vurugu hazitakuwepo nchini na Tanzania patakuwa mahali salama kuishi kwa kila mtu,” alisema. 

Alisema vurugu ni changamoto mpya ya usalama wa raia, mali zao na nchi ambayo polisi hawana  budi kukabiliana nayo. 

Alisema polisi hawanabudi kukaa kitako na kutafakari kwa makini kiini cha vurugu na jinsi ya kukabiliana nazo kwa maana ya kuzuia zisitokee na zinapotokea zinamalizwa haraka bila ya kuwa na athari kubwa au kupunguza madhara kwa watakaoathirika. 

Alisema kila mdau anatakiwa kuutambua wajibu huo na kuhakikisha kuwa anatimiza ipasavyo yale yanayomhusu. 

“Nyinyi katika jeshi la polisi mnajua vyema wajibu wenu katika kudhibiti vurugu.  Bahati nzuri wajibu huo umetamkwa kisheria na una miongozo yake ambayo imeandikwa na hufundishwa katika vyuo na hufanyiwa mazoezi vikosini.Nawaomba suala la kuzuia na kudhibiti vurugu mlipe kipaumbele cha juu,” alisema.

Alisema siku za nyuma haikuwa lazima kufanya hivyo kwa sababu halikuwa tatizo kubwa lakini siku hizi hali imebadilika.

Alisema vurugu zinakuwa nyingi na za aina nyingi hivyo kugeuka kuwa shughuli kubwa kwa jeshi la polisi.

“Vurugu  zinasababishwa na mambo mengi, zipo zinazosababishwa na vyama vya siasa kwa kufanya mikutano na maandamano yasiyoruhusiwa.  Wakati mwingine hata pale yaliporuhusiwa wahusika hufanya mambo yasiyohusika ama wakati au baada ya mkutano,” alisema.

Lakini alisema zipo pia vurugu zinazosababishwa na kauli na vitendo vya baadhi ya viongozi wa dini na waumini wao akitolea mfano wa vurugu za hivi karibuni zilizotokea Buseresere, Geita.

“Hatukuwa na  hali tuliyonayo sasa ya watu kutumia njia ya vurugu kuelezea hisia zao au kujaribu kutatua matatizo yanayowakabili.  Maadam sasa yameanza kujitokeza kwa nguvu hatunabudi kukabiliana kisawasawa na aina hii ya uhalifu.
 Hatunabudi kujifunza namna bora ya kukabiliana na vurugu. Hatuwezi kusema yatapita, lazima tukubali ukweli kuwa matukio haya yanaweza kuendelea kuwepo na hata kuongezeka siku za usoni,” alitahadharisha.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.