Habari za Punde

KUJIUZULU PAPA Kanisa njia panda


VATICAN, Italia
BAADA ya uamuzi wa Papa Benedict wa XVI kujiuzulu, kanisa Katoliki limejikuta katika hali ambayo halijawahi kuwemo kwa kipindi cha takribani miaka 700, swali kubwa sasa ni nini kinachofuata.

Ni washauri wachache tu walio karibu na Papa, ambao walijua mpango wake wa kujiuzulu kabla ya kutangazwa hadharani.

Hata vigogo katika uongozi wa Vatican walistushwa na uamuzi wa Papa kujiuzulu.

Kadinali Angelo Sodano alisema uamuzi huo ulikuwa kama radi katika anga lisilo na mawingu.

Naye Kadinali Paul Poupard wa Ufaransa alisema neno la kwanza katika risala ya Papa liliashiria kitu kisichokuwa cha kawaida, na alipoangalia watu waliokuwa karibu naye, aliona nyuso zilizoduwaa kwa mshangao.


Maoni mchanganyiko

 Kuna maoni mchanganyiko miongoni mwa waumini
wa kanisa katoliki wapatao bilioni 1.1 kote duniani.

Kuna wale ambao walisema uamuzi wake ni wa kishujaa, na utaleta nguvu mpya katika kanisa hilo linalokabiliwa na migogoro, na pengine kumaliza mtindo wa kuwachagua wakongwe kuliongoza kanisa hilo.

Lakini pia wako wale ambao wamebaki na maswali yasio na majibu, wakishindwa kuelewa namna mtu mwenye wadhifa ambao unatajwa kupatikana kwa mwongozo wa roho mtakatifu, anavyoweza kufanya uamuzi wa kujiuzulu.

Ni vigumu kutabiri mrithi

 Tetesi zimeanza kuhusu nani atachaguliwa kuwa Papa mpya, mwengine wakisema kuwa huenda Papa mpya akatoka Nigeria au Ghana.

 Swali kubwa ni nini kanisa katoliki litakifanya kuanzia tangazo la Papa lilipotolewa, hadi tarehe ya kujiuzulu rasmi ambayo ni 28 Februari.

Mwandishi wa siku nyingi wa shirika la habari la kikatoliki, KNA, Ludwig Ring-Eifel, alisema hakuna anayeweza kulijibu swali hilo kikamilifu.

''Hatuelewi kila kitu kitakachofanyika, tunachojua ni kwamba tarehe 27 Papa atapata nafasi ya kuwaaga waumini mbele ya hadhara kubwa mjini Roma. Baada ya hapo mchakato wa kumtafuta mrithi wake utaanza, kupitia utaratibu ule ule unaotumika ikiwa Papa amekufa. Maana yake, nafasi ijulikanayo kama kiti cha Petro itakuwa wazi, na kanisa litakuwa na siku kati ya 15 na 20 kumchagua Papa mwingine.''

Ama kutoka kwa viongozi wa dunia, maoni yamekuwa kuheshimu uamuzi wa Papa na kushukuru mchango wake katika kutafuta maelewano ya kimadhehebu.

Muda mfupi, changamoto nyingi

Miaka 8 aliyoushikilia wadhifa wa Papa ni moja ya vipindi vifupi katika historia ya wadhifa huo.

Hata hivyo, kipindi hicho kilitosha kumpatia Papa Benedict maadui wengi, wakiwemo mashoga na wanaharakati wa kupambana na ugonjwa wa UKIMWI.

Katika kipindi hicho pia kashfa nyingi za visa vya mapadre kuwanajisi watoto zilifichuliwa.

Uvumi kuhusu nani anaweza kuchaguliwa kuwa Papa mpya ulianza mara tu baada ya Papa anayeondoka kutangaza uamuzi wake.

 Lakini, hata wale wenye uzoefu mkubwa katika masuala ya Vatican, wametoa tahadhari kwamba si rahisi kutabiri nani atachaguliwa.

Vatican imesema inatarajia kuwa Papa mpya atajulikana kabla ya siku kuu ya Pasaka, ambayo ni tarehe 31 mwezi Machi, ingawa kila kitu kitategemea mkutano wa faragha wa makardinali.

3 comments:

  1. ameshashtuka mapema anaona ni bora kung'atuka kuliko kung'ang'ania mfupa uliomshinda fisi karibu home papaaaaa

    ReplyDelete
  2. Huwenda ameuwona ukweli uko wapi ndio maana anajiuzulu, anaogopa siku ya siku kila mmoja atajijutia!! ikiwa kenda na amali mbaya!!

    ReplyDelete
  3. mmhhh!!!!!!!!!!!!! mambo ya dunia anayaweza yule mwenye nguvu na muumba wa mbingu na ardhi na vilivyomo...*****

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.