Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif akiwa na ujumbe wa Kamati ya Bajeti ya Bunge la Ujerumani ofisini kwake Migombani
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Kamati ya Bajeti ya Bunge la Ujerumani baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika ofisini kwake Migombani
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif akizungumza na Balozi wa Cuba nchini Tanzania balozi Jorge Luis Tormo ofisini kwake Migombani.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif akisalimiana na Balozi wa Cuba nchini Tanzania balozi Jorge Luis Tormo ofisini kwake Migombani.
Na Hassan Hamad OMKR
Ujumbe wa Kamati ya Bunge la Ujerumani umeelezea kuridhishwa kwake na matumizi mazuri ya misaada wanayoitoa katika hatua za kusaidia miradi ya maendeleo nchini.
Kiongozi wa Ujumbe huo Bw. Clouse Peter Willsch ameeleza hayo alipokuwa na mazungumzo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ofisini kwake Migombani.
Ujumbe huo ambao upo nchini kwa ajili ya kukagua miradi inayofadhiliwa na serikali ya Ujerumani katika maeneo ya jeshi, umepata fursa ya kutembelea hospitali ya Lugalo jijini Dar es Salaam na hospitali ya Bububu iliyopo Zanzibar, na kuelezea kufarajika kwake na matumizi ya misaada hiyo.
Bw. Clouse amesema Ujerumani itaendelea kushirikiana na Zanzibar katika maeneo mbali mbali na kusaidia juhudi za serikali katika kubabiliana na maafa.
Ameahidi kuziangalia kwa karibu fursa za uwekezaji zilizopo Zanzibar ikiwa ni pamoja na sekta ya utalii na viwanda vidogo vidogo, ili kuona namna ya nchi hiyo kuweza kuwekeza katika maeneo hayo.
Mapema Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ameueleza ujumbe huo kuwa Zanzibar ni mahali salama pa kuwekeza, na kwamba zipo fursa nyingi na mazingira salama kwa ajili ya uwekezaji.
Ameelezea matumaini yake kuwa ujio wa ujumbe huo wa Kamati ya Bajeti ya Bunge la Ujerumani utasaidia kuitangaza Zanzibar pamoja na kuimarisha uhusiano baina ya Zanzibar na Ujerumani.
Amesifu mchango wa Ujerumani kwa Zanzibar ambapo imekuwa ikisaidia harakati za maendeleo katika sekta mbali mbali ikiwa ni pamoja na uimarishaji wa hospitali ya Bububu ambayo iko chini ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania.
Wakati huo huo Maalim Seif amekutana na Balozi wa Cuba nchini Tanzania balozi Jorge Luis Tormo, na kuelezea matumaini yake juu ya kuendelea kwa mashirikiano katika sekta za biashara na kilimo.
Amesema Zanzibar na Cuba zinaweza kushirikiana katika maeneo hayo kutokana na nchi hiyo kuwa na uzoufu mkubwa katika masuala hayo, na kwamba kufanya hivyo kutaongeza maeneo mapya ya ushirikiano baina ya nchi mbili hizi.
Cuba imekuwa ikishirikiana na Zanzibar kwa kipidi kirefu hasa katika sekta ya afya ambapo imekuwa ikituma wataalamu wake nchini pamoja na kuanzisha chuo kwa ajili ya kuwafundisha madaktari wa Zanzibar.
Maalim Seif ameiomba Cuba kuangalia uwezekano wa kusaidia matibabu kwa ajili ya wananchi wa Zanzibar nchini Cuba, ili kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopelekwa nchini India kwa ajili ya matibabu.
Nae Balozi Luis Tormo amesema yapo maeneo mengi ambayo Cuba inaweza kushirikiana na Zanzibar, na kuahidi kupeleka mapendekezo yake nchi Cuba ili waweze kuyafanyia kazi.
Amesema kuna umuhimu wa kipekee wa kuendeleza mashirikiano katika maeneo mengine ya kiuchumi, hatua ambayo itakuza mashirikiano baina ya Cuba na Zanzibar
No comments:
Post a Comment