Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Uongozi wa Kamati ya Bajeti ya Bunge la Shirikisho la Ujerumani unaofanya ziara ya siku sita Nchini Tanzania Kuangalia miradi iliyofadhiliwa na Nchi hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa katika Picha ya pamoja na Ujumbe wa Kamati ya Bajeti ya Bunge la Shirikisho la Ujerumani mbele ya lango la Ofisi yake iliyopo Vuga mara baada ya mazungumzo yao.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ
Na Othman Khamis Ame, OMPR
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuthamini jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa Cuba katika kusaidia uimarishaji wa huduma za afya hapa Zanzibar.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati wa mazungumzo yake na Balozi Mpya wa Jamuhuri ya Watu wa Cuba Nchini Tanzania Bwana Jorge Luis Lopez Tormo hapo nyumbani kwake Mazizini Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Balozi Seif alisema Wananchi walio wengi hapa Zanzibar wamekuwa akielezea faraja yao kutokana na huduma mbali mbali wanazozipata kutoka kwa Wataalamu na Madakari bingwa wa Cuba waliopo hapa Nchini.
Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar alimuhakikishia Balozi Lopez Tormo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwajengea mazingira bora ya makaazi Wataalamu na madaktari hao ili watekeleze vyema jukumu lao.
Balozi Seif alifahamisha kwamba ipo haja kwa uhusiano wa Kihistoria uliopo kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Jamuhuri ya Watu wa Cuba ukaendelezwa zaidi kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliishauri Cuba kuangalia uwezekano wa taasisi na makampuni yake ya Kitalii nchini humo kutumia fursa liyotolewa na Zanzibar katika uwekezaji vitega uchumi kwenye Sekta ya Utalii.
Alisema Cuba imepiga hatua kubwa ya maendeleo katika uwekezaji ndani ya sekta ya Utalii na kuipatia mapato makubwa, hivyo ni vyema kwa Nchi hiyo kuangalia jinsi inavyoweza kutanua wigo wake hadi Zanzibar.
Naye Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa Cuba Nchini Tanzania Bwana Jorge Luis Lopez Tormo ameelezea kuridhika kwake na huduma bora wanazopatiwa Wataalamu na Madaktari Bingwa wa Nchi yake wanaofanya Kazi hapa Zanzibar.
“ Nimepata fursa ya kutembelea makaazi ya Wataalamu na Madaktari Bingwa wa Nchi yangu na kuridhika na mazingira mazuri waliyowekewa na Serikali ambayo sina budi kuipongeza SMZ kwa hatua hii niliyoishuhudia”. Alifafanua Balozi huyo mpya wa Cuba Nchini Tanzania.
Balozi Lopez Tormo ambae aliwahi kushika wadhifa huo Nchini Botswana alimuahidi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba uhusiano kati ya pande hizo mbili utaimarishwa na kuendelezwa zaidi.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alionana na Kamati ya Bajeti ya Bunge la Ujerumani ikiongozwa na Mheshimiwa Claude Peter Willsch hapo Ofisini kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.
Ujumbe huo wa Viongozi kumi wa Kamati ya Bajet ya Ujerumani upo Nchini Tanzania kwa ziara ya siku sita kuangalia miradi mbali mbali ya maendeleo, Kijamii na Uchumi iliyopo Nchini ambayo imefadhiliwa na Serikali ya Shirikisho la Ujerumani.
Katika mazungumzo yao Kiongozi wa Ujumbe Huo Bwana Claude Peter Willsch alieleza kwamba Nchi imejipanga kutumia Euro Milioni 4,000,000 kusaidia miradi minane iliyojipangia kuitekeleza Nchini Tanzania katika kipindi kijacho.
Bwana Claude aliutaja mradi uliotekelezwa na Ujerumani hapa Zanzibar wa Hospitali ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania { JWTZ } uliopo Bububu ambao unaongezewa vifaa vya umeme unaotumia jua utakaosaidia hospitali hiyo kufanya kazi muda wote.
“ Tumeona ipo haja kwa Hospitali hiyo kuwa na umeme wa Solar utakaokidhi mahitaji ya operesheni wakati wote endepo umeme wa kawaida utazimwa au kuwa na hitilafu ya kiufundi”. Alifafanua Bw. Claude Peter.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliueleza Ujumbe huo kwamba Hospitali ya Jeshi iliyopo Bububu imekuwa mkombozi mkubwa kwa wananachi wa Zanzibar katika kujipatia huduma za Afya.
Alisema mradi huo mbali ya kuiongezea nguvu Hospitaki kuu ya Mnazi Mmoja lakini pia unakwenda sambamba na ile azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuwa na sehemu za huduma za afya kila baada ya kilo mita tano.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliishauri Serikali ya Shirikisho la Ujerumani kupitia Ujumbe huo katika mipango yake ya baadaye kufikiria kuwa na mradi mwengine wa Kijamii Kisiwani Pemba.
No comments:
Post a Comment