Na Hasssan Hamad OMKR
Maelfu ya wananchi wakiongozwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, wamejumuika katika mazishi ya Mbunge wa Zamani wa jimbo la Ziwani (CUF), marehemu Hashul Nassor.
Marehemu Hashul ambaye pia ni mwalimu wa siku nyingi katika visiwa vya Zanzibar, amefariki dunia katika hospitali ya Mnazimmoja na kuzikwa katika makaburi ya Nyamanzi Wilaya ya Magharibi Unguja.
Akizungumza katika mazishi hayo, Mkurugenzi wa Habari na Haki za Binadamu wa CUF Bw. Salim Bimani amesema marehemu Hashul ametoa mchango mkubwa katika chama hicho na taifa kwa jumla.
Amefahamisha kuwa marehemu Hashul ni miongoni mwa waanzilishi wa CUF na siasa za vyama vingi Tanzania, na aliwahi kuwa Mbunge wa Ziwani kupitia CUF katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995 hadi 2000.
Hadi kufariki kwake marehemu alikuwa mtendaji wa CUF na afisa mafunzo ndani ya chama hicho.
Pia amewahi kuwa mwalimu wa siku nyingi wa masomo ya sayansi na alifundisha skuli mbali mbali za Unguja na Pemba ikiwemo Skuli ya Sekondari ya Fidel-Castro.
Bimani alisema CUF kimempoteza mtu muhimu ndani ya chama hicho ambaye alikuwa akitoa mchango mkubwa hasa katika masuala ya taaluma.
Marehemu Hashul alifariki dunia jana alfajiri (04/02/2013) katika hospitali kuu ya Mnazi mmoja baada ya kusumbuliwa na matatizo ya moyo.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi (Ammin).
No comments:
Post a Comment