Habari za Punde

Makachero watumwa kuchunguza mauaji ya Padri Mushi.·

Watatu mbaroni, Z’bar yazizima. 
JK awaagiza polisi kuzishirikisha nchi rafiki kuchunguza

Na waandishi wetu Zanzibar, DSM
MKUU wa jeshi la Polisi nchini IGP, Said Mwema amesema timu ya makachero  waliobobea katika masuala ya kukusanya taarifa na kiintelejesia wametumwa Zanzibar kuchunguza tukio la mauaji ya Padrid, Evaristitus Mushi wa kanisa katoliki Parokia ya Mtakatifu Joseph, Shangani yaliyofanywa na watu wasiojulikana jana asubuhi katika eneo la Beit El Ras mjini Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam  kufuatia mauaji hayo, IGP Mwema alisema tayari watu watatu wanashikiliwa na polisi wakihusishwa na mauaji  hayo.

Alisema polisi itawakamata na kuwachukulia hatua kali watu wote waliohusika na mauaji hayo pamoja na wengine wanaochochea, kufadhili, kushiriki na kushawishi vitendo vya kihalifu.

IGP Mwama alilaani mauaji ya Padri huyo na kusema jeshi litawasaka na kuwakamata wauaji hao.
Aidha alisema polisi imeanza kuwatia mbaroni watu wote wanaoonekana kutoa kauli za uchochochezi kwa mahojiano.

Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amelaani mauaji hayo na kusema serikali haiwezi kukubali kuona kikundi cha watu kinavuruga amani na utulivu uliopo  na kuingiza nchi katika mgogoro wa kidini.

Aidha ameliagiza jeshi la polisi kushirikiana na vyombo vyengine vya ulinzi na usalama vya ndani na nchi jirani kufanya uchunguzi wa kina kuhusu mauaji ya viongozi wa dini na matukio mengine yanayotishia uvunjifu wa amani.



Akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya polisi Kilimani, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dk. Emmanuel Nchimbi aliyaita mauaji ya Padri huyo kuwa ya kigaidi.

Alisisitiza kuwa jeshi la polisi litafanya kila liwezekanalo kuwatia mbaroni  wauaji na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.

Aidha alisema serikali imeshatoa ruhusa kwa jeshi la polisi kushirikiana na vyombo vyengine vya usalama kutoka nje ya nchi kuchunguza chanzo cha mauaji hayo pamoja na kuwatia nguvuni wahusika.

Alisema mauaji hayo yana nia ya kuwachonganisha Watanzania kidini, lakini aliwataka Watanzania kuendelea kuwa wamoja na kuimarisha misingi ya upendo, amani na utulivu uliopo.

Alisema mazingira ya muaji ya Padri Mushi yanalingana na tukio la kujeruhiwa kwa risasi  Padri Ambros Mkenda, tukio ambalo lilitokea Disemba mwaka uliopita.

Aidha alisema silaha iliyotumika kumshambulia Padri Mushi ndio ile ile iliyotumika kumjeruhi Padri Mkenda.

Kwa upande wake serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za mauaji ya Padri huyo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud  ameliagiza jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa kina ili kuwatambua wale wote waliohusika na mauaji hayo.

Amewaomba wananchi kuendea kutulia na kuliacha jeshi la polisi kutekeleza wajibu wake.

Pia alisema serikali inatoa mkono wa pole kwa familia wa marehemu pamoja waumini  na kuwataka kuwa wastahamilivu  katika kipindi hichi kigumu.

Kwa upande wake, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema Padri Mushi,alipigwa risasi akiwa ndani ya gari na kujeruhiwa vibaya sehemu za kichwa na kifua.

Alisema  baada ya tukio hilo baadhi ya waumini wa kanisa hilo waliofika katika kanisa hilo  kwa ajili ya ibada, walimpeleka Padri Mushi katika hospitali kuu ya Mnazimmoja kwa matibabu  na alifariki  muda mfupi baadae.

“Kutokana na uzito wa tukio hili jeshi la polisi Zanzibar linaendelea na upelelezi wa kina kuhakikisha wahusika wote wanafikishwa katika vyombo vya kisheria,“ alisema.  

“Natoa wito kwa wananchi washirikiane na maafisa wetu juu ya taarifa zozote zinazohusiana na tukio hili ili tuweze kutekeleza majukumu yetu kwa wakati,” alisisitiza. 

Kamanda wa polisi mkoa wa Mjini Magharibi,ACP Aziz Mohamed alisema kwa sasa jeshi la polisi linaendelea na doria katika maeneo mbalimbali ya mjini ili kuhakikisha wale wote waliohusika katika mauaji ya Padri huyo wanakamatwa.  

Naye Mkuu wa Mkoa Mjini Magharib, Abdallah Mwinyi alifika katika hospitali ya Mnazimoja kuwafariji jamaa,ndugu na waumini wa dini hiyo waliofika katika eneo hilo kwa ajili ya kufuatilia hatima ya kiongozi wao.  

Akizungumzia tukio hilo,msemaji wa kanisa hilo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Kanisa Katoliki,jimbo la Zanzibar, Padri Cosmas Shayo aliwataka waumini wa kanisa hilo,kuwa wavumilivu katika kipindi hichi hadi suala hilo litakapopatiwa ufumbuzi.  

Alisema uongozi wa kanisa hilo,umepokea mauaji hayo kwa masikitiko makubwa na pia kufariki kwa Padri huyo ni miongoni mwa pigo kubwa kwa waumini na kanisa kwa ujumla.

Alisema kanisa linathamini mchango mkubwa uliotolewa na marehemu wakati wa uhai wake,katika kuliendeleza kanisa kwenye huduma za kiimani na kiroho kwa waumini wa kanisa.  

Baadhi ya mashuhuda ,waliozungumza kwa nyakati tofauti katika eneo la tukio, walisema kwamba wakati waumini wa kanisa hilo wakijiandaa kwa ibada,pembeni mwa kanisa hilo kulikuwa na watu watatu ambao hawajulikani na mara baada ya kufika Padri huyo walisikia milio ya risasi na baadae watu wawili wakaondoka kwa kutumia vespa mwengine akakimbilia vichochoroni.

Kufuatia mauaji hayo hali ya mji wa Zanzibar umekuwa kimya kwa muda mrefu huku askari polisi wenye silaha wakionekana kuranda randa kila kona ya barabara za mji huo kuimarisha doria huku wananchi wakiwa wamejikusanya makundi kuzungumzia mauaji ya Padri huyo.

Hilo ni tukio la tatu kwa viongozi wa dini kushambuliwa visiwani Zanzibar, ambapo katika tukio la kwanza Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Suleiman Soraga alishambuliwa kwa kumwagiwa tindi kali mwezi Septemba wakati akifanya mazoezi.

Habari hii imeandaliwa na Khamis Amani, Husna Shehe na mwandishi wetu, DSM

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.