VATICAN, Italia
MAELFU ya watu
walikusanyika katika uwanja wa kanisa la mtakatifu Petro jana kuhudhuria tukio
la mwisho la Papa Benedict wa XVI la kuwaombea waumini hadharani.
Hiyo ilikuwa ibada ya mwisho ya Papa kabla ya kuachia
kabisa nafasi hiyo ya kuliongoza kanisa katoliki duniani.
Kimsingi misa hiyo ya mchana ya Jumapili huwavutia watu
wachache ikiwa ni pamoja na watalii lakini mara hii wamejitokeza maelfu kwa
maelfu ya waumini katika uwanja huo kumshuhudia kwa mara yao ya mwisho Papa
Benedict.
Inasaidikiwa kwamba watu 150,000 walihudhuria misa hiyo
ya wazi katika uwanja wa mtakatifu Petro.
Baadhi ya watalii walisikika wakisema kwamba wamefika
katika uwanja huo kumuaga na kumtakia mema na zaidi ya yote, mtalii kama Amy Champion
aliyetokea Uingereza alisema inahitaji ujasiri kufanya kazi ya Papa na vile
vile wakati unapoamua kuachia ngazi.
Kuanzia Jumapili jioni Papa hatoweza kuonekana tena mbele ya hadhara
katika kipindi cha wiki nzima, ambacho kanisa mjini Vatican linaanza kipindi
maalum cha maombi na tafakari.
Jumapili ya jana uongozi wa mji wa Roma uliongeza usafiri
wa mabasi na treni za chini kwa chini ili kusaidia kukabiliana na msongamano wa
watu waliokuwa wanamiminika kuelekea Vatican pamoja na kutoa usafiri bure wa
mabasi madogo kwa ajili ya watu wakongwe na walemavu.
Papa Benedict
aliushtua ulimwengu wiki iliyopita kwa kutangaza anajiuzulu kuanzia Februari
28, kitendo ambacho hakijawahi kushuhudiwa na kanisa hilo kwa kipindi cha miaka
600.
Wakati Makadinali wakitazamiwa kumchagua mrithi wake mpya
katika kikao maalum cha siri, Papa Benedict
mwenye umri wa miaka 85 atakuwa katika mapumziko na kufanya ibada katika makazi
ya kanisa huko Kusini mashariki mwa mji wa Roma.
Baada ya wiki kadhaa anatazamiwa kuhamia kwenye makaazi
mengine yaliyoko kwenye eneo la Vatican ambako ataishi maisha ya kitawa.
Makao makuu ya kanisa Katoliki mjini Vatican hayajatangaza tarehe ya
kuanza kwa kiao cha siri cha kumchagua kiongozi mpya lakini yametangaza kwamba
kikao hicho huenda kikafanyika mapema kabla ya Machi 15 na tarehe hiyo mpya
inaweza kutangazwa chini sheria za sasa za kanisa.
Papa atahitajika kutia saini juu ya tarehe hiyo kitendo
ambacho kitakamilisha kabisa kipindi chake cha takriban miaka 8 ya uongozi wa
kanisa.
Wakati huohuo tayari Makadinali wameshaanza kuwasili Roma
kuanza kipindi cha kujadiliana kwa mujibu wa sheria za kanisa kuamua ni kina
nani walio wagombea wenye nafasi nzuri ya kuchukua wadhifa huo wa Papa.
Askofu Mkuu Robert Sarah mzaliwa wa Guinea, ambaye ni Kadinali
anayeongoza ofisi ya misaada ya Vatican amewaambia waandishi wa habari kwamba
viongozi wa kanisa watapaswa kumchagua Papa mpya kwa utulivu na kuaminiana.
No comments:
Post a Comment