Habari za Punde

                      STATE HOUSE ZANZIBAROFFICE OF THE PRESS SECRETARY
                                                         PRESS RELEASE

                                         
                                               TARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesifu azma ya Jumuiya ya Al-Youseif ya kuja kuekeza  hapa Zanzibar.
Dk. Shein aliyasema hayo wakati alipokuwa na mazungumzo na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Sheikh Al-Yousef huko Ikulu mjini Zanzibar na kutumia fursa hiyo kwa kumpongeza kiongozi huyo kwa azma yake hiyo.
Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alisema kuwa hatua hiyo itasaidia katika kuimarisha sekta ya uekezaji hapa nchini sambamba na kukuza uchumi na kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo ufugaji, kilimo na hata kukuza sekta ya ajira. Aidha, Dk. Shein alitoa pongezi kwa Jumuiya ya  Al- Youseif kwa azma yake ya kuunga mkono juhudi za Serikali anayoiongoza katika kuwasaidia wanawake kwa kuanzisha benki itakayotoa mikopo kwa ajili ya wanawake pekee.
 
Alisema kua hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuwasaidia wanawake katika juhudi za kupambana na umasikini na kuweza kuinua kipato chao cha maisha.
 
Dk. Shein alieleza kuwa miongoni mwa azma na malengo yake ilikuwa ni kuhakikisha kuwa wanawake wanasaidiwa na kuungwa mkono katika juhudi zao za kupambana na umasikini kwa kuanzishwa benki ambayo itakuwa maalum kwa kuwapa wanawake huduma hizo za mikopo ya fedha.
 

Pamoja na hayo, Dk. Shein alimueleza Sheikh Al-Yousef kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itahakikisha inaweka mazingira mazuri katika sekta ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mradi anaotaka kuanzisha unaenda vizuri.
 
Nae Sheikh Al-Yousef alimueleza Dk. Shein kuwa lengo na madhumini ya Jumuiya yake ni kuekeza kwa kuanzisha mradi wa kuzalisha mayai ya kuku, ngombe na wanyama wengine, mradi ambao unatarajiwa kuzalisha mayai milioni moja ya kuku kwa siku.
 
Alisema kuwa tayari hatua za awali zimeshaanza kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuleta mashine kadhaa sambamba na kutafuta soko zaidi nje ya Zanzibar. Pia, alitumia fursa hiyo kwa kuishuruku Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kumtengea eneo la ardhi kwa ajili ya kuendesha mradi huo.
 
Aidha, Sheikh Al-Youseif alimueleza Dk. Shein kuwa amekusudia kuanzisha mradi wa kuchimba visima 80 Unguja na Pemba na kuahidi kuleta mashine mpya, kubwa na za kisasa kwa ajili ya kuchimbia visima.
Alieleza kuwa mashine hizo za kuchibia visima zitakuwa maalum pamoja na pampu za kisasa za kusukumia maji kutoka visimani ambazo zitakuwa na nguvu kubwa ya kusukumia maji.
 
Kwa upande wa Benki ya Wanawake, Sheikh Al-Youseif alisema kuwa mtaji maalum utawekwa na Jumuiya yake kwa ajili ya kuwasaidia wanawake watakaowekwa katika  makundi maalum ambapo utawahusisha wanawake wakiwemo wajane, vizuka, vijana, wajasiriamali na wanawake wengineo.
 
Pia, Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Al-Youseif, alieleza azma yake ya kuendelea na mradi mkubwa wa maji huko kisiwani Pemba katika kijiji cha Kiuyu na maeneo mengineyo.
 
Sheikh Al-Youseif alimueleza Dk. Shein azma yake ya kujenga nyumba 400 za mkopo nafuu huko kisiwani Pemba kwa ajili ya wananchi ambapo kwa hivi sasa tayari taratibu za awali zimeanza kuchukuliwa.
 
Sambamba na hayo, Sheikh Al-Youseif alipongeza juhudi za Dk. Shein katika kuimarisha amani, utulivu na maendeleo hapa nchini na kusisitiza kuwa sifa hizo zimekuwa zikizungumzwa duniani kote na ndio miongoni mwa sababu zilizompelekea kuja kuekeza Zanzibar.
 
 Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar                  

27-2-2013                

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.