Na Mwandishi
maalum, Kenya
WAGOMBEA wa
urais nchini Kenya wameingia katika wiki ya lala salama ya kampeni, huku kila
mmoja akitangaza kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya uchumi, ajira na
viwanda nchini humo.
Ushindani mkubwa
upo kati ya mgombea wa muungano wa CORD, Waziri Mkuu, Raila Odinga na mpinzani
wake mkubwa, mgombea wa muungano wa Jublee, Naibu Waziri Mkuu, Uhuru Kenyatta.
Akiwa mjini
Mombasa, Odinga aliwambia wafuasi wake kwamba ana kila sababu ya kushinda
katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo na kusema serikali yake itaimarisha
huduma za elimu kwa kuhakikisha wanafunzi wote wanasoma bure hadi sekondari
ya upili.
Aidha ameahidi
kuimarisha sekta ya ajira, kuboresha uchumi wa Kenya, kuimarisha sekta ya
kilimo na viwanda.
Odinga ambae
anaungwa mkono na idadi kubwa ya vijana, alisema uchumi wa Kenya utajengwa upya
katika kipindi cha miaka mitano cha serikali yake.
Kenyatta kwa
upande wake, akiwa mjini Nyeri aliwahakikishia Wakenya maendeleo bora ya
kiuchumi, kupunguza pengo la umaskini na kuboresha maisha ya wananchi.
Alisema serikali
yake itatoa kipaumbele kwa vijana kujiajiri na kuajiriwa katika sekta za umma
na binafsi pamoja na kupanua wigo wa uimarishaji viwanda.
Aliahidi
kusimamia amani na umoja wa Wakenya na kusisitiza kuwa uchaguzi huo utafanyika
kwa misingi amani na utulivu.
Kura ya hivi
karibuni ya maoni inaonesha kuwa wapiga kura wenye umri wa zaidi ya miaka 51
wanampendelea zaidi Kenyatta kuliongoza taifa hilo lenye uchumi mkubwa Afrika
Mashariki ilhali mwenzake wa Cord Raila Odinga anaungwa mkono zaidi na vijana.
Odinga na
mgombea wake mwenza Kalonzo Musyoka wanaungwa mkono na asilimia 58 ya vijana wa
umri wa kati ya miaka 18 na 20 akilinganishwa na Kenyatta na mgombea mwenza
William Ruto wanaoungwa mkono na asilimia 32 ya vijana.
Kijinsia, kura
tofauti ya maoni iliyofanywa na kampuni ya Strategic Africa, ambayo pia utafiti
wake ulidhaminiwa na kampuni ya Nation Media Group inaonyesha vyama vya Restore
and Build Kenya (RBK) na Narc Kenya vinaungwa mkono zaidi na wanawake kwa
asilimia 62 na 60.
Nao wanaume
wengi zaidi wanaunga mkono muungano wa Eagle, asilimia 61.4 ukifuatwa na Cord
(60.5), Amani (57.9) na hatimaye Jubilee (57.2).
Pia inaonekana
Profesa James Ole Kiyiapi wa RBK anaungwa mkono na wanawake wengi zaidi kwa
asilimia 85.7 dhidi ya asilimia 14.3 ya wanaume.
Wakati huo huo
mgombea urais wa muungano wa Cord, Raila Odinga, amelalamika kwamba baadhi ya
familia katika Kaunti ya Nakuru zimetishiwa kuondoka eneo hilo kabla ya
uchaguzi mkuu wa Machi 4.
Aliwaonya
wanaotoa vitisho na kuziambia familia hizo kutohama.
“Usiache nyumba yako ukipokea vitisho vya aina
hiyo. Serikali itakulinda,” alisema Odinga akihutubia mkutano wa kampeni katika
uwanja wa Afraha, mjini Nakuru.
Lakini Mkuu wa
Mkoa wa Rift Valley, Osman Warfa,
alisema hakuna aliyetishwa kuhama, huku akisema baadhi ya wafanyakazi wa
mashamba ya maua katika eneo la Naivasha walikuwa wakielekea walikojiandikisha
kupiga kura ili kushiriki uchaguzi huo.
“Wanaenda walikojisajili kupiga kura na ndio
maana wanaondoka,” alisema Warfa.
Mwenyekiti wa
Ford Kenya Moses Wetang’ula alikuwa wa
kwanza kudai baadhi ya watu walitishwa kuhama Nakuru.
“Kuna watu
wanaotisha wengine kwamba watafurushwa makwao wakisema maisha yao yamo
hatarini. Wanawaambia wahame Nakuru,” alisema.
Warfa aliwaonya
wanasiasa dhidi ya kujadili jambo hilo wakati huu kwa sababu mkoa huo wakati wa
uchaguzi mkuu hukumbwa na ghasia.
Mkuu wa mkoa
aliongeza kwamba kamati za usalama za wilaya zinajadili jambo hilo.
Katika mkutano
huo wa kampeni Odinga aliahidi kutatua matatizo ya ardhi akichaguliwa kuwa rais.
Alisema
inasikitisha kuona watu waliofurushwa makwao kwenye ghasia za baada ya uchaguzi
wa 2007 wanahangaika katika kambi za wakimbizi ilhali baadhi ya viongozi wa Muungano wa Jubilee
wana zaidi ekari 500,000 za ardhi.
Mgombea mwenza
wa Odinga, Kalonzo Musyoka alisema serikali ya Cord itahakikisha masomo bila
malipoi kuanzia shule ya chekechea hadi upili.
Wakati huo huo
jana wagombea hao walishiriki katika mjadala wa mwisho ambao uligusia masuala
matatu muhimu ya uchumi, rasilimali na usimamizi wa rasilimali,sera za
ushirikiano na mataifa ya kigeni.
Kuna hofu kwamba
huenda upigaji kura ukachelewa kukamilika kwa wakati kwa sababu wapiga kura
wengi hawajaelewa utaratibu utakaotumika uchaguzini na watahitaji dakika tano
kila mmoja kufanya hivyo.
No comments:
Post a Comment