Habari za Punde

Wananchi Ziwani wapinga kundi la vijana linalohamasisha liwatwi



Na Abdi Suleiman, Pemba
WANANCHI wa Jimbo la Ziwani Mkoa wa Kusini Pemba, jana walifunga safari hadi zilipo ofisi za Wizara ya Katiba na Sheria Pemba kwenda kuwasilisha malalamiko yao juu ya kuwepo kundi la vijana linalopita vijiji mbali mbali vya jimbo hilo, kutangaza na kueneza madhebu ya shia, ambayo wao wanayapinga vikali.
Wakizungumza mara baada ya kufika wizarani hapo, wananchi hao kike kwa kiume, walisema vijana hao wamekuwa wakihamasisha ndoa za muda mfupi (Muta’aa) na kulawiti.
Aidha walisema vijana hao wamekuwa wakiitafsiri wapendavyo Quran pamoja na hadithi za Mtume (SAW).

Walisema kuhalalisha liwati na ndoa za muda mfupi ni kinyume na maarisho ya Mwenyezi Mungu na kusema tayari kuna baadhi ya watoto wao wameanza kufuata madhehebi hayo.
 “Wanapita kila kijiji na kuhalalisha ndoa za muda mfupi na kulawitiana kwa watu walio kwenye ndoa vitendo ambavyo ni haramu katika imani ya kiislamu,” walisema.

Walionya kuwa vijana hao wasipopigwa vita, wanaweza kusababisha udhalilishaji mkubwa wa kijinsia na kingono hasa kwa wanawake walio kwenye ndoa.
Mmoja kati ya wananchi hao,Tatu Khamisi Bakari,  aliiomba wizara ya Katiba kupitia ofisi ya Mufti kulitolea ufafanuzi suala hilo na kuwaondosha haraka vijana hao kabla hawajachukua hatua za kuwaondoa kwa nguvu, jambo ambalo linaweza kusababisha vurugu.
Mohammed  Mussa  Juma,  ambae ni  mwanakijiji  wa  Ziwani, alisema vijana hao wamekuwa wakiwatumia zaidi watoto walio na umri kuanzia miaka 15-20, ambapo huwachukua kutoka kwa wazazi wao na kuwasafirisha hadi Dar es Salaam kwa madai ya kwenda kuwafundisha uislamu lakini badala yake huwafundisha ushia.
Alisema tayari kuna vijana wengi wa kijiji hicho walioko Dar es Salaam kufundishwa madhehebu hayo, na kuiomba serikali kufanya liwezekanalo kuhakikisha vijana hao wanarejeshwa.
Mkuu wa Makosa ya Jinai na Upelelezi wa polisi, Wilaya ya Chake Chake, Ali Mzee, alisema hitilafu za kidini zinashughulikiwa na ofisi ya Mufti, hivyo  aliwataka wananchi wa Ziwani, kuwa tayari  kutetea haki zao ofisi ya Mufti na kuepuka  kufanya vitendo vinavyoweza kusababisha vurugu.
Alisema madhehebu ya Suni na Shia, yote ni madhehebu ya kidini hivyo hawapaswi kutafarukiana.
Naye Kaimu Msaidizi Mufti Pemba, Abrahamani Abdalla Naamani, amewahidi wananchi hao kwamba madai  yao yatafikishwa katika ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, kwa kufanyiwa kazi.
Aliwasisitiza wananchi hao kuwa na umoja na mshikamano, katika kulipatia ufumbuzi tatizo hilo, na wasichoke kufuatilia.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.