Na Rajab Mkasaba, Ikulu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, amemtumia salamu za rambi rambi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Anne Makinda kufuatia kifo cha Mbunge wa Jimbo la Chambani, Pemba Mhe. Salim Hemed Khamis.
Katika salamu hizo za rambi rambi, Dk. Shein alisema kuwa amepokea kwa mshituko na huzuni kubwa taarifa ya kifo cha ghafla cha Mhe. Salim Hemed Khamis, Mbunge wa Chambani Pemba.
Salam hizo zilieleza kuwa yeye mwenye binafsi pamoja na wananchi wa Zanzibar wamesikitishwa na kuhuzunishwa sana na kifo hicho.
“Tunakuomba utufikishie salamu zetu za rambirambi kwa Waheshimiwa Wabunge na jamaa wote waliohusika na msiba huu mkubwa....Kifo cha Mheshimiwa Salim ni pigo kwa watu wa Jimbo la Chambani Pemba na taifa zima kwa jumla”,alieleza Dk. Shein.
Salamu hizo zilieleza kuwa kutokozewa na maradhi akiwa kazini ni kielelezo cha kutosha cha sifa ya uchapakazi wake Marehemu Salim.
“Mimi namfahamu Mheshimiwa Salim kuwa ni kiongozi mahiri, aliyependa kazi, mvumilivu na aliekuwa na mashirikiano mazuri na wenzake”,alieleza sehemu ya salamu ya rambirambi hizo.
Aidha, kupitia salamu hizo za rambirambi, Dk. Shein alimuomba MwenyeziMungu kuwapa moyo wa subira na ubvumilivu wakati huu wa msiba, Wabunge wenzake, familia, marafiki, ndugu pamoja na wananchi wote wa Jimbo la Chambani na nchi yote kwa jumla.
Salamu hizo ziliendelea kumuomba MwenyeziMungu kumpa rehma na kumjaalia makaazi mema peponi Marehemu Salim Hemed, Amin.
No comments:
Post a Comment