Na Maryam Nassor, Pemba
MADAKTARI wa hospitali ya Chake Chake kisiwani Pemba, wameilalamikia wizara ya Afya, kwa kutowalipa posho zao za kufanyakazi muda wa ziada huku wenzao wa Unguja wakipatiwa posho hizo.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi hospitalini hapo, madaktari hao, walisema wao pia wanafanyakazi katika mazingira magumu na wanaitwa muda ambao si wa kazi, lakini hawalipwi posho.
Madaktari hao, ambao hawakutaka kuandikwa majina yao gazetini, walisema Zanzibar ina Wizara moja tu ya afya, iweje wenzao wa Unguja walipwe, lakini wao kukosa haki hiyo?.
Walieleza kuwa baadhi yao, wamekuwa wakikosa hata mapunziko kutokana na kuitwa mara kwa mara hospitali hasa pale wanapotokea wagonjwa wa dharura au kesi kubwa.
“Ukifika nyumbani unategemea ukae na watoto na kujipunzisha, ghafla unaona simu inapigwa unahitajika hospitali, huwezi kukataa maana tunatoa huduma kwa ndugu na jamaa zetu, lakini basi hata sabuni ya ziada hatupewi?,” alihoji mmoja wa madakatari hao.
Aidha walisema suala hilo limekuwa likisababishwa na uhaba wa madaktari
na siku zote wamekuwa wakihimizwa kuongezewa madaktari, lakini wizara bado inaendelea kukaa kimya.
“Uhaba wa madaktari unatusababishia sisi tuliopo tufanye kazi kwa muda mrefu tena bila ya kupatiwa posho, kama wenzetu walioko Unguja, inakuwaje wakati sisi sote ni wafanyakazi wa nchi moja?,”walihoji.
Akijibu hoja hizo kwa njia ya simu, Afisa Mdhamini wa Wizara hiyo Pemba, Mkasha Hija Mkasha, alikiri kuwa madaktari wa Unguja wamekuwa wakipata posho na Pemba kukosa, kutokana na mgao mdogo wa fedha wanaopokea kutoka wizarani.
“Ni kweli madakatari wa Pemba katika miezi ya hivi karibuni, wamekuwa wakikosa posho zao za muda wa kazi wa ziada, lakini serikali hilo inalielewa na iko mbioni kutekeleza hayo, na kuanzia mwenzi ujao baadhi yao wataanza kulipwa,” alisema.
Kwa upande wake, Daktari Dhamana wa hospitali ya Chake chake, Yussuf Hamad Iddi, alisema ipo haja kwa wafanyakazi kulipwa posho zao, ili kuwatia hamu na hamasa ya kufanya kazi.
“Ni vyema kwa serikali kupitia wizara yetu ya afya, kuwalipa madaktari posho zao, ili kuwatia hamu na hamasa ya kufanya kazi, maana bila ya kuwapa posho utendaji wao wa kazi utashuka,” alisema.
Wiki iliopita Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote za Pemba, walikuwa na kikao kizito na uongozi wa Wizara ya Afya Pemba, kutokana na kukithiri kwa malalamiko ya wananchi, juu utendaji mbovu wa madaktari.
serikali inazo pesa kuwalipa wabunge na wawakilishi kwenda kukoroma na kulala bungeni eti sitting allowance wakati hizo ni kazi zao , lakini hawana pesa kuwalipa madaktari , manesi na walimu
ReplyDelete