Habari za Punde

Matangazo ya digitali ya ZBC ni huduma si biashara - Waziri


Na Mwashamba Juma
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar, Said Ali Mbarouk amesema matangazo ya digital yanayorushwa na Tume ya Utangazaji Zanzibar (ZBC) hayapo kibiashara bali lengo ni kuwapatia huduma wananchi wake ili kuendana sambamba na teknolojia mpya.

Akizungumza na waandishi wa habari huko katika ukumbi wa Bwawani, wakati wa ufunguzi wa matangazo ya digitali kwa ZBC ambayo Waziri Mbarouk alisema yameanza rasmi jana, kuanza kwa matangazo hayo hakutokuwa na sababu ya kuzima moja kwa moja matangazo ya mfumo wa zamani wa analogia bali yataendelea hadi ving’amuzi vienee nchi nzima.

Alisema tayari miundombinu ya mfumo wa digitali imeshawekwa nchi nzima likiwemo jengo lililopo Rahaleo mjini Zanzibar, miundombinu ya digital kwenye mnara wa Masingini, Wilaya ya Kaskazini Unguja kwenye mnara wa Nungwi, Mnara wa Kichunjuu, mnara wa Zantel Kizimkazi-Muyuni, Mnara wa Mkoroshoni, pamoja na mnara wa Konde vilima vitatu.

Akitoa ufafanuzi wa kupanda kwa bei ya ving’amuzi kutoka bei ya shilingi 50,000 kama ilivyotangazwa awali na kufikia shilingi 73,000, Waziri huyo alisema bei ya ving’amuzi itaendelea kuwa 50,000 ili kuwapa unafuu wananchi na badala yake watalipa 8,000 ikiwa ni ada ya mwezi wa tatu na 15,000 fedha za usajili na uunganishwaji.

Alisema Serikali haiko kwa ajili ya kufanya biashara ya matangazo hayo, bali iko kwa ajili ya kuwapa huduma zinazostahili wananchi wake na ndio maana bei za ving’amuzi vyake ni tofauti na taasisi nyengine zinazoendesha matangazo hayo kibiashara.

Waziri Mbarouk alisema Zanzibar imeingia rasmi katika matangazo ya digital ili kwenda sambamba na makubaliano yaliyofikiwa na nchi za Afika Mashariki kwa kuzima matangazo ya zamani ya mfumo wa analojia mwanzoni mwa mwaka huu.

Akizungumzia suala la ukatikaji wa matangazo kabla ya wakati yanayochangiwa na matumizi ya wananchi, Waziri Mbarouk alisema huduma za ving’amuzi vya ZBC zipo kwa ajili ya Wananchi, hivyo Serikali imewalazimisha kampuni inayosimamia mradi huo kuhakikisha matangazo hayakatwi hadi kwa mwezi uliolipiwa na mwananchi, sambamba na kudhibiti tatizo la kukatika kwa umeme wakati matangazo yakiendelea.

Aidha Waziri Mbarouk alisema Wizara yake ililazimika kuingia mkataba na kampuni ya Agape kutokana na kutimiza masharti waliokubaliana ikiwa ni pamoja na Miundombinu yote ya matangazo hayo kuwa ni mali ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, sambamba na vifaa vya miundombinu hiyo kutokea Ujerumani.

Matangazo ya digital ya ZBC yanasimamiwa na kampuni ya Agape ya Dar es Salaam kwa mashirikiano na kampuni ya Afrika Kusini, awali makampuni kadhaa yalijitokeza kusimamia matangazo hayo lakini yalishindwa kutokana na vigezo na makubaliano ya Serikali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.