Na Khamis Amani
SERIKALI ya mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, imeviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kusimamia vyema sheria za nchi ili kuimarisha nidhamu ndani ya mkoa huo, pamoja na kuurejeshea hali ya kuheshimu na kutii sheria.
Serikali ya mkoa imefahamisha kuwa, siku za hivi karibuni kumejitokeza baadhi ya watu wenye nia ya kuidhoofisha hali hiyo, ili hatimae waiondoe haiba kwa kufanya vitendo kinyume na mila, hulka na desturi za Mzanzibari.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa mkoa huo, Abdallah Mwinyi Khamis, katika taarifa yake kwa wananchi kupitia vyombo vya habari kufuatia kuibuka kwa vitendo mbali mbali vya uvunjifu wa sheria vinavyofanyika ndani ya mkoa.
Katika taarifa hiyo, Mkuu wa mkoa alisema kwamba mkoa wa mjini magharibi una asili ya kuwa ni mahali patulivu, penye historia ya haiba nzuri na kuvutia kila mtu jambo ambalo huwafanya walio wengi kupatamani ama kuishi au angalau kutembelea.
Alifahamisha kuwa, hali hiyo hivi sasa imeonekana kudhoofishwa kwa makusudi na wakorofi wachache, licha ya kuwepo kwa jitihada mbali mbali zinazochukuliwa na Baraza la Manispaa la Zanzibar, Halmashauri ya wilaya ya Magharibi na taasisi mbali mbali halali za serikali za mitaa katika kukabiliana na kuchukua hatua za kudhibiti kwa lengo la kuondoa vitendo hivyo viovu.
"Serikali ya mkoa imevumilia hali hiyo muda mrefu kwa lengo la kuwapa elimu na kutoa fursa kwa wananchi wote ya kutii sheria bila ya shuruti, lakini imedhihirika kuwa wananchi hao wachache wametumia muda huo kwa kubeza, kudharau na hata kukejeli taaluma inayotolewa kwao na adhabu hafifu zilizochukuliwa wakati uliopita," alisema Mkuu wa mkoa.
Kutokana na hali hiyo, alisema serikali hivi sasa imejidhatiti na kuanza utekelezaji wa zoezi la kupambana na ukiukwaji wa sheria ikiwemo suala zima la uzururaji ovyo wa wanyama ndani ya mkoa huo.
"Nachukua fursa hii kwa mara ya mwisho kuwaomba wananchi wote wa mkoa huu na wale wa mkoa jirani, ambao muda wao mwingi wanatekeleza shughuli zao za kiuchumi na maendeleo katika mkoa huu kuondoa mifugo yao katika eneo la mji wa Zanzibar," alitanabahisha.
Kwa upande wa wajasiriamali pamoja na watumiaji wa vyombo vya moto na baiskeli, aliwataka kufuata sheria zilizopo kama vile sheria za mifugo, mazingira, usafi wa mji, barabara na nyenginezo ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria dhidi yao.
Alisema kwamba, serikali ya mkoa imedhamiria kwa dhati kabisa kuimarisha usimamizi wa sheria kwa kuendelea kwa namna yake kudhibiti aina yoyote ile ya uvunjifu wa sheria kupitia mkakati wake uitwao "Operesheni rejesha nidhamu 2013".
Alitanabahisha kuwa mnyama yoyote atakaekamatwa atahifadhiwa eneo maalumu na kutunzwa kwa muda, na endapo mmiliki wake hatajitokeza ndani ya muda uliopangwa kwa mujibu wa sheria namba 11/1999 za mifugo na kanuni za Baraza la Manispaa, atataifishwa na kuwa mali ya umma na hatarejeshwa tena.
"Sasa naomba kutamka rasmi kwa niaba ya serikali ya mkoa kuwa sasa basi, kwa taarifa hii naviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kutekeleza "operesheni rejesha nidhamu 2013".
Katika operesheni hiyo tayari ng’ombe 40, Kondoo wane na Punda wawili ambao walionekana wakizurura tayari wamekamatwa.
Wilaya ya mjini ina ng’ombe, mbuzi,kondoo na punda wa gari 391,000 ambapo kati yao 152,000 ndio wanaozurura.
No comments:
Post a Comment