STATE HOUSE ZANZIBAROFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 7.3.20113
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameuambia ujumbe wa Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC) kuwa Tanzania imejiandaa vyema kushiriki katika awamu ya pili ya utekelezaji wa miradi chini ya ufadhili wa Mfuko huo.
Dk. Shein ameuambia ujumbe huo ulioongozwa na Mkuu wa Utumishi wa MCC Bwana Steve Kaufmann kuwa Tanzania inajivunia heshma kubwa iliyopewa na MCC kwa kuwa moja ya nchi chache na za mwanzo kushirikishwa katika awamu ya pili ya mradi huo.
“tumefurahi sana kuwa nchi yetu imepewa sifa ya kuwa ya mfano katika utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na Mfuko wa Changamoto za Milenia hivyo kupewa heshma ya kuwa miongoni mwa nchi za mwanzo kushirikishwa katika awamu ya pili ya mradi huu”alieleza Dk. Shein.
Rais wa Zanzibar aliuhakikishia ujumbe huo kuwa uzoefu uliopatikana katika kutekeleza miradi ya awamu ya kwanza utatumika ili kuhakikisha kuwa miradi itakayotekelezwa katika awamu ya pili inafanyika kwa ufanisi na kutoa mafanikio zaidi.
“Ninakuhakikishia kuwa timu yetu iko imara na iko tayari kwa mashauriano ya awamu ya pili ya mradi…ninaamini kuwa uzoefu walioupata wakati wa awamu ya kwanza itakuwa hazina kubwa katika kufanikisha miradi ya awamu ya pili” Rais alisisitiza.
Katika mazungumzo hayo Dk. Shein aliueleza ujumbe huo kuwa Serikali na wananchi wa Tanzania wamefarijika sana na ufadhili wa Mfuko huo na kutolea mfano kwa Zanzibar mradi wa kujenga waya mpya wa umeme unaounganisha Zanzibar na gridi ya taifa ya Tanzania Bara, Ujenzi wa barabara kisiwani Pemba pamoja na utekelezaji wa Mpango wa Kupunguza Umasikini kwa Zanzibar –MKUZA.
Naye Bwana Kaufmann alisema kuwa Mfuko wa Changamoto za Milenia pamoja na Serikali ya Marekani imeridhishwa na kufurahishwa na utekelezaji wa miradi iliyo chini ya mfuko huo na ndio maana Tanzania imepewa fursa ya kwanza kushirikishwa katika awamu ya pili ya utekelezaji ya miradi ya mfuko huo.
“Tanzania imekuwa nchi ya mfano mzuri wa mafanikio ya miradi ya MCC na hapa Zanzibar utekelezaji nao umekwenda vizuri kwa hiyo Tanzania imepewa fursa tena ya kushiriki awamu ya pili ya mradi… hilo ni jambo zuri kwa mustakabala wa ushirikiano wetu na Tanzania kwa manufaa ya wananchi wa nchi zetu”alieleza bwana Kaufmann.
Bwana Kaufmann alibainisha kuwa mashauriano kuhusu miradi ya awamu ya pili hadi utekelezaji utachukua miaka miwili lakini akasifu hatua ya Tanzania katika maandalizi ya mashauriano hayo ambapo tayari imeshaunda timu yake kwa ajili hiyo.
Katika mazungumzo hayo Bwana Kaufmann alifuatana na Naibu Rais wa MCC Kanda ya Afrika Mashariki Bwana Andrew Mayok, Bwana Matthew Kavaragh Naibu Mkurugenzi Mkaazi wa Mfuko huo Tanzania na Afisa Mkuu wa Mfuko huo kwa Zanzibar bwana Jefferson Smith.
Said Ameir, Ikulu Zanzibar.
No comments:
Post a Comment