Ombi la kutaka viongozi hao Jumiki wafunguliwe mashtaka upya limewasilishwa
na Mwendesha Mashitaka wa Serikali kutoka ofisi ya DPP, Mohamed Ali Mohammed, na
kusababisha kesi hiyo kukwama kuanza kusikilizwa jana mjini Zanzibar.
Alisema kwamba kulingana na ushahidi unaotarajiwa kutolewa katika kesi hiyo
kuna umuhimu mkubwa wa hati ya mashtaka ya awali kubadilishwa kwa washtakiwa
hao.
“Mheshimiwa tumeamua kubadilisha hati ya mashtaka kulingana na ushahidi wa
kesi tuliyokuwa nao,” alisema.
Hata hivyo alisema upelelezi wa kesi hiyo tayari umekamilika na upande wa
mashtaka uko tayari kuleta mashahidi kabla ya kutolewa hukumu ya kesi hiyo.
Hata hivyo maombi hayo ya kubadilisha hati ya mashtaka yalipingwa vikali na
mawakili wa upande wa utetezi, Salum Toufiq na Abdalla Juma ‘Kaka’.
Wakili Salum alisema kwamba kesi hiyo imefunguliwa kipindi kirefu bila ya
kusikilizwa na kwa mujibu wa sheria inapaswa kufutwa na wateja wake kuachiwa
huru.
Alisema kwamba kumbukumbu zinaonyesha wateja wake walifikishwa mahakamani
Aprili mwaka jana lakini hadi sasa kesi imekuwa ikichechemea kuanza kusikilizwa
na kuchelewesha haki ya kisheria dhidi ya watenja wake.
Upande wake Wakili Abdalla Juma alisema kwamba jambo la kushangaza upande wa
serikali unataka kubadilisha hati ya mashtaka wakati mahakama ikiwa imepanga
tarehe ya kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo.
Hata hivyo akijibu hoja za mawakili, mwendesha mashtaka katika kesi hiyo,
Mohamed Ali, aliipinga hoja ya kutaka kesi kufutwa kwa sababu washtakiwa namba 6
na 7 ndiyo walisababisha kuchelewa kuanza kusikilizwa kesi hiyo baada ya mara
mbili kushindwa kufika mahakamni na kushindwa kutolewa ushahidi wa kesi
hiyo.
Alisema washtakiwa hao walishindwa kufika mahakamani Desemba 27 na Julai 6
mwaka jana wakati mashahidi wa kesi wakiwa tayari wameitwa kutoa ushahidi
wao.
Baada ya Hakimu Khamis Jafari kusikiliza hoja zilizotolewa, alisema kwamba
atatoa uamuzi kuhusu hati ya mashtaka kubadilishwa au la leo kabla ya mashahidi
kuanza kutoa ushahidi.
Viongozi hao wa Uamsho awali walifunguliwa shtaka kufanya mkusanyiko usio
halali kinyume na sheria no 6 ya mwaka 2004 ya sheria ya Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar.
Imeelezwa katika kesi hiyo kuwa washtakiwa hao wanadaiwa kuwa Mei 26 mwaka
jana, saa 6.30 waliandaa maandamano yasiyo na kibali kuanzia maeneo ya Kinazini,
Msikiti, Mabuluu, Michenzani hadi Kwa Biziredi kinyume cha sheria.
Washtakiwa hawa ni Masheikh Farid Hadi Ahmed, Mussa Juma Issa, Mbarouk Saidi
Khalfan, Haji Sadifa Haji, Suleman Juma Suleiman, Fikirini Majaliwa, Abdallah
Said Ali na Mbarouk Saidi Khalfan na walikana mashtaka hayo.
Chanzo - Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment