Habari za Punde

ZFA yajikosha


 Yawalisha pipi wadau wanaotaka mageuzi
 
Makamu asema muda wa kuondoka bado
 
  Na Abdi Suleiman, Pemba
 
MAKAMU Rais wa Chama cha Soka Zanzibar ZFA anayefanyia kazi ofisi ya Pemba Ali Mohammed Ali, amesema muda wa kuvunja uongozi wa chama hicho haujafika kama wadau wengi wa soka nchini wanavyotaka.
 
 Akizungumza na mwandishi wa habari hizi juu ya ajenda zilizojadiliwa katika kikao cha kamati tendaji ya ZFA Pemba na viongozi wa juu wa chama hicho Jumamosi iliyopita katika ukumbi wa uwanja wa Gombani, Mohammed amewataka wadau hao wavute subira kwani mambo mazuri yako njiani.
 
Maelezo hayo yamekuja, huku kukiwa na kila dalili kuwa, serikali iko katika hatua ya kunoa panga ili kuuondoa uongozi wa sasa wa chama hicho na kuunda kamati ya mpito kwa lengo la kuweka mazingira mazuri na kukidhi matakwa ya wadau wa soka nchini.


Alieleza kuwa, kikao chao na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk Machi 22, mwaka huu, hakikuzungumzia haja ya kuufuta uongozi wa chama hicho, bali aliwakumbusha majukumu yao kwa lengo la kurekebisha kasoro zilizopo kwa manufaa ya soka la visiwa hivi. “Ninawashauri wadau wasubiri muda mfupi tu, mabadiliko makubwa yatatokea katika soka la Zanzibar.
 
Tunajipanga kuifanyia kazi hotuba ya Waziri aliyoitoa wakati tulipokutana naye”, alieleza kiongozi huyo.
 
Kwa upande wa katiba, Mohammed alisema pia katika muda mfupi usiozidi miezi mitatu, ZFA imejipanga kuwa na rasimu ya katiba mpya, itakayopelekwa kwa kila mdau, kuiona na kuitolea maoni kabla kupata baraka za kuwa katiba rasmi. “Tunajiandaa kuipeleka rasimu ya katiba kwa wadau wote, na bila shaka itakidhi masharti ya mashirikisho ya soka ya kimataifa, CECAFA, CAF na FIFA.
 
Mbali na ajenda hiyo katika kikao kilichochukua zaidi ya saa tisa, chama hicho pia kilijadili haja kwa viongozi na wajumbe wa chama hicho kushikamana, kuondoa tafauti zao na kufanya kazi kwa maslahi ya Zanzibar, katika kuendeleza mpira wa miguu.
 
Wakati huo huo, uongozi wa ZFA Unguja, uliamua kuufuta mkutano na waandishi wa habari uliokuwa ufanyike jana mchana katika ofisi za chama hicho Kiembesamaki, bila kutoa sababu za hatua hiyo

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.