Na Mwandishi wetu
MAHAKAMA Kuu ya Zanzibar, imewasomea upya mashtaka katika kesi ya jinai namba
9 ya mwaka 2012, viongozi wa Jumuiya ya Mihadhara ya Kislamu (Uamsho).
Akiwasomea mashtaka yao, Mwendesaha Mashtaka wa Serikali, Ramadhan Nasibu,
aliwataja washtakiwa kuwa ni Farid Hadi Ahmed (41) mkaazi wa Mbuyuni, Mselem Ali
Mselem (52) mkaazi wa Kwamtipura, Mussa Juma Mussa (47) mkaazi wa Makadara na
Azan Khalid (48) mkaazi wa Mfenesini.
Wengine ni Suleiman Juma Suleiman (66) mkazi wa Makadara; Khamis Ali Suleiman
(59) (Mwanakwerekwe); Hassan Bakar Suleiman (39) (Tomondo); Ghalib Ahmada Juma
(39) (Mwanakwerekwe); na Abdallah Saidi (48) (Misufini).
Mashtaka waliyosomewa ni kuharibu mali, uchochezi, ushawishi na kuhamasisha
fujo na kula njama ya kufanya kosa.
Kosa la nne linamkabili mshtakiwa namba nne pekee, Azan Khalid, ambaye
anadaiwa kutoa maneno ya matusi kwa Kamishna wa Polisi, kitendo kinachoweza
kusababisha uvunjifu wa amani.
Vitendo hivyo vinadaiwa kufanyika kati ya Oktoba 17 hadi 19 katika maeneo
tofauti katika manispaa ya mji wa Zanzibar ambapo washtakiwa wote walikana
makosa yote.
Mara baada ya kuwasomea mashtaka yao, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, alidai
kuwa upelelezi wa shauri hilo tayari umekamilika.
Hata hivyo aliiomba mahakama hiyo kusubiri kwa kuwa upande wa mashtaka
umekata rufaa katika Mahkama ya Rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu ya
Zanzibzar.
Alidai kuwa iwapo mahakama itaendelea na kesi hiyo inaweza kuifanya Mahakama
ya Rufaa kutoa uamuzi ambao unaweza kuathiri uamuzi wa mahakama hiyo.
Mapema upande wa utetezi ukiongozwa na Salum Taufiq, uliiomba mahakama hiyo
kuwapatia dhamana wateja wao hasa ikiangaliwa kuwa tayari wameshakaa ndani kwa
muda mrefu sasa.
Jaji Fatma Hamid Mahmoud anayesikiliza kesi hiyo alisema kuwa atayachukuwa
maombi ya pande zote mbili na kuyapitia kwa umakini ili baadaye aweze kutoa
uamuzi ulio sahihi.
Kesi hiyo iliahirishwa na watuhumiwa kurudi rumande hadi Machi 27 ambapo
uamuzi wa washtakiwa kupatiwa dhamana au la utatolewa.
Chanzo - Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment